25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Meya Songea ‘afilisi’ Saccos Dar

MEYA wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji.
MEYA wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji.

Na Mwandishi Wetu,

MEYA wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji, ameingia matatani kutokana na tuhuma za ‘kufilisi’ chama cha kuweka na kukopa kijulikanacho kwa jina la Shirikisho Saccos, jijini Dar es Salaam.

Mshaweji ambaye ni Diwani wa Kata ya Subira katika Manispaa ya Songea kwa tiketi ya CCM, amekumbwa na kashfa hiyo baada ya kushindwa kulipa deni la mkopo wa Sh milioni 75. 789 kwa zaidi ya miaka mitano sasa na kuifanya Saccos hiyo kuwa taabani.

Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa, Mshaweji ni miongoni mwa wadaiwa sugu ambaye kwa kiasi kikubwa ameifanya Saccos hiyo ishindwe kujiendesha.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wanachama wameandika barua za kujitoa, kutokana na chama hicho kushindwa kutoa mikopo mipya kwa wanachama wake.

“Saccos hii imezorota kutokana na ukata uliopo, kasi ya uwekaji na utoaji wa mikopo kwa wanachama ni ndogo sana ni kama vile haupo kabisa.

“Msingi wa vyama hivi ni mikopo kwa wanachama wake. Saccos maana yake ni kuweka na kukopa, mwanachama anaweka fedha kutokana na malengo na malengo yake ni kupata mkopo ili afanya shughuli zake za maendeleo.

“Kuna wanachama wengi wanaohitaji mikopo wenye sifa lakini mikopo hakuna, hali hii inaathiri makuzi ya chama, kuna wanachama wameandika barua za kujitoa kwa sababu hawapati mikopo.

“Jambo hili halina afya katika chama, siyo kwamba Shirikisho haina fedha, fedha zipo lakini fedha zenyewe zipo mikoni mwa watu.

“Kuna baadhi ya watu na wengine ni wakubwa wamezikalia, wamekopa fedha nyingi lakini hawataki kurejesha ili wengine nao wakope,” kilisema chanzo hicho na kumtaja meya huyo.

Chanzo hicho kilisema kuwa, Mshaweji ambaye wakati huo alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika nchini (SCULT) na mlezi wa Shirikisho Saccos, alipewa mkopo huo mwaka 2006.

Chanzo hicho kiliendelea kusema, Mshaweji ambaye miongoni mwa wanachama waanzilishi wa Saccos hiyo mwenye namba 13, alitumia nafasi yake kushawishi menejimenti ya chama hicho kukopa kiwango hicho cha fedha.

Hata hivyo MTANZANIA ilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho Saccos, Habib Mhezi, kuzungumzia madai hayo ambaye alikiri kuwa meya huyo alichukua mkopo huo, ambao hadi sasa hajamaliza.

Mhezi alimtaja meya huyo kuwa ni chanzo cha kuzorota kwa Saccos hiyo kutokana na kushindwa kwake kumaliza kulipa mkopo wake.

Mwenyekiti huyo alisema mwaka 2006, Mshaweji alipewa mkopo wa Sh milioni 65. 083 ambao riba yake ni Sh milioni 10.706 na hivyo kufanya jumla ya deni la kopo kuwa Sh milioni 75.789.

Mhezi alisema, hadi Novemba 2012 Mshaweji alikuwa amerejesha Sh milioni 32.450 na hivyo kubakiwa na deni la Sh milioni 43.339.

“Mwaka huo ndo mwisho wa marejesho yake, hajafanya marejesho mengine tena. Tulichofanya tumechukua akiba yake Sh milioni 19.701 pamoja na hisa zake Sh 250,000 ukitoa hapo linabaki la Sh milioni 23.388.

“Hapo kuna adhabu kutokana na ucheleweshaji wa mkopo, adhabu yake ni Sh milioni 10.725 kwa hiyo deni lake halisi kwa sasa baada ya kutoa akiba na hisa zake ni Sh milioni 34.113.

“Kwa mujibu taratibu na katiba ya Saccos mwanachama akichelewesha rejesho la mwezi anatozwa faini asilimia 10 ya rejesho. Sasa mheshimiwa huyu aliacha kulipa tangu 2012.

“Kwa hiyo tukisema tufuate utaratibu huyu mtu anatakiwa kulipa fedha nyingi, lakini sisi kama bodi tumesema alipe hiyo milioni 34 tu ili wanachama wengine waweze kukopa,” alisema.

Alipoulizwa ni hatua zipi zitachukuliwa iwapo meya huyo atashindwa kulipa deni hilo, Mhezi alisema. “Wiki ijayo tunakikao cha bodi tutakwenda kujadili hatua za kuchukua, hii ni pamoja na kumfikisha katika vyombo vya sheria kwa sababu fedha hizi ni za wanachama,” alisema.

Kwa upande wake Mshaweji alipotafutwa na MTANZANIA kuzungumzia madai hayo, alimtaka mwandishi ampigie baada ya saa moja kwani asingeweza kuzungumza kutokana na watu wengi waliokuwapo eneo hilo.

“Niko njiani Manyoni na Dodoma hapa, siwezi kuzungumza hapa kuna watu wengi,” alisema. Hata alipoelezwa kuwa majibu yake ni muhimu kutokana na habari inamyohusu alisema. “Siwezi hapa, naomba nivulimie baada ya saa moja nitakuwa nimefika,” alisema.

Baada ya saa moja kupita mwandishi alimtafuta, lakini meya huyo alisema hawezi kuzungumza mbele za watu na badala yake akataka atumiwe ujumbe mfupi wa simu.

Hata hivyo wakati tunaenda mtamboni, meya huyo alimpigia simu mwandishi akisema hawezi kuzungumza naye hadi amtumie nakala ya kitambulisho chake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles