26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mambo 10 yaliyotikisa bungeni

Na FREDY AZZAH, Dodoma

MKUTANO wa 13 wa Bunge la 11 umeisha juzi huku mambo 10 yakitikisa vikao vya mkutano huo vilivyodumu kwa siku tisa.

Pamoja na mambo mengine mkutano huu ulijadili Mapandekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2019/20, pamoja na kupitisha hati ya dharura ya Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya Mwaka 2018. Aidha suala la Katiba mpya nalo lilijitokeza kwa kujadiliwa kwa mitazamo tofauti na wabunge wa pande zote.

Kwa upande wao wabunge wa upinzani walidai kuwa suala la Katiba mpya limezikwa na viongozi wa awamu ya tano.

licha ya kuwa ndiyo mwarobaini wa demokrasia na maendeleo nchini.

Yamkini madai ya wabunge wa upinzani yametokana na msimamo wa Rais Magufuli alioutoa Novemba Mosi, mwaka huu wakati akizungumza kwenye kongamano la uchumi na siasa lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDSM.

Rais Magufuli aliweka wazi kuwa hayupo tayari kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba na kusema kufanya hivyo ni sawa na kuwapeleka watu walipane posho ilhali kuna masuala mengine ya maendeleo yanayohitaji fedha ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Mchakato wa Katiba Mpya ulizinduliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, na kuundwa Tume ya Ma badiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Bunge Maalumu la Katiba lilipoketi kuliibuka mvutano mkali kati ya wajumbe wa bunge hilo na kusababisha baadhi ya vyama vya upinzani kujitoa ndipo ulipoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA.

“Sasa sifahamu baada ya rasimu ya Jaji Warioba miaka minne iliyopita tunaendelea na hiyo rasimu au tunakwenda kuanza upya. Badala ya kulumbana kwa hayo ya Katiba bora tufanye kazi sasa.

“Watu wameng’ang’ania katiba mpya utadhani ndiyo suluhisho la matatizo yote,”amesema Rais Magufuli

Hata hivyo hoja ya wabunge wa upinzani ilipingwa vikali na wabunge wengi wa CCM waliodai kuwa wabunge wa upinzani wanaibua hoja hiyo ili kumtoa Rais John Magufuli kwenye reli.

Walidai upinzani wanataka viongozi waache kushughulika na suala la maendeleo badala yake wahamie kwenye suala la Katiba ili mwaka 2020 kwenye uchaguzi wapate hoja ya kusema kuwa CCM hawakusaidia nchi kusonga mbele kwenye maendeleo.

Miongoni mwa hoja zilizoibuka katika Bunge hilo ni pamoja na suala la shughuli za kiuchumi yakiwamo maduka kufungwa baada ya saa tano usiku.

Jambo hilo lilisababisha Spika Job Ndugai kuchagiza kwa kusema “wakati mwingine huwa najiuliza, hivi baada ya saa tano serikali haitaki fedha, kwasababu ikishafika saa tano usiku askari wako kila mahali wakilazimisha watu kufunga biashara.”

Sakata la korosho halikuwa nyuma, kwani nalo liliwagawa wabunge wa upinzani na wale wa CCM, ambapo awali wote walikuwa wakilalamikia bei ya zao hilo kuporomoka.

Baada ya uamuzi wa Rais Magufuli kutumia jeshi kuzinunua, wabunge hao waligawanyika huku wale wa CCM wakimpongeza Rais  na upinzani wakidai kuwa hatua hiyo inaondoa imani ya wafanyabiasha nchini.

Walidai pia mfumo alioutumia Rais hauna afya kwa uchumi wa nchi kwa sababu Serikali haitakiwi kufanya biashara, badala yake inatakiwa itengeneze mazingira bora kwa wafanyabiashara.

Pia suala la mauaji ya raia na askari mkoani Kigoma iliibuka ingawa Spika Ndugai, alikatisha hoja hiyo kwa kile alichosema kuwa  madai hayo ni makubwa yanahitaji uthibitisho ili yajadiliwe.

Pia historia ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto, Kabwe kujiuzulu ubunge wake ndani ya ukumbi wa Bunge wakati akiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini wakati wa Bunge la 10 ilijirudia.

Safari hii aliyetumia ukumbi wa Bunge kujiuzulu nafasi yake ni aliyekuwa mbunge wa Temeke kwa tiketi ya Chama cha Wananchi-CUF, Abdallah Mtolea, alidai kuwa hali ya siasa ndani ya chama chake ndiyo imemsukuma kuchukua uamuzi huo.

Suala jingine ni kujiuzulu ubunge kwa Ahamed Katani, Mbunge wa Tandahimba –CUF kisha kukanusha suala nako kulijadiliwa huku wabunge wa vyama vyote na watu wake wa karibu waliamini kuwa mwakilishi huyo alikuwa ajiuzulu siku hiyo hiyo aliyojiuzulu Mtolea.

Kudorora kwa demokrasa kuliwaibua abunge wengi wa upinzani huku wakidai kuwa hali hiyo imesababisha nchi  kunyimwa mikopo na misaada mbalimbali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alilazimika kukanusha madai hayo na kusema kuwa yeye ndiye waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha hana taarifa za wahisani kusitisha misaada ama mikopo kwa sababu yoyote ile.

Kwa upande mwingine suala la watu wenye kipato cha chini kubanwa zaidi kupitia sheria ya huduma ndogo ya fedha ambayo Bunge lilipitisha muswada wake lilitawala mjadala na kuungwa mkono na pande zote.

Wengi walidai muswada huo utaumiza wanachi wengi na Serikali ingetakiwa iwasaidie wananchi hao badala ya kuwaumiza kwa kuwawekea masharti magumu.

Katika mkutano huo, suala la kupiga marufuku ushoga liliibuka huku baadhi ya wabunge wakidai kuwa matamko mbalimbali ya viongozi yanaiweka nchi katika hatari ya kutengwa na ulimwengu.

Mambo mengine yaliyojitokeza kwenye mkutano huo ni pamoja na kusomwa kwa mara ya kwanza kwa Muswada wa Marekebisho wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2018.

Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2018, Muswada wa Hali ya Hewa wa Mwaka 2018 na Muswada wa Mamlaka ya Usimamizi wa Nchi Kavu.

Pia muswada wa Huduma Ndogo ya Fedha wa mwaka 2018 (Micro Finance), ulipitishwa kwa hati ya dharura.

Mbali na miswada hiyo, mkutano huo pia uliidhinisha maazimio matatu ambayo ni Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hati miliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea, Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kibayolojia na la Mwisho ni Mkataba wa Takwimu wa Afrika.

Pia wabunge nane walikula kiapo cha uaminifu ambao ni Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga), Zuberi Kuchauka (Liwale) na Timothy Mzava (Korogwe Vijijini), wote wa CCM watakula kiapo cha utii leo.

Wengine ni Paulina Gekuli (Babati Mjini), James Ole Miliya  (Simanjiro), Marwa Chacha (Serengeti) na Joseph Mkundi (Ukerewe) wote wa CCM, wataapishwa kwenye kikao cha Bunge kijacho.

Wabunge wote nane walijiuzulu nyadhifa zao kwenye chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kujiunga na CCM ambapo walipewa nafasi ya kutetea nafasi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles