MAULI MUYENJWA NA LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda jana ameongoza na viongozi mbalimbali kuaga mwili wa aliyekuwa mwandishi wa habari, Adolf Kivamwo ambaye mazishi yake yalifanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu Kivamwo, Makonda alisema ni vizuri kumkumbuka kwa mema aliyoyafanya ikiwa ni pamoja na kuendeleza mambo mazuri aliyoyaacha.
“Hii ni safari ya wote, marehemu aliishi na sisi vizuri tumuombee Mungu, ni vizuri kumuenzi kwa mambo mema ambayo alikuwa akiyafanya katika jamii,”alisema.
Kutokana na kuguswa na msiba huo, Makonda aliahidi kuwalipia ada watoto wa marehemu Sh milioni 4 mwaka huu.
Viongozi wengine, waliokuwapo ni Mbunge wa Chalinze,Ridhiwani Kikwete (CCM), Mbunge wa Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji,Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), Mbunge wa Ubungo,Saed Kubenea (Chadema), Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP na Dk.Regnald Mengi.
Marehemu Kivamwo alifariki dunia Septemba 23, mwaka huu kwa maradhi ya saratani aliyokuwa akiuugua muda mrefu.