27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mikakati Kamati ya Ukimwi kumlinda Mkemia Mkuu  

Wabunge walio katika Kamati ya Ukimwi wakiwa katika ziara yao ya kutembelea Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.KAMATI za Bunge zinakutana kwa takribani wiki ya tatu sasa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.

Kamati hizi zinakutana kabla kuanza kwa Bunge la Bajeti Aprili 19 mwaka huu zikifanya shuguli mbali ikiwamo kusikiliza taarifa za utendaji wa wizara na tassisi mbalimbali za Serikali pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo.

Mojawapo ya kamati hizi ni Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi ambayo mbali na kujadili masuala mbalimbali mtambuka kuhusia na maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi na tatizo la dawa la za kulevya nchini pia ilipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali.

Mojawapo ya sehemu ambayo kamati hiyo ilitembelea ni pamoja Ofsi ya Mkemia Mkuu iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na ofisi hiyo.

Lengo hasa la kamati katika ofisi hiyo lilikuwa ni kujielimisha kazi na wajibu wa Mkemia Mkuu wa Serikali hasa katika suala la dawa.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Masuala ya Ukimwi ilisema kwamba iko tayari kuiunga mkono Serikali iwapo itawasilisha Muswada wa Sheria ya Kuilinda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Ahadi hiyo ilitokana na taarifa ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Khamis Kigwangala ambapo iliieleza kamati hiyo kwamba ipo haja ya kuleta muswada huo ambao utaipa mamlaka kamili Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Mwilima, anasema kamati yake inafahamu majukumu nyeti ya maabara hiyo na kwamba itaunga mkono muswada huo wakati utakapowasilishwa.

“Kamati iko tayari kuunga mkono muswada huo utakapokuwa tayari ili ofisi hii isiporwe mamlaka yake na taasisi nyingine,” anasema.

Anasema ofisi hiyo ni muhimu kwa kuwa imekuwa ikishughulika na masuala mbalimbali  ya uchunguzi wa kimaabara kama vile upimaji wa vinasaba (DNA), uchunguzi wa maiti kwa vifo vyenye utata na upimaji wa dawa za kulevya na vileo vya aina mbalimbali.

“Kwa hali iliyopo sasa inatishia uhai wa ofisi ya Mkemia Mkuu kwa kutokuwa na mipaka ya kimajukumu kati ya mashirika mengine ya viwango na ofisi hiyo,” anasema.
Aidha, mwenyekiti huyo ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuitengea ofisi hiyo bajeti ya Sh bilioni mbili kwa ajili ya kununua mashine za kisasa na kukarabati zilizopo.

Kwa upande wake Dk. Kigwangala anasema kutokana na ofisi hiyo kutokuwa na ulinzi wa kisheria inakosa mapato na pia inabaki kama yatima.

“Hali hii inasabaisha baadhi ya zilizokuwa idara hapa kujitenga na kuwa wakala unaojitegemea kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango nchini (TBS),” anasema.

Anasema umefika wakati ambapo Polisi na wao wanataka kufungua maabara yao kwa ajili ya uchunguzi hali itakayoondoa jicho la tatu katika utoaji wa haki kwa kuwa watakuwa wanafanya kila kitu wao.

“Polisi wakifungua maabara yao, kwa mfano kwa kesi kama ya dawa za kulevya, watakuwa wanakamata wao, wanachunguza wao, wanapima wao dawa zilizokamatwa kwenye maabara zao, pia wanapeleka wao mahakamani hali itakayoondoa utoaji haki katika jicho la tatu na kudhoofisha Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali,” anasema.

Anasema hali hiyo pia inaikosesha mapato ofisi hiyo ya Mkemia Mkuu ambayo kwa asilimia kubwa inajiendesha yenyewe.

“Hali hii inasababisha idara nyingine zichepuke na kwenda kujitengenezea mamlaka zenye nguvu na kujikusanyia mapato ingawa zinafanya kazi ambazo kimsingi zilitakiwa kufanywa na Mkemia Mkuu,” anasema.

Anasema njia pekee ya kuimarisha ofisi hiyo ni kuiwekea ulinzi wa kisheria na kwamba muswada ulishaandaliwa na unatarajiwa kuwasilishwa bungeni  wakati wowote nafasi itakapopatikana.

Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ofisi hiyo, Profesa Samwel Manyele, anaelezea changamoto ambazo ofisi yake inakabiliana nazo ikiwamo kutokarabatiwa kwa baadhi ya majengo na baadhi ya mashine.

“Hata hivyo jukumu la kuendesha taasisi hii ni letu isipokuwa kwa mishahara ya wafanyakazi peke yake,” anasema.

Anasema ofisi yake ina majukumu mbalimbali ikiwamo kufanya uchunguzi kwa miili ya marehemu waliokufa vifo vyenye utata, kupima dawa za kulevya na vileo, kupima dawa mbalimbali za mifugo na kemikali zilizopo kwenye vyakula na kupima vinasaba.

Akizungumzia tatizo la dawa za kulevya ambapo ofisi yake ndiyo inahusika katika kupima sampuli mbalimbali za aina za dawa hizo, anasema tatizo hilo bado ni kubwa na kwamba Tanzania kwa kawaida hutumika kama njia za kupitishia dawa hizo.

Anasema kwa sasa taasisi yake inajipanga kuanza kutekeleza agizo la Waziri wa Afya la kuwapima madereva, wanafunzi na waajiriwa wapya kama wanatumia dawa za kulevya.

“Tunataka tuanze mpango wa kuwapima vijana waliopo shuleni kuona kama wanatumia dawa za kulevya kwa lengo la kujua mapema athari walizopata na jinsi ya kuweza kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizo,” anasema.

Kuhusu vipimo vya vinasaba (DNA), anasema asilimia 49 hadi 51 ya watoto waliokwenda kupima kipimo hicho waligundulika kwamba baba zao hawakuwa hao.

“Idadi hiyo si kwa Watanzania wote bali kwa wale tu walioenda kupima, kipimo hiki kinaeleza ukweli kwa asilimia 99.99,” anasema.

Anasema gharama halisi za kupima kipimo hicho ni Sh 800,000 lakini ofisi hiyo inapima kwa Sh 100,000 na kwamba gharama nyingine zinachangiwa na ofisi hiyo.

“Sheria inakataza mtu kwenda kupima kipimo cha DNA nje ya nchi, Ofisi ya Mkemia Mkuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuchukua sampuli  na kuipeleka nje ya nchi kwa ajili ya vipimo na si vingenevyo,” anasema.

Kamati hiyo hadi sasa imeshatembelea maeneo mbalimbali ikiwamo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na vituo vya kutolea huduma ya methodine kwa waathirika wa Dawa za Kulevya vya Mwananyamala na Muhimbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles