Na Sheila Katikula, Mwanza
WANANCHI walio na magonjwa ya kudumu, magonjwa ya muda mrefu na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na makundi maalumu ya wazee, watumishi wa afya, waandishi wa habari mkoani Mwanza wameombwa kujitokeza kwa wingi agosti 4 mwaka huu kwenye vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kutoa chanjo ya UVIKO 19.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa elimu ya Afya wa Magonjwa ya mlipuko kutoka Wizara ya Afya, Tumaini Haonga kwenye kikao kazi cha timu ya uhamasishaji wa hatua za afya mkoa wa Mwanza kilichoshirikisha viongozi wa dini, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, viongozi wa bodaboda na waandishi wa habari.
Alisema makundi hayo maalumu ni vema wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata chanjo hiyo sanjari na kufuata maelekezo ya wataalamu na itatolewa kwa watu ambao hawana virusi, dalili za maambukizi ya ugonjwa ili miili yao iweze kupokea chanjo hiyo na kuujenga mwili na uwe imara dhidi ya UVIKO-19.
“Tunawaomba watu ambao watakuwa wamechanja chanjo hii inayotolewa kwa hiari waendelee kizingatia njia zote za kujikinga ili wasipate maambukizi kwani dawa hiyo hufanya kazi baada ya siku kadhaa, kufuata maelekezo ya wataalamu, sanjari na kumalizia dozi kwani chanjo hizo zipo za aina tofauti zinazotarajia kuingia.
Alisema ni vema wananchi kuendelea kuzingatia taarifa kutoka Wizara ya afya ili waweze kupata taarifa sahihi na kuondokana na upotoshaji na serikali imeweka nguvu kubwa kwa wataalamu wa afya, mabingwa na wabobezi kwa kutoa mafunzo makubwa ndani na nje ya nchi kwenye maeneo chanjo itakapotolewa.
“Wataalamu hawa tumekuwa tukiwatumia kwenye kutoa elimu na kuandaa miongozi mbalimbali na wanasaidia kukabiliana na tishio la maradhi ya ugonjwa wa mlipuko,”alisema Haonga.
Naye Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma mkoa wa Mwanza, Denis Kashaija alisema lengo la kutoa chanjo hiyo kwa makundi hayo ni kuwakinga na wimbi na wimbi la tatu la UVIKO-19 ingawa kila mtu anao wajibu wa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya na kufuata njia za kujikinga.
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho Mwenyekiti wa madereva bodaboda Wilaya ya Nyamagana Mohammed Mohammed na Mhudumu wa afya ya Jamii (CHW) Mosha Sitta walisema wataifikisha elimu waliyoipata kwa wananchi ili jamii ibaki salama dhidi ya UVIKO-19.
Naye Padri Faustine Bangwa ameongeza kuwa ataendelea kuwashawishi waumini na kuwapatia elimu ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kwa lengo la kuwakinga dhidi ya UVIKO-19.