*Aingia studio na polisi, maofisa wa idara nyeti wenye silaha nzito
*Hofu yatawala, Nape, Bashe, Lissu, Mbowe watoa neno
Na ASHA BANI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anadaiwa ‘kuteka’ kituo cha redio jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi majira ya saa 4:46 usiku ambapo video zake zilianza kusambazwa jana kwenye mitandao ya kijamii zikimwonesha Makonda akiingia katika ofisi za studio za redio na Televisheni ya Clouds, huku akiwa na polisi na makachero wa idara nyeti ya Serikali ambapo walikuwa wamebeba silaha nzito.
Taarifa kutoka ndani ya Clouds Media zinaeleza kwamba Makonda alivamia kituo hicho usiku, huku baadhi ya vipindi vikiwa vinaendelea kwa kuendeshwa na watangazaji wa zamu.
Inaelezwa kwamba Makonda alifika katika kituo hicho na kudai kwenda kuwatisha kwa kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kilichokuwa chini ya Mtangazaji ‘Soudy Brown’…
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaama kama vita ya mashambulizi anayoyapata kutoka kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye anaendelea kurusha ‘makombora’ yake kuhusu madai ya kiongozi huyo kughushi vyeti.
Kwa mujibu wa habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa Clouds Media ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini kwa kuhofia usalama wao walisema kiongozi huyo wa mkoa hufika katika kituo hicho mara kwa mara lakini kwa staili aliyoitumia juzi imewatia hofu kiasi cha kujenga shaka naye.
Makonda alifika Alhamis katika ofisi hizo na kukaa mpaka usiku huku akimtafuta mwendesha kipindi cha Shirika la Wambea Duniani ‘SHILAWADU’ Soudy Brown na Qwisser ambao muda huo walikuwa bado hawajafika kazini.
“Baada ya kuona watangazaji hao hawajafika alianza kuzunguka zunguka katika ofisi hizo mithili ya mfanyakazi wa Clouds.
“…kwenye mida ya saa 10 hivi akakutana na kina Soudy pamoja na prodyuza wa kipindi wakawa wanaongea kwa uficho hivi na usiri tukajua tu ni mambo ya kawaida ya kuhitaji uprivate lakini siku ile ilikuwa inatia shaka sana,’’ kilieleza chanzo hicho.
Inaelezwa kwamba Makonda alikwenda Clouds akiwa na habari iliyomuhusu mwanamke mmoja ambaye alidai amezaa na Mchungaji Gwajima aliyemtekeleza akawa anataka arekodiwe na ‘ubuyu’ uruke kwenye kipindi cha Shilawadu.
“Walikubaliana habari ya mwanamke huyo arekodiwe na kipindi kiruke siku ya jana (juzi) na kawaida ilikuwa kila mtu apewe nafasi ya kujieleza katika pande mbili ambazo zinatuhumiana.
“Makonda siku hiyo hiyo ya Alhamisi akamwambia Soudy ajiandae halafu huyo mwanamke mnayemuona kwenye video na mtoto aliletwa na wasaidizi wa Makonda ahojiwe na Soudy Brown tayari kwa kurushwa kwa kipindi,’’ alidai mtoa taarifa huyo.
Taarifa hizo zinaeleza kwamba Ijumaa ambayo ilikuwa Shilawadu wamtafute Gwajima kwa upande wake kama analifahamu hilo suala kuhusu mwanamke huyo kwani wanafahamu ugomvi uliopo kati ya Makonda na kiongozi huyo wa kiroho.
‘Kwa bahati mbaya Gwajima hakupatikana jana Ijumaa kwa ajili ya kurekodiwa na kufanyiwa mahojiano. Shilawadu wakatumia busara mpaka apatikane Gwajima tukio la dada mwenye mtoto ziende kwa pamoja na ya Mchungaji Gwajima kama kawaida ya povu inavyokuwaga,’’ alisema
Kwa mujibu wa kipande cha video ambacho kimerekodiwa kupitia Kamera za CCTV zilizopo katika studio hiyo zinaonyesha kwamba Makaonda alifika katika studio hizo saa 4:46 usiku huku akiwa na askari kama wanane huku nyuma kukiwa na kijana ambaye alikuwa amepigwa bumbuwazi kutokana na maelekezo ya askari hao waliovalia nguo za polisi pamoja na wale wa idara nyeti wa Serikali wakiwa wameshika mitutu ya bunduki.
Walipoingia mapokezi Makonda na askari hao waliingia ndani ambapo ilielezwa walikwenda moja kwa moja hadi studio ambapo walikuta watangazaji wakiwa wanamalizia kipindi cha Shilawadu.
“Geti la kawaida mlinzi alifungua geti kwasababu amezoeleka Makonda anafikaga mjengoni wakafunguliwa kisha wakaingia ndani, walipofika mapokezi wakazuiwa kuingia ndani sababu hakuna utaratibu wa kuruhusu wageni baada ya saa nne usiku kama siyo mfanyakazi wa Clouds,’’ ilieleza taarifa za ndani.
“Makonda akawatoa nje Soudy na mwenzake Qwisser akawauliza kwanini video aliyowaletea haijachezwa wakaelezea jinsi utaratibu ulivyokuwa. Qwisser wakati anajielezea akapigwa mtama akaanguka chini wakavamia mitambo ya transmission kwenye traycaster wakitaka kile kipande kirushwe hewani prodyuza wa kipindi akamuambia Makonda kwanini anavunja utaratibu na kutumia nguvu na ameshapewa utaratibu akapigwa na kitako cha bunduki mgongoni akaanguka chini bahati mbaya kipindi kilikuwa kimefika mwisho,’’ alisema mtoa taarifa huyo.
Kutokana na hali hiyo inadaiwa Makonda akiwa na polisi hao pamoja na wale wa idara nyeti walimshurutisha Prodyuza wa Shilawadu aliyetajwa kwa jina la Chriss awape kile kipande na cha video ya mwanamke huyo na kuondoka nacho kusikojulijkana.
Uongozi wajichimbia
MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo alimtaka mwandishi amtafute baada ya muda.
“Dada samahani naomba nizungumze baadaye ,’’ alisema Ruge na kukata simu.
Alipotafutwa tena hakupatikana hadi hapo tetesi za kuwa Ruge alikuwa akihojiwa Kituo cha Polisi Ostarbay zilipopatikana, ambapo alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda, alisema hana taarifa za kuhojiwa kwa Mkurugenzi huyo wa Clouds Media Group.
“Sina taarifa za kuhojiwa kwa Ruge asante,” alisema Kamanda Kaganda.
Hata hivyo taarifa za ndani ziliambia MTANZANIA kuwa kutokana na tukio hilo jana menejimenti ya kampuni hiyo ilikutana kwa dharura kujadili tukio hilo ambalo watalitolea taarifa maalumu.
Katika mtandao wa kijamii wa kundi laWhatApp la ‘Hapa Kazi tu 2015-2020’ alinukuliwa Ruge akipinga kitendo hicho ambapo aliandika kuwa “Kilichotokea sio sawa kabisa kinaumiza sana sana na naogopa sana future yetu inaelekea wapi, kijana wa miaka 28 anapopata presha kwa uoga kwenye nchi kama Tanzania inasikitisha .
“Nitazungumza wakati mwafaka ukifika ila kwa sasa tuna tension kubwa Clouds acha vijana watulie kwanza tutaongea baadaye,’’ aliandika Ruge.
Hata hivyo ilipofika saa 11 jioni Clouds Media Group, ilitoa tamko la awali lilisema
Tamko la Clouds Media Group
Mkurugenzi wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba ametoa taarifa yenye ufafanuzi wa tukio linalomuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kumekuwa na habari mbalimbali akiwepo Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Kiini cha habari hizi ni uwepo wa taarifa zinazomuhusu mwanamke anayedai kuzaa na askofu Gwajima.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa ni kweli habari ya uwepo wa mama huyo iliwafikia kupitia kipindi cha ‘De weekend chat show’ (SHILAWADU)lakini baada ya uchunguzi wa kina waligundua kwamba habari haina mashiko,inakosa vigezo vya habari inayofaa kuonyeshwa na kusimamia katika kanuni za taaluma na kuzuia kuonyeshwa kwa taarifa hiyo.
“Kuzuiwa kwa taarifa hiyo kumezua matukio mbalimbali ikiwemo mijadala inayosambaa juu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,’Paul Makonda’ kuvamia kuvamia ofisi zetu,pia kumekuwa na video zinazosambaa kuhusiana na matukio hayo,’’
Jambo hili limezua hofu kubwa kwawadau wote wanaojali uhuru wa vyombo vya habari lakini hofu pia imetanda kwa wafanyakazi wote wa Clouds Media Group .
Taarifa hiyoiliendelea kueleza kuwa pamoja na ukweli wa mengi wa matukio hayo, jambo hilo lipo katika uchunguzi wa kina unaofanywa na wenyewe Clouds media Group.kwa kushirikiana na mamlaka zote zinazohusika.
“Tunaomba radhi kwa madhara yoyote na jambo hili na tunawaomba Watanzania wote kutupa muda zaidi kabla ya kutoa tamko rasmi kuhusu yote yaliyotokea. Katika kipindi hiki na katika siku zijazo tunaendelea kufanya kazi kwa weledi na viwango huku tukiendelea kugusa watu kwa kuwa sisi ni redio ya watu na Televisheni ya watu,’’ alisema Ruge katika tamko lake.
Nape Nnauye
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, alisema leo atatembelea Clouds Media Group ili kujua kilichotokea.
“Kesho asubuhi (leo) kama waziri mwenye dhamana na habari nitatembelea Clouds Media kujua kilichotokea , nawaomba sana wanahabari nchini kutulia kwa sasa,” alisema Waziri Nape.
Hussein Bashe
Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alivitaka vyombo vya ulinzi kulinda heshima yake.
“Kumekuwa na total mis use nimeona Dodoma kwangu binafsi na hili la Clouds lazima lilaaniwe ,’’alisema Bashe katika ukurasa wake wa Tweet.
Kauli hiyo ya Bashe imetokana na kukamatwa kwake kabla wakati wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ambapo ilidaiwa mbunge huyo alikuwa amebeba anjenda ya kwenda kumpinga Mwenyekiti.
Elibariki Kingu
Naye Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), alisema amesikitishwa na kitendo hicho na kumtaka Rais Dk. John Magufuli huku Idara ya Usalama wa Taifa ikikaa kimya na CCM ikiendelea kutukanwa kila kona.
“Nilisema nitanyamaza lakini nimeshindwa, nimethibitisha bila mashaka Clouds kuvamiwa na RC akiwa na ulinzi na askari wenye silaha mpaka kwenye matangazo.
“Najua hofu mliyonayo Watanzania juu ya huyu RC, ikiwa mamlaka zitaendelea kufumbia macho, mimi Elibariki Kingu mbunge wa CCM nitakuwa wa kwanza kufukuzwa CCM kama kupinga matendo maovu ya RC huyu itaonekana ni usaliti kwa nchi,’’ alieleza Kingu.
Aliendelea kueleza kuwa haiwezekani Rais atukanwe kila kona kwa matendo ya Mkuu wa Mkoa huyo.
‘Wana CCM ukimya wetu kwenye hili halikubaliki. Rais Magufuli juzi ametuliza Dodoma kwa kuongea kwa hisia. Idara za usalama kweli mmeamua kuacha tutukanwe? Alihoji Kingu.
Kamanda Sirro
Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo alipokea simu na mwandishi alipojitambulisha na kuuliza swali alikata simu na kutojibu lolote.
Chadema watangaza ‘vita’
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa tamkoa na kuwataka viongozi wote kuanzia ngazi ya mitaa, madiwani, mameya na wabunge wa chama hicho kutompa ushirikiano wa aina yoyote kiongozi huyo.
Hatua hiyo imetokana na mkuu huyo wa mkoa kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi wa Chadema hadi pale atakapotoa ufafanuzi wa vyeti vyake vya elimu, mali pamoja na kuvamia kwake kituo cha redio cha Clouds na Tv vinavyomilikwia na Clouds Media Group.
Lissu na JPM
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Tundu Lissu ametoa tamko lake la kwanza na kumshauri Rais Dk. John Magufuli, atengue uteuzi wake haraka iwezekanavyo kabla hajachafua zaidi taswira ya Serikali na ya Rais Magufuli mwenyewe.
“Waheshimiwa wananchi wa Tanzania. Nimesikia taarifa za kuvamiwa kwa kituo cha habari cha Clouds Media. Mkuu wa Mkoa katika nchi yetu sio kamanda wa kikosi chochote cha jeshi lolote lililoanzishwa kwa mujibu wa sheria.
“Mamlaka aliyo nayo kwa mujibu wa sheria za nchi yetu hayajumuishi kuamrisha askari jeshi au polisi au usalama wa taifa kuvamia makazi au sehemu za biashara za watu.
“Mkuu huyu wa mkoa hastahili kuendelea kwenye madaraka hayo kwa siku moja zaidi. Hana tena sifa wala maadili wala sababu za kuendelea kuwa kiongozi wa umma,” alisema Lissu katika taarifa yake.