27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAMA WEMA SEPETU AMLIZA STEVE NYERERE

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam

MSANII wa filamu, Steven Mengere, maarufu kama Steve Nyerere, jana alimwaga chozi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu rekodi mbili za sauti zinazosambaa zikihusisha mazungumzo yake na Miriam ambaye ni mama wa aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania 2006, Wema Sepetu.

Steve ambaye pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  na miongoni mwa wasanii waliopata kuunda kundi la Mama Ongea na Mwanao lililokuwa likizunguka kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea mwenza wa CCM ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, rekodi za mazungumzo yake na mama Wema zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii Alhamisi iliyopita.

Katika sauti hizo, mbali na mama Wema kumlalamikia Steve kwa kutokwenda kumuona Wema alipokuwa ameshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa siku saba kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya, lakini yeye mwenyewe anasikika akijitetea kwa kueleza jitihada alizofanya ikiwamo kuzungumza na baadhi ya mawaziri ambao aliwataja kwa majina ili kuhakikisha msanii  mwenzake huyo anaachiwa huru.

Katika sauti hizo, Steve alisikika akizungumza na mama Wema na kuwataja baadhi ya viongozi alioonana nao  ambao ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na kuwaelezea kusikitishwa kwao na kukamatwa kwa Wema na wote waliahidi kumsaidia.

Steve pia alimwambia mama Wema kuwa ameshagombana na Makonda na kwa kipindi kile walikuwa hawaongei kwa sababu ya Wema.

Akizungumza kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi, Steve alikiri kuwa sauti hiyo inayosambaa ni ya kwake, lakini alisisitiza kuwa yalikuwa ni mazungumzo binafsi baina yake na mama Wema.

Kwa sababu hiyo alisema kitendo cha kuzisambaza sauti hizo pasipo kushirikishwa ni hatari na ni wazi kuwa mama huyo alikuwa na nia ovu ya kumuharibia maisha kwa   kumgombanisha na viongozi wa CCM na Serikali.

“Sauti ile ni yangu na tuliongea mimi na mama Sepetu, yasipindishwe, nilifanya vile kwa kutumia sanaa yangu, niliongea kumridhisha mama Sepetu, lakini niliyoyaongea kwenye maongezi sikuyafanya, pale ilihitajika kutumia sanaa kwa sababu kwa hali aliyokuwa nayo ningemjibu hovyo huenda hata angeanguka.

“Maneno niliyoyasema katika simu na mama Wema na kutaja viongozi ni ya uongo, ilibidi nifanye hivyo maana sikuwa na jinsi, uwezo wa kuwaambia wabunge au kuwaelekeza cha kufanya sina, sina ujanja huo… namuomba radhi Spika Job Ndugai,” alisema Steve.

Alisema lengo la maongezi hayo ilikuwa ni kukitetea chama chake cha CCM kwa kutumia uwezo wa kuongea alionao kwakuwa tayari mama Wema alikuwa ameshakasirika na kuanza kumtupia lawama huku akigusia kukihama chama.

 “Namwomba radhi Rais wa Jamhuri, Dk. John Magufuli kwa kuhusisha viongozi wake, naomba radhi Chama cha CCM, wanisamehe na familia pia, niliteleza, natubu na kuomba radhi, wakati naongea na mama niliamini ni mama yangu mzazi, kumbe ni mtu mbaya na sikuwa na nia mbaya, mfano katika yale mazungumzo ningemtukana mtu si angekuwa ameshaniharibia maisha, sasa hivi unafikiri ningekuwa wapi,” alisema.

Alisema aliamini mama Wema alimpigia simu kwakuwa alikuwa anaweza kufanya jitihada za kumtoa polisi mtoto wake, kumbe alikuwa na malengo mengine.

“Simu tumeongea Februari 14, lakini imekuja kutoka baada ya siku tano mbele, hii inaonyesha kuwa watu hao walikuwa na malengo mabaya na mimi, nimejiuliza kwa nini nirekodiwe mimi, nina mambo gani mabaya hadi nirekodiwe, kwanini imesambazwa na baadaye watu wakahama chama, huu ni uuaji, walitaka kuniharibia maisha yangu,” alisema Steve.

Juzi mama Wema alipoulizwa kuhusu sauti hiyo, licha ya kusema hajaisikia zaidi ya kusikia maneno ya watu, lakini alisisitiza kuwa hawezi kuizungumzia.

“Steve ni mwanangu, mimi nasikia tu kuna sauti inasambaa, lakini sijaisikia, sijawasha simu siku nyingi na nikiwasha inakuwa mara moja tu naizima, hivi karibuni simu yangu iliharibika kabisa, hivyo siwezi kuongelea hayo mambo na kwa sasa sitaki kusikia chochote maana nilikuwa najiandaa kuhamia Chadema,” alisema mama Wema.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari jana, Steve alipoulizwa iwapo anachokizungumza katika mkutano huo ni cha kweli na anathibitisha vipi hafanyi maigizo kama aliyomfanyia mama Wema, alisema ameamua kutoa ufafanuzi huo kwa sababu ya maneno yanayosambaa.

“Nanyooshewa vidole sana, watu wananiongelea kila mahali, nimeamua kufanya hivi kwa utashi wangu, sijatishwa na mtu na wala siongei maigizo,” alisema Steve.

Pia alisisitiza hana ugomvi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama ilivyosikika katika sauti hiyo.

Kuhusu kushikiliwa na polisi, Steve alihoji akisema bila kufafanua: “Ningekuwa nimekamatwa ningekuwepo hapa?”

Msanii huyo aliongeza kuwa mama Wema hakuwa na sababu ya kuiingiza CCM katika matatizo ya mtoto wake kwakuwa waliposaini mkataba wa kufanya kampeni hakukuwa na kipengele cha msanii kusaidiwa atakapopata matatizo.

“Katika kundi la Mama Ongea na Mwanao na wasanii wote tulioshiriki kampeni tulisaini mkataba, na hakuna sehemu ambayo inaonyesha mtu akikamatwa au akipata shida chama kitamsaidia, halafu si ajabu kuwa mwanachama usisaidiwe wapo watu ndugu zao wanaumwa wa tumbo moja na hawahudumiwi, hiyo ni hali tu ya kawaida,” alisema Steve.

Akielezea kuhusu madeni ya wasanii ambayo Wema juzi alisema wanadai CCM pamoja na wasanii wenzake walioshiriki kampeni, Steve alikanusha.

 “Mimi ndiye nilikuwa mwenyekiti wa kundi la Mama Ongea na Mwanao, Wema alikuwa makamu mwenyekiti katika kundi lile, wote tulilipwa na kama kuna msanii anasema hajalipwa ajitokeze nimuone, kama hawajalipwa labda wengine, lakini sio kundi letu na kati ya watu waliolipwa fedha nyingi ni dada yangu Wema Sepetu, yeye hadai hata senti tano,” alisema Steve.

Alisema hata kama Wema amehama CCM aache kuongea uongo kwakuwa chama hicho hakikumfanyia mambo mabaya pekee, yapo na mazuri.

Juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari, Wema alisema tangu kumalizika kwa kampeni hawajalipwa madeni yao na kila wakidai wanaambiwa waende kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles