27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Makundi ya urais yaibukia ALAT

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

MAKUNDI yanayosaka urais mwakani, yameibukia katika Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), ambako mmoja wa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo anadaiwa kumwaga fedha ili afanyiwe kampeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa ALAT, Habraham Shamumoyo, alisema taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa fedha kwa jumuiya hiyo ili iweze kumfanyia kampeni ya urais.

Shamumoyo alisema kuwa lengo la taarifa hiyo ni kuchafua sifa ya jumuiya hiyo iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Pinda.

Alisema kuwa Septemba 17, mwaka huu katika mtandao wa Jamii Forum ilisambazwa taarifa kwamba Pinda ametoa rushwa kwa dola za Kimarekani kwa ALAT chini ya kiongozi wake Didas Masaburi ili kuratibu zoezi la kumpigia kampeni.

“ALAT haijawahi kupokea fedha za Kitanzania wala dola za Kimarekani kutoka kwa Pinda kwa ajili ya kampeni zozote au kwa kugawa kwa ajili ya mtu yeyote. Jumuiya inaendeshwa kwa michango halali ya wanachama wake na misaada ya wabia katika maendeleo.

“Jumuiya hii ina mfumo wake wa kisiasa na kiutendaji na inaendeshwa kwa kufuata taratibu za fedha ambapo kila mwaka mahesabu ya fedha hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) ,” alisema Shamumoyo.

Alisema kuwa taarifa hiyo ilisema fedha hizo zilisambazwa na Masaburi ilihali kiongozi huyo yupo Ujerumani kwa ziara rasmi ya kikazi.

“Mwenyekiti yupo Ujerumani kikazi, sasa nashangaa hizo fedha amezigawa kwa utaratibu gani na kwa njia gani,” alisema.

Aidha alisema endapo aliyeandika habari hizo ana ushahidi, auwasilishe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili hatua zaidi zichukuliwe.

“Kwa kushirikiana na mwanasheria wetu, tunatafuta namna ya kufanya ili tuweze kuwabaini waweka  taarifa hizo kwenye mtandao na baadaye tutawachukulia hatua za kisheria,” alisema Shamumoyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles