24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Tishio kwa Trump, mtihani upinzani

NA SUBI SABATO, MAREKANI

KWA miaka miwili sasa, chama tawala Republicans kinachoongozwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kimekuwa na turufu ya kufanya maamuzi yote katika Bunge ambayo huhitaji kupitishwa tu kwa wingi wa kura za wabunge bila kujali wanatokea upande wa chama kimoja tu, na usiohitaji kuushirikisha upinzani, hivyo kuweza kuwaburuza chama cha Democratic katika kupitisha maazimio ya wabunge au matakwa ya rais.

Wakati Rais Trump anaingia madarakani, Republicans kilishachukua hatamu za uongozi wa chemba zote za baraza la Congress (Senate na House).

Hata hivyo hali imebadilika baada ya uchaguzi wa Novemba 6, mwaka huu ambapo sasa Democratic kimepata idadi kubwa ya wawakilishi katika House of Representatives ambao ni 227 (mpaka naandika makala haya) kati ya nafasi ya 435. Kimsingi chama kinatakiwa kuibuka na ushindi kwa kupata wawakilishi 218 tu, lakini Democratic wamevuka idadi hiyo hadi sasa.

Republicans wamebakia na ushindi kwenye Bunge la Seneti baada ya kupata wabunge 51 (katika wale 100 wanaotakiwa katika Bunge hili). Sheria inasema ili uibue mshindi kwenye Bunge la Seneti unatakiwa kupata wabunge 51.

Hali kadhalika, wananchi walichagua magavana katika baadhi ya maeneo ambako kipindi chao kiliangukia wakati huu na katika hao, 25 wamechaguliwa kutokana na chama cha Republican huku Democratic ikipata magavana 23 (kutoka 16 iliyokuwa navyo awali) baada ya kuwanyanganya Republicans viti 7.

Ingawaje Republicans wana idadi kubwa ya magavana ikilinganishwa na wapinzani wao (Democratic), lakini ni chama ambacho kinaonekana kupata faida kutokana na kumendea majimbo muhimu ambayo yalikuwa ngome muhimu za ushindi katika chaguzi zote zitakazofanyika ndani ya miaka 10 baada ya sensa ya mwaka 2020 na mgawanyo wa majimbo kwa mlingano wa uwiano wa watu mwaka 2021/2022.

Msimamizi mkuu wa zoezi hili ni Gavana wa jimbo akishirikiana na kamati au kamisheni iliyoundwa kwa mujibu wa sheria za jimbo husika.

Habari hii si nzuri sana kwa Republicans kwa sababu uwaiano wa watu uliofanywa kwa mara ya mwisho ulikuwa chini ya mikono yao na walifanya upendeleo kama walivyosema Wahenga kuwa, “kila mwamba ngoma, ngozi huvutia kwake”, kwa kukusanya taarifa ambazo huweza kuashiria kuwa watu wenye mwelekeo fulani watawapa kura zaidi wao na wapinzani watatawanywa kiasi kwamba kura zao zitagawanyika na kuwa pungufu.

Kwa kufanya hivi, walijiweka katika mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa kwa namna yoyote upigaji kura utakapofanyika watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kunyakua ushindi.

Suala hili limekuwa mwiba sana kiasi cha kusababisha baadhi ya majimbo kuburutana mahakamani au kuweka kipengele cha kupigiwa kura (ballot initiative) ili kubadilisha mfumo wa uchoraji mipaka hii ya kiuchaguzi.

Kutokana na ushindi wa Democratic, inatarajiwa kuwa ama watalipiza kisasi au watafanya suluhu kwa kurekebisha ramani hizo na kufanya upigaji kura na uwakilishi kuwa wa haki na wenye uwiano.

Tishio kwa Trump

Hakika, matokeo ya uchaguzi wa muhula huu yanauweka uongozi wa Rais Trump katika hali isiyo nzuri kutokana na mlolongo wa mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi bila kujali mrengo wa chama, wakilaumu ukiukwaji wa baadhi ya mambo kama vile ajira kwa ndugu, jambo ambalo japo kisheria halikatazwi lakini haikuwa hulka ya viongozi waliotangulia.

Vile vile kuna suala la kurudisha imani kwa wananchi kwa kukubali kuanika ripoti za ulipaji kodi kwa baadhi ya viongozi kama ishara ya uaminifu na kuwahimiza wananchi kufanya hiyo.

Hoja hiyo inashadidiwa hasa ikizingatiwa kuwa Rais Trump ni kiongozi mwenye utajiri mkubwa, hii imekuwa ni desturi ya marais wengi nchini Marekani kuanika ripoti za ulipaji kodi, lakini rais huyu amekuwa akijitetea kuwa hawezi kufanya hivyo kwa kuwa bado anakaguliwa kutokana na kuwa na biashara nyingi.

Utetezi wake unachukuliwa kama kisingizio tu kwa sababu hata Rais Richard Nixon aliwahi kuwa katika hali hiyo ya kukaguliwa lakini aliruhusu wananchi kuona mrejesho wake wa kodi.

Wananchi wanadhani Rais wa sasa hana nia ya dhati ya kufanya hivyo, wakihisi huenda anafanya makusudi kwa vile anatambua kuwa amekwepa kulipa kodi na hataki kuaibika.

Huu ni mtihani kwa democratic kwani baada ya kupata ushindi, wanaweza kutumia nguvu waliyonayo kutaka mamlaka ya kodi (IRS – Internal Revenue Authority) iwasilishe kwa mwenyekiti wa kamati mojawapo ya Bunge rekodi ya ulipaji kodi wa rais.

Ikiwa Democratic watafanikiwa, inawezekana kabisa taarifa hiyo ikadukuliwa au kiongozi mmojawapo kujitoa ufahamu na kuianika hadharani, hali akijua analofanya ni kosa la kisheria litakalosababisha aburuzwe mahakamani na kuishia jela. Tayari Rais Trump ameshaonya ya kuwa, endapo Democratic watamchunguza, naye atawachunguza, ingawaje hakufafanua ni katika maeneo gani atawachunguza.

Matokeo ya uchaguzi huu pia yanaashiria baadhi ya mambo yatakayofanyika ifikapo Januari mwakani, wakati shughuli za Bunge zitakapoanza rasmi.

Tayari baadhi ya viongozi wa Democratic wameshatamka nia yao ya kutaka kupitisha azimio la kutokuwa na imani na rais (impeachment) na inakisiwa kuwa tayari wanayo mashitaka kati ya 60 hadi 85 wanayodhani wanaweza kuyatumia moja baada ya jingine ili kumpata na hatia inayolazimisha ajiuzulu ama Katiba ifuate mkondo wake wa kumfukuza madarakani.

Jambo hilo limewahi kujaribiwa kwa marais watatu bila kufanikiwa, kwani mmoja alijiuzulu (Richard Nixon mwaka 1972) kabla hata ya ‘impeachment’ na wawili waliponea chupuchupu (Andrew Jackson mwaka 1868 na Bill Clinton mwaka 1998) baada ya hoja dhidi yao kukosa nguvu na mashiko ilipowasilishwa kwenye Seneti.

Wabunge wa Seneti hufanya kikao kama mahakama ili kujadili na kutoa hukumu mara baada ya hoja ya ‘impeachment’ kupitishwa kwenye House of Representatives.

Hadi sasa ni jambo la kinadharia tu na huenda watakwama kwa kuwa pia miongoni mwa wana-Democratic wapo wabunge wanaodhani si njia sahihi ya kufuata kwa wakati huu, isipokuwa tu litokee jambo la ugonjwa utakaomwondolea rais uwezo wa kutimiza majukumu yake ya kikazi au afanye kosa kubwa sana ambalo halitakuwa na tashwishi, kama vile kuhatarisha usalama wa nchi na raia, au kuporomoka kwa uchumi, hivyo kutokuwa na jinsi bali kumwondoa madarakani rais.

Vinginevyo hoja hii itakwama tena kwenye Seneti kwa kuwa bado inashikiliwa na Republicans ambao kwa wingi wao wa kura wanaweza kukubaliana kulinda masilahi yao na ya chama kwa kupiga kura ya za hapana wote 51 ili kuzishinda kura 49 za ‘ndiyo’ za Democratic.

Inatarajiwa kuwa Rais Trump anajipanga kukabiliana na upinzani katika kupitisha ajenda na kutimiza mipango na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni, ili kuwa katika wakati mzuri wa kuweza kuuambia umma mafanikio yake na kuutaka umpe kura zitakazoridhia kipindi cha pili cha uongozi.

Inatarajiwa pia kuwa Rais Trump atatumia njia za “my way or the highway” kwa majadiliano na Democratic kupatania baadhi ya mambo kutoka kila upande. Njia hii ikishindikana, Trump anaweza kupitisha ajenda zake kwa kutumia turufu yake ya urais ya kuandika oda maalumu ‘executive orders’, ambazo hazihitaji kuidhinishwa na kupitishwa na Bunge, ila zinaweza kufutwa na rais ajaye ikiwa ataona hazina tija.

Hata hivyo, endapo njia hizi zitashindikaka, Rais Trump anaweza kutumia mbinu ya kuwalaumu Democrats kuwa wapinga maendeleo na hivyo kuwashitakia kwa wananchi na kuwaomba wampe nafasi ya pili kisha wamchagulie wabunge wanaotokana na Republicans ili aweze kutimiza malengo yao.

Kwa upande wao Democratic, ni dhahiri kuwa watachukua uongozi wa kamati zote muhimu katika Bunge la Wawakilishi na hili ni muhimu kwao kwani ndiko zinakopitia hoja na masuala mengi muhimu yanayoihusu serikali na wananchi.

Inatarajiwa kuwa wataweza kuchunguza baadhi ya mambo ambayo yameshindikana kuchunguzwa na Republicans kutokana na kumlinda rais anayetokana na chama chao ili asipoteze imani kwa wananchi yeye pamoja na chama.

Mambo ambayo wanaweza kuchunguza ni pamoja na ajira zilizotolewa kwa ndugu na jamaa wa rais bila kujali ustaarabu wa kuepuka mwingiliano wa kimasilahi.

Vile vile Democratic watataka kufahamu ni kwa kiasi gani Rais Trump ameshiriki katika kuchangia pato la nchi kupitia ulipaji kodi kama raia wote wanavyopaswa kufanya, jambo ambalo si lazima kufanya ila imekuwa ni desturi ya marais wote kufanya hivi ikiwa kama mfano na kutokana na wananchi kutaka kufahamu.

Jambo jingine wanalotarajiwa kuchunguza ni matumizi ya fedha kama ilivyoidhinishwa na kupangwa na hasa kwenye suala muhimu la bima ya afya kwa wastaafu na watu wasio na bima kabisa kutokana na kutokuwa na ajira au kutokuipata kutoka kwa mwajiri.

Jambo la mwisho muhimu pengine ni suala la uhamiaji na uraia ambalo lilizungumziwa sana kipindi cha uchaguzi lakini halikuonekana kuwa na mashiko au umuhimu sana kwa wapiga kura. Hili nalo litaonyesha tafsiri ya mwelekeo wa urais wa Trump kuelekea mwaka 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles