23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda, Sirro washikana pabaya

masiro

JONAS MUSHI NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

SASA ni dhahiri kwamba sakata la kilevi cha shisha limewavuruga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro, baada ya kila mmoja kutoa utetezi wake wa namna operesheni za kukidhibiti inavyofanyika.

Hali ya kuvurugana huko imetokea baada ya Makonda kumtuhumu Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo cha uboreshaji huduma za umeme, iliyofanyika Dar es Salaam juzi, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba huenda wanapokea rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa kikundi cha wafanyabiashara 10 (kila mmoja aliahidi kutoa Sh milioni tano) wa kilevi hicho waliomshauri azichukue yeye kila mwisho wa mwezi ili waendelee kufanya biashara hiyo, lakini alikataa kwa kile alichodai kuwa walikuwa ni mawakala wa shetani.

Makonda aliendelea kutoa tuhuma hizo kwamba, pengine kutokana na rushwa hiyo ndiyo maana Sirro na Kaganda wanalegalega kuwakamata wafanyabiashara hao waliomfuata ofisini kwake, licha ya kuwaagiza kufanya hivyo.

Licha ya Makonda kutoa tuhuma hizo, lakini Majaliwa alimtaka kufuatilia maagizo aliyowapa kina Sirro na asipofanya hivyo atamwajibisha kwa kushindwa kusimamia maagizo yanayotolewa na viongozi wa juu serikalini, ikiwamo kupiga marufuku biashara ya shisha jijini Dar es Salaam.

Kutokana na tuhuma za kina Sirro kuibua mjadala, Makonda aliendelea kuzizungumzia katika kipindi cha Power Break Fast, kilichorushwa jana na Kituo cha Redio cha Clouds FM, kwa lengo la kutoa ufafanuzi zaidi na alisema anashangaa kuona vyombo vya habari vikizungumzia zaidi kauli yake badala ya kuelimisha madhara ya shisha.

“Nilifikiri watu wote wenye fikra pana wana wajibu wa kutafuta madhara ya shisha kuliko kuhangaika na kauli ambayo madhara yake hayapo,” alisema Makonda na kuongeza:

“Jana (juzi) tulikuwa na maadhimisho ya watoto njiti duniani na moja ya sababu zinazosababisha watoto hao ni utumiaji wa shisha, nilifikiri ningeona leo (jana) vyombo vya habari vimelizungumzia hilo, lakini hakuna kilichofanya hivyo.”

Pia alipoulizwa kwanini hakuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara 10 waliotaka kumpa rushwa, Makonda, alisema si kila hatua inayochukuliwa inasemwa.

“Haujui hatua zinazochukuliwa, si kila hatua inasemwa. Ukifanya jambo kama hili maana yake unatangaza katika namna mbili  mbili, kwanza unaongeza awareness (uelewa) kwamba hawa watu, si kwamba wanafanya biashara ya shisha kwa sababu ni biashara, bali wanatafuta faida kwa nguvu yoyote, hata ya kukuangamiza wewe unayekwenda kutumia,” alisema Makonda.

Kuhusu kuwataja wafanyabiashara hao katika vyombo vya kuzuia rushwa, alisema hakuwataja hadharani kwa sababu majina yanatajwa katika vyombo husika.

“Pale sikutaja majina kwa sababu majina yanatajwa katika vyombo husika, kwa hiyo wenye vyombo wakienda kuuliza watapata majibu kuwa kuna taratibu gani zinazochukuliwa,” alisema Makonda.

Alipoulizwa kwanini hakwenda kumuuliza Majaliwa suala la kutoa vibali vya shisha akasubiri kwenda kusema hadharani alisema: “Nilimuuliza hadharani ili wale wanaosingizia na kudanganya watu kuwa Waziri Mkuu ametoa vibali waweze kusikia hadharani majibu yake.

“Alichosema waziri mkuu ni kwamba, hatoi kibali na hatua lazima zichukuliwe kwa watu wanaoendelea kuuza.”

Pia alisema aliwatilia shaka kina Sirro kwa sababu alifanya msako mwenyewe na kukamata watu wanaouza shisha, licha ya jeshi hilo kumwambia hakuna wauzaji.

“Nimepita maeneo 10, likiwemo karibu na kwa Mzee Mwinyi (nyumbani kwa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (Mikocheni) anapoingilia getini kwake pale pembeni tumekuta watu wanauza shisha, Dar Free Market wanauza shisha, Maisha Basement wanauza shisha na mengine mengi,” alisema Makonda na kuongeza:

“Kila ninapouliza Jeshi la Polisi wananiambia operesheni inaendelea na taarifa nilizopewa hiyo kitu hakuna. Lakini mimi nimekamata hawa watu tumekuta watoto hadi wa miaka 20, 18, wakati tunahangaika kutoa mikopo kwa wanafunzi wengine wanavuta shisha. Ndiyo maana katika nukuu yangu nikasema mzee huu ukimya wale walionipitia hawajawapitia na kuwapa polisi rushwa?”

Makonda aliendelea kusema kuwa, polisi wanafanya kazi kubwa ya kupambana na majambazi, lakini wauzaji wa shisha nao ni majambazi wanaotumia teknolojia ya shisha kuua vijana.

Alisema alichotaka ni kuhakikisha hakuna mtu anayemilikishwa suala la shisha kwa sababu watu wengi wamekuwa wakitupia mpira watu fulani.

“Mimi pale nilichokuwa nakitafuta ni hii shisha, asiwepo mtu anayemilikishwa kwamba hii shisha ni fulani na wengine wanahoji kwani wewe una uchungu gani na maisha yetu kuliko wazazi wetu. Mimi ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, ikiwemo usalama wa afya za watu, hivyo ni wajibu wangu,” alisema Makonda.

Alisema aliweka suala hilo hadharani kwa sababu mambo yote yanafanyika hadharani, ikiwemo uuzaji wa shisha.

Pia alirusha vijembe kwa watu wanaomkejeli kuhusu hatua anazochukua.

“Hata kama watu wote wataona kwamba niko kinyume katika suala hili na lipo moja ya gazeti limeandika Waziri Mkuu amuumbua Makonda, acha niumbuke kwa kulinda afya za watoto wao, ipo siku watanishukuru,” alisema Makonda.

Kwa upande wa Sirro, licha ya kuahidi juzi kuwa angezungumzia tuhuma hizo kwa waandishi wa habari ofisini kwake jana, lakini aliahirisha hadi keshokutwa Jumatatu kwa kile alichodai kuwa ni kutokana na dharura aliyoipata, lakini alizungumzia kwa ufupi alipohojiwa na Kituo cha Redio cha Times Fm cha Dar es Salaam.

Akizungumza kupitia kipindi cha Sunrise,  kinachorushwa asubuhi na kituo hicho, Sirro alimtaka Makonda achukue hatua  kulingana na nafasi aliyonayo ya Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Dar es Salaam, kama atakuwa na wasiwasi na utendaji wa polisi katika operesheni ya kuondoa wafanyabiashara wa kilevi hicho.

“Mkuu wa Mkoa ana wasiwasi, huo ni wasiwasi na ubaki kuwa wasiwasi, kikubwa niseme sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, yeye ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama na kama atakuwa na wasiwasi na chombo chake najua atatuita na kutuambia nini cha kufanya, lakini kama ana wasiwasi zaidi yeye ni kiongozi, atajua achukue hatua gani dhidi ya sisi,” alisema Sirro.

Pia alisema operesheni ya kutokomeza shisha jijini Dar es Salaam inaendelea na hadi sasa watu waliokamatwa ni wengi na taratibu zinafanyika ili kuweza kuwafikisha mahakamani.

“Kinachofanyika lazima jalada lipelekwe kwa wakili wa Serikali ili kuandaa mashtaka na kupeleka mahakamani, kazi inafanyika, labda kama tutacheleweshwa na masuala ya ushahidi,” alisema Sirro.

Kuhusu wafanyabiashara 10 wa shisha waliotaka kumpa rushwa Makonda ili kumziba mdomo, alisema hawezi kusema chochote katika hilo.

“Mkuu wa Mkoa ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama, aseme yeye alipeleka wapi? Maana vitu vingine ni siri, siwezi kumsemea kama alipeleka wapi, ukimaliza kuongea  na mimi mtafute umuulize alipeleka wapi anaweza akakujibu,” alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema licha ya tuhuma za kina Sirro kufikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), lakini wao pia wana utaratibu wa kuchunguza tuhuma zinazotolewa dhidi ya polisi.

Kauli hiyo aliitoa alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

“Kuna taasisi maalumu ya kuhusiana na rushwa inachunguza suala hilo, lakini na sisi tumepokea kama tuhuma na kwa mujibu wa taratibu zetu, tuhuma zote zinazotolewa kwa askari wetu zinachunguzwa,” alisema.

Wakati Boaz akitangaza uchunguzi huo, Takukuru nayo imetangaza kuanza kumchunguza Sirro na Kaganda dhidi ya tuhuma hizo, zilizotolewa dhidi yao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles