27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Thabo Mbeki atoa somo zito kwa wasomi UDSM

RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki
RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki

Na MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM

RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewakumbusha wasomi kuhusu malengo mazito ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza wakati wa mahafali ya 46 ya UDSM baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa chuo hicho, Mbeki alisema lengo kubwa ilikuwa ni kuzalisha wasomi ili kutatua matatizo yaliyopo katika jamii.

Mbeki alisema lengo la Mwalimu Nyerere ambalo alilitoa mwaka 1963, la kuwa na elimu ya juu iliyojikita kuwapata wataalamu katika nyanja mbalimbali, ambao wangeweza kufanya tafiti na kuyapatia majibu matatizo yaliyopo katika jamii, bado halijatimia.

“Kuna changamoto nyingi kama mabadiliko ya hali ya hewa, kutojua ni namna gani ya kutumia rasilimali za asili, vita, migogoro ya mipaka na mengineyo, lakini yote haya yalitakiwa kutatuliwa na wasomi na ndilo lilikuwa lengo kubwa la kuanzishwa elimu ya juu Afrika,” alisema Mbeki.

Aliwataka wanafunzi wanaohitimu katika fani mbalimbali kutumia elimu zao katika kutatua matatizo yaliyopo katika jamii na kuacha kukumbatia vyeti na kukaa navyo bila faida yoyote.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alitumia fursa hiyo kuaga kuhudhuria kama Makamu Mkuu wa Chuo kwa kuwa muda wake umefikia ukingoni.

“Miaka 10 iliyopita nimekuwa nikihudhuria sherehe hizi tangu mwaka 2006, sherehe hizi ni za mwisho, muda wangu umefikia ukingoni na siku chache zijazo nitakabidhiwa mrithi wa nafasi hii atakayeteuliwa,” alisema Profesa Mukandala.

Alitoa rai kwa wanafunzi waliohitimu kuwa anaamini wameandaliwa vizuri, hivyo jamii inawategemea katika kuleta maendeleo kwa nchi na hata dunia nzima.

Mwanzo wa mahafali hayo rais mstaafu wa awamu ya nne, Kikwete, alisimikwa rasmi kuwa mkuu wa chuo hicho ambapo kuanzia jana ataanza majukumu yake kama Mkuu wa a UDSM.

Profesa Mukandala alisema mwaka huu kutakuwa na jumla ya wahitimu 6,717, ambapo kati yao, 61 watatunukiwa shahada ya uzamivu, 627 shahada za umahiri na 59 stashahada ya uzamili na jumla ya wahitimu 5,968 watatunukiwa shahada za awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles