26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

‘Dunia inanenepa’, hakuna hatua zinazochukuliwa kuizuia

MikeJOSEPH HIZA

MAJESHI ya uchumi hayalali ili kuongeza utajiri na hivyo moja kwa moja kusababisha ongezeko kubwa la watu wenye uzito wa kupindukia duniani.

Mwelekeo huo unatufanya sasa tuishi katika dunia yenye watu wengi wenye uzito wa kupindukia zaidi ya wale wenye uzito wa chini.

Kwa ongezeko la kipato, mataifa yanaongeza kiwango cha matumizi ya milo yenye kalori nyingi, watu wanahamia mijini kutoka vijijini kufuata kile wanachokiona fursa nono zilizopo huko.

Wakiwa mijini watu wanakutana na vyakula vya holela (junk food) pamoja na vinavyotokana na usindikaji viwandani kwa gharama nafuu, ambavyo bila kujiuliza mara mbili mbili wanavitia tumboni siku hadi siku.

Mashine, hasa roboti sasa zinafanya kazi nyingi, ambazo awali zilikuwa zikifanywa na binadamu na hivyo kupunguza kiwango cha nishati inayojishughulisha mwilini.

Hilo moja kwa moja linatengeneza kundi la watu wasiojishughulisha, ambao unaweza kusema wanaishi kivivu.

Kwa sasa kuna mataifa 114 duniani, ambayo zaidi ya nusu ya watu wake wazima wanahesabika kuwa wanene kupindukia ikiwamo sehemu kubwa za Amerika, Ulaya na Mashariki ya Kati kwa mujibu ya takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika mataifa madogo ya visiwa vya Pasifiki na mataifa ya Ghuba ya Uajemi, zaidi ya theluthi mbili ya watu wake wanahesabika kuwa wenye uzito wa kupita kiasi au wanene.

Katika takwimu  hizo, China na Marekani, ambazo ndizo zinazoongoza duniani kwa ukubwa wa uchumi wao, pia zinaongoza kwa wingi wa watu wenye uzito wa kupindukia.

Wakati ikiwa hivyo, Uingereza inaongoza mataifa ya Ulaya kwa uzito mkubwa miongoni mwa watu wake huku Japan likiwa taifa tajiri lililo na watu wachache wenye uzito mkubwa.

Ikimaanisha kuwa Wajapan ni watu wenye kudhibiti ulaji wao pamoja na kuwa na mazoea ya kujishughulisha licha ya utajiri na wingi wa roboti zilizopora kazi za shuruba za binadamu.

Kwa mujibu wa utafiti mpya, zaidi ya watu milioni 640 wameongeza unene uliopindukia mwilini, kiwango kikubwa kuliko cha wale wenye uzito mdogo wa kupindukia.

Utafiti huo umeonesha kuwa mmoja kati ya wanaume 10 ana unene wa kupita kiasi huku mmoja kati ya wanawake saba akiwa katika hali hiyo pia.

Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, idadi ya watu wanene wenye uzito wa kupindukia imeongezeka mno.

Watu walio na viwango vya vipimo 30 na zaidi vya kisayansi vinavyolinganisha urefu na uzito wa binadamu yaani kwa Body Mass Index (BMI), wameongezeka kutoka watu milioni 105 mwaka 1975 hadi watu milioni 641 mwaka 2014.

Uzito ulio sawa hubainishwa kisayansi kwa kupima uzito wa mtu kwa kilo kisha kuugawa na urefu wake kwanzia mguu hadi kichwani.

Uzito huo wa BMI unaozidi 25 huwa umepita kiwango na zaidi ya 30 ni wa kupindukia, huku unapofika 40 na zaidi huitwa uzito wa ugonjwa kwa kimombo ‘morbidly obese’.

Walioko katika hali hii hupata taabu kupumua na kutembea na hukumba asilimia moja ya wanaume na asilimia mbili ya wanawake.

Utafiti huo uliofanywa na watafiti 700 na kulijumuisha WHO, ulihusisha watu wazima milioni 20 kutoka mataifa 186.

Hata hivyo, kama ambavyo tumeona awali hapo juu, wengi ya wanaokumbwa na hali hii hutoka mataifa yaliyo tajiri na kwa maana hiyo wengi ya wanaotoka mataifa masikini wana uzito wa chini.

Ripoti ya utafiti huo imeongeza kuwa moja ya tano ya watu wazima watakuwa na uzito kupindukia ifikapo mwaka 2025.

Profesa Majid Ezzati kutoka Chuo cha Afya ya Umma mjini London, Uingereza anasema uzito kupindukia unaokumba idadi kubwa ya watu ulimwenguni kote hivi sasa ni tishio kwa afya zao.

Ameongeza kuwa suala hilo haliwezi kusuluhishwa tu kimatibabu, au kupunguza bei za dawa za kudhibiti uzito kupindukia wala kuongeza barabara za matembezi na watu kuendesha baiskeli ili kupunguza uzito,.

Bali anaseme, sharti kuwe na mikakati kabambe duniani ikiwemo kupunguza bei za vyakula vinavyokuza lishe bora na kuongeza bei za vyakula vinavyozidisha uzito mwilini mfano sukari na vyakula vinavyotengenezwa viwandani.

Hata hivyo, uzito uliopungua pia umetajwa kuwa changamoto katika baadhi ya mataifa, mfano robo ya watu katika bara Asia wamepungukiwa uzito.

Katika Afrika ya Kati na Mashariki asilimia 12 ya wanawake na 15 ya wanaume wanao uzito uliopungua viwango vinavyohitajika.

Awali ukiwa umehesabiwa kama tatizo la nchi za kipato cha juu tu, unene kwa sasa unapaa pia katika nchi za kipato cha chini na hasa cha kati hasa katika maeneo ya mijini.

Katika mataifa yanayoendelea hasa yanayokuja juu kiuchumi ambayo yaliwekwa na Benki ya Dunia kama mataifa ya kipato cha chini na kati, viwango vya ongezeko la watoto wenye uzito kupindukia na unene umeongezeka zaidi ya asilimia 30 ya nchi zilizoendelea.

Uzito wa kupindukia na unene unahusishwa na vifo zaidi duniani kuliko uzito mdogo wa kupindukia.

Kwa maneno mengine wengi wa watu duniani wanaishi katika nchi ambazo uzito wa kupindukia na unene unaua watu zaidi kuliko zenye uzito mdogo kupindukia.

Nini kinasababisha unene na uzito kupindukia?

Kimsingi sababu ya unene na uzito kupita kiasi ni kutokuwepo uwiano baina ya kalori zinazoingia na kutoka mwilini.

Duniani kwa sasa imeshuhudia; ongezeko la vyakula vyenye wanga ambavyo vina mafuta kwa wingi; na ongezeko la watu wasiojishughulisha kimazoezi kutokana na ongezeko la wingi wa kazi, kubadili mifumo ya usafiri na ukuaji wa miji.

Mabadiliko ya mlo na kukosekana ujishughulishaji kimazoezi mara nyingi hutokana na mabadiliko ya kimazingira na kijamii yanayotokana na kupigwa hatua za maendeleo na ukosefu wa sera zinazounga mkono sekta kama vile afya, kilimo, uchukuzi, mipango mijini, mazingira, usindikaji vyakula, usambazaji, masoko na elimu.

Nini kifanyike?

Ongezeko la upatikanaji wa chakula na ukuaji wa utajiri na miji kunatarajia kuendelea, hali ambayo itaendelea kuongeza watu wanene kupindukia.

Kwa sababu hiyo, kuna umuhimu wa uzingatiaji wa masuala ya afya, mipango miji, kilimo, usindikaji vyakula, mazingira, masoko na elimu na hasa wakati wa utengenezaji wa sera zinazolenga kukuza utajiri yaani za kiuchumi na kibiashara.

Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha unafuu wa bei za vyakula bora na kuongeza kodi kwa vile vya kusindika viwandani na vyenye kalori nyingi.

Bila kuchukua hatua kama hizo, dunia itazidi kunenepa na kufikia kiwango ambacho tutashtuka tumechelewa kuchukua hatua.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles