29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mama, watoto wachinjwa kinyama

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

Na Mwandishi Wetu, Nzega

WIMBI la mauaji ya kutisha limeendelea kutikisa nchini, baada ya watu wasiojulikana kuwaua mama na watoto wake wawili kwa kuwakatakata kwa mapanga usiku wa kuamkia juzi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika Kijiji cha Nata wilayani Nzega mkoani Tabora.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, aliwataja waliouawa kuwa ni mama Leticia Thomas, Marietha Nicolaus ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mwanaruru na Magreth Nicholas ambaye umri wake haukutambulika.

“Mama wa watoto hao aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga sehemu za kichwani na bega la kushoto, hali iliyosababisha apoteze maisha hapo hapo kutokana na majeraha mengi.

“Lakini pia watoto Marietha na Magreth nao walikatwakatwa hivyo hivyo… mauaji haya ni mabaya, tunaendelea na msako mkali wa kuhakikisha wahusika wanatiwa nguvuni,” alisema Kamanda Kaganda.

Alisema mpaka sasa chanzo cha mauaji hayo ya kinyama hakijajulikana, ingawa kuna taarifa kuwa inawezekana yamesababishwa na masuala ya mapenzi.

“Polisi tunaendelea na uchunguzi wetu wa kina, hatujapata chanzo cha mauaji haya, tunaomba mtupatie muda wakati huu ambao askari wangu wanaendelea na kazi,” alisema Kamanda Kaganda.

Alisema mpaka jana hakuna mtu hata mmoja aliyetiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.

“Kwa vile polisi tunafanya kazi zetu kisayansi, naamini tutafanikiwa ingawa mpaka sasa hakuna mtu aliyetiwa mbaroni,” alisema Kamanda.

Alisema taarifa za kugundulika kwa miili hiyo zilitolewa na majirani ambao walilazimika kwenda kumwangalia mama Magreth baada ya kuona amechelewa kuamka.

“Inaonekana baada ya tukio lile kulipopambazuka asubuhi, mama Magreth alikuwa hajafungua mlango majirani wakaamua kwenda kugonga mlango walipoona kimya wakaamua kuvunja mlango na kukuta familia yote imeuawa,” alisema Kamanda.

Matukio ya watu kuchinjwa yamekuwa yakitokea kila mara ambapo Septemba 16 mwaka huu, mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Melasi Ndabi aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa kufika nyumbani kwake katika Kijiji cha Lisu wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles