22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya AG Z’bar kujiuzulu Bunge la Katiba yabainika

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman

NA WAANDISHI WETU, DAR NA DODOMA

SIRI ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, imebainika.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo, kililiambia MTANZANIA kuwa wakati vikao vya kamati hiyo vikiendelea, Othman alipendekeza mambo 17 yenye maslahi kwa Zanzibar yaingizwe ndani ya Katiba inayopendekezwa na Bunge, lakini yakakatiliwa.

Kujiuzulu kwa kigogo huyo wa SMZ kulizua taharuki ya ndani ya Bunge la Katiba na hata baadhi ya wajumbe kutaka kujua sababu ya kufikia hatua hiyo.

Kikiendelea kufafanua suala hilo, chanzo hicho kilisema baada ya kukataliwa kwa maswala hayo, Othman aliamua kumwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, na kumweleza uamuzi wake wa kujiuzulu.

Kutokana na sintofahamu hiyo, iliwalazimu viongozi wa juu wa CCM kukutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa mwanasheria huyo kwa kile walichodai amekisaliti chama.

Chanzo hicho kilisema baada ya Othman kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na Ikulu ya Zanzibar na kuomba nafasi ya kukutana na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Baada ya kukutana na Dk. Shein, Othman alieleza namna Kamati ya Uandishi ilivyopinga kuingizwa kwa mambo 17 ambayo yana maslahi kwa Zanzibar. Kutokana na uzito wa hoja hizo, kiliitishwa kikao cha Baraza la Mapinduzi.

“Kikao hicho kiliwashirikisha mawaziri wote wa SMZ wakiongozwa na Mwenyekiti Dk. Shein, walipewa taarifa hiyo na kuijadili kwa kina na kisha kukubaliana na hoja za Mwanasheria Mkuu juu ya masuala hayo 17.

“Kikao kile chini ya Dk. Shein kiliazimia hoja hizo 17 ziwasilishwe kwenye Baraza la Mawaziri la Muungano,” kilisema chanzo chetu.

Hatua hiyo ya Baraza la Mapinduzi kuungana na Othman, ilifanya juzi Baraza la Mawaziri la Muungano chini ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukaa, na pamoja na mambo mengine lilijadili hoja 17 za SMZ na kukataa baadhi yake.

Taarifa zilizopatikana mjini Dodoma tangu kujiuzulu kwa mwanasheria huyo, zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wamekuwa na vikao vya siri lengo likiwa ni kushinikiza mambo hayo 17 kuingizwa kwenye Katiba mpya.

Katiba hiyo inayopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa leo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kabla ya kujiuzulu, Othman mara kadhaa alinukuliwa na vyombo vya habari akitetea muundo wa Muungano wa Serikali tatu.

KAULI YA IKULU Z’BAR

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Hassan Hassan, alikana kuwapo kwa taarifa hizo huku akitaka atafutwe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

“Hakuna kikao chochote kilichoketi na kujadili suala la Mwanasheria Mkuu ila ninachoweza kusema mtafute Makamu wa Pili yeye ndio msemaji wa Serikali,” alisema Hassan.

MNYIKA, SAKAYA WAPINGA MAREKEBISHO YA KANUNI

Kwa upande wao Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika na Magdalena Sakaya wa CUF Bara, wamepinga Bunge Maalumu la Katiba kufanya marekebisho ya kanuni zinazoruhusu wajumbe wa Bunge hilo kupiga kura ya kupitisha Katiba hata wakiwa nje ya nchi.

Mnyika alisema hatua hiyo ni kulazimisha kutafuta kura za kifisadi zitakazowezesha kupatikana kwa akidi ya theluthi mbili.

“Kama Bunge hilo linavunja sheria kwa kitendo chake cha kukusanya maoni kwa wajumbe walioko nje ya Bunge, kwani wakati wa utengenezaji wa kanuni nilipeleka pendekezo la kupiga kura kwa wajumbe toka nje, jambo hilo lilikataliwa na kuelezwa kuwa ni kinyume na sheria,” alihoji Mnyika.

Naye Sakaya alisema hatua ya Sitta kulazimisha kubadili kanuni kumeshusha heshima yake na katu mwanasiasa huyo hafai kuongoza hata Serikali ya Mtaa.

“Sitta amevunja heshima yake, kwa hili hafai hata kuongoza Serikali za Mitaa,” alisema Sakaya.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. Nilimheshimu sana mh sitta hapo kabla.ila mara baada ya kuukwa uenyekiti wa bunge maalum ndo undumilakuwili wake ameuanika hadharani. Kwa sasa angekuwa kijijin kwetu hata ubalozi wa nyumba kumi tusingempa!!.

  2. jamani hata kama watanzania tunaburuzwa, kwa mambo mengine ninyi viongozi jaribuni kuwa na aibu! ivi mtu atapigiaje rasimu kula wakati hajui hata kilichozungumziwa? Eti apige hata akiwa nyumbani kwake! jamani acheni muzaha na uhai wa inchi!

  3. Serikali ya CCM kwa kuendelea kuwa na moyo mgumu katika kuukataa ukweli ni jambo lililo dhahiri kuwa inajihakikishia anguko lisilo dhuhurika hata kama upinzani utakuwa dhaifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles