ALHAMISI ya wiki iliyopita alizaliwa mtoto wa ajabu katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino, mkoani Dodoma katika Zahanati ya Manchali.
Mtoto huyo alikuwa hana sehemu kubwa ya kichwa na utosi ukiwa nje.
Mara baada ya kuzaliwa kwa mtoto huyo, wakazi wa eneo hilo wanasema si mara ya kwanza kuzaliwa mtoto wa ajabu na kwamba hiyo ni mara ya tatu.
Diwani wa kata hiyo, Merry Matonya, anasema si mara ya kwanza kuzaliwa kwa watoto waina hiyo.
Anasema Januari mwaka huu alizaliwa mtoto akiwa na kichwa kikubwa huku akiwa hana jinsi ya aina yoyote ambaye muda mfupi baada ya kuzaliwa alifariki.
Anasema Februari mwaka huu alizaliwa tena mtoto akiwa hana mikono wala kichwa huku akiwa tayari ameishafariki.
“Kama nilivyokwambia, huyu anakuwa mtoto wa tatu kuzaliwa katika kata hii ya Manchali,” anasema.
ALIYEJIFUNGUA ASIMULIA
Joyce Eliasi (22) ndiye aliyejifungua mtoto huyo wa ajabu, anasema alianza kujisikia vibaya siku mbili kabla ya kujifungua hivyo akamwomba mama mkwe wake Failet Mlaba, amsindikize katika Kituo cha Afya cha Manchali.
Anasema alipofika huko alipokelewa vizuri na wauguzi kisha wakampigia simu daktari ili aje amwangalie.
Anasema daktari alipofika alimchunguza na kusema kesho yake Alhamisi anatakiwa apelekwe katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kutokana na kuwa na mimba ya mapacha.
“Kumbuka hiyo ilikuwa ni jioni hivyo usiku kucha niliendelea kusikia maumivu ya uchungu, ilipofika majira ya saa moja asubuhi uchungu ulizidi hivyo nikamwita nesi ili anisaidie.
‘’Nesi alifika akawa karibu na mimi uchungu ulizidi ilipifika saa tatu, daktari akaja kuniambia nijitayarishe ili niende Dodoma kwani Ambulance ipo njiani inakuja.
“Kila mara walikuwa wanaenda pembeni na kuanza kunong’ona maneno niliyokuwa nikisikia twendeni tukajaribu lakini kichwa hatukioni, nilikata tamaa ya kuishi nilijua nakufa,” anasimulia.
Anasema mara baada ya kuanza kujifungua alishangaa nesi akitaka kukimbia na alipojifungua mtoto alishangaa zaidi wote waliokuwa chumbani walikuwa kama wanauoga.
“Ndugu zangu walipofika pamoja na majirani walipomwangalia mwanangu nikaona wanakimbia nikawa nashangaa kuna nini mpaka wanakimbia nilishikwa na hamu na mimi niangalie lakini nilikuwa siwezi kutokana na maumivu niliyokuwa nayo na nguvu kuniishia.
“Mama akanifuata kuniambia kwamba nimezaa mtoto wa ajabu macho yapo juu, utosi upo nje ila ni mzima jitahidi ukamwangalie,”anasema.
Anasema alijikaza na kwenda kumwona mwanae lakini alishangaa kwa jinsi alivyokuwa sehemu za nyuma ya kichwa.
Anaendelea kusimulia: “Jamani mwanangu (huku akilia)alikuwa ni mzuri sana tena wa kiume alifanana na mimi pamoja na baba yake lakini nilishindwa nifanyaje zaidi ya kulia tu.
Anasema huo ni uzao wake wa pili ambapo mwanawe wa kwanza anayeitwa God ana umri wa miaka mtatu na miezi nane.
Anasema mwanawe wa kwanza alijifungulia katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na hakuwa na tatizo.
ALIVYOLEA UJAUZITO
Joyce anasema wakati wa ujauzito sehemu za siri zilikuwa zikimuuma hivyo akaamua kwenda Zahanati ya Chilonwa ili kuangalia kama alikuwa na tatizo.
Anasema katika kipindi chote cha mimba yake alihudhuria kliniki mara tatu tu.
“Nilienda mara ya kwanza mikiwa na mimba ya miezi minne na baadaye miezi sita baada ya kuona sehemu za siri zinauma. Nikiwa na miezi nane nilikwenda tena na baadaye kujifungua.
Anasema alipoenda katika Zahanati ya Chilonwa, daktari alimwambia ana uchafu katika sehemu za siri hivyo akampa dawa za kutumia.
Baada ya hapo hakurudi tena bali alitumia dawa lakini aliendelea kupata maumivu.
Anasema japo mwanae alifariki lakini ataendelea kumkumbuka kutokana na kuzaliwa akiwa na sura ya kuvutia.
Joyce anaiomba Serikali kuweka vifaa pamoja na dawa katika zahanati zilizopo kijijini ili kubaini kama watu wana matatizo na kuchukua hatua kabla ya kujifungua.
MAMA MZAZI WA JOYCE
Juliana Sango ambaye ni mama mzazi wa Joyce, anasema yeye ndiye aliyemsindikiza mwanae hospitalini kujifungua.
Anasema wakati akijifungua alishangaa kuwaona manesi wakikimbia jambo ambalo lilimshangaza.
“Ilibidi nimfuate nesi mmoja nikamuuliza mbona unakimbia akaniambia Joyce kajifungua kitu cha ajabu.
“Nilipoenda kwa daktari akaniambia wanajaribu kutafuta kichwa lakini hawakioni, nikataharuki nikijua hili litakuwa tatizo.
“Baadaye kidogo daktari akaniambia kajifungua salama nikamwone ila kama haelewi, ikabidi niende nikamwangalie, nilichokiona sikuamini mjukuu wangu alikuwa hana utosi huku sehemu za nyuma zote zikiwa wazi,” anasimulia.
Katika familia yake hakuna aliyewahi kuzaa mtoto wa aina hiyo, hivyo alikuwa akishangaa tu.
MAJIRANI WANENA
Agness Daniel, anasema alienda hospitali kwa nia ya kumsindikiza jirani yake lakini kile kilichozaliwa hadi leo haamini.
“Tunaamini ni mipango ya Mungu ila jamani inatisha na mimi ndio nilikimbia niliona maajabu mtoto haeleweki. Nimepata somo tunatakiwa kuwahi kliniki pindi tunapopata ujauzito ili kubaini tatizo mapema,” anasema Agness.
MZEE WA KIMILA AZUNGUMZA
Naye Stanley Mlewa ambaye ni mzee wa kimila katika eneo hilo anasema tatizo kama hilo liliwahi kutokea pia mwaka 1956 ambapo mara baada ya kuzaliwa mtoto wa aina hiyo wakazi wa eneo hilo walivuna sana.
“Labda na mwaka huu tutavuna sana lakini siku hizi tunaamini Kristo tofauti na miaka ya nyuma ila pia kwenda hospitali mapema ni jambo la muhimu,”anasema.
MUME
Kwa upande wake baba wa mtoto huyo, Athanasio Korongoo, anasema alimpa huduma zote anazotakiwa kupewa mke wake.
“Hata aliposema sehemu za siri zinamuuma mimi ndio nilimshauri aende Chilonwa, akaenda na kupewa dawa.
“Ila tunatakiwa tukubali kwa kuwa ndio mipango ya Mungu ila inauma na kusikitisha, angekuwa mtoto wangu wa pili tena wa kiume,” anasema.
DIWANI
Diwani wa kata hiyo, Marry Mazengo, anasema tatizo kubwa la wakazi wa eneo hilo ni kukataa kujifungulia hospitali huku wengi wakitaka kujifungulia nyumbani.
“Matatizo haya yanasababishwa na watu kupenda kujifungulia nyumbani, hapa hawataki kabisa kujifungulia hospitali au katika kituo cha afya,” anasema.
Anasema kutokana na hilo alianzisha kampeni ya mama ambaye atajifungulia nyumbani atatozwa faini ya Sh 50,000 ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kina mama kwenda katika vituo vya afya.
Anataja changamoto nyingine inayowakabili wakazi wa eneo hilo kuwa ni kuogopa kwenda kujifungulia katika vituo vya afya kutokana na ukali wa manesi.
“Mbali na kuwaogopa manesi wengi wamekuwa hawaogi hata kwa siku sita na zaidi hivyo wanaogopa wakienda kwa manesi watawatukana kutokana na uchafu hivyo kuamua kujifungulia nyumbani,” anasema.
Diwani huyo anaiomba Serikali kupeleka wataalamu wa afya ili kuweza kugundua ni tatizo gani limekuwa likiwakumba wakazi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake Mganga wa Zahanati ya kijiji hicho, Gaudensia Mpokwa, anasema tukio hili ni la tatu ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
“Nahisi pia katika vyakula wanavyokula wanakuwa wanakosa baadhi ya vitamin ndio maana haya yanatokea,” anasema.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Mzee Nassoro, anasema hizo ni dalili za kukosekana kwa baadhi ya vitamini.
“Hili ni tatizo la ukosefu wa baadhi ya vitamini ndio maana wanazaliwa hawa watoto tutapeleka wataalamu ili waliangalie kwa umakini suala hilo,” anasema.