31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AJIBU MASHAMBULIZI

makonda

EVANS MAGEGE NA VERONICA ROMWALD – dar es salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amejibu mashambulizi yaliyotokana na mjadala wa mamilioni ya fedha anayoyatoa kupitia misaada anayoiahidi kwa wananchi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana katika Viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, alisema watu wanaohoji fedha anazozitumia kusaidia wananchi ni vichaa, wajinga na haiwahusu.

“Anayehoji ni mjinga, ni kichaa asiyejua kuhangaika na shida za watu akijifikiria yeye, ni vichaa na wajinga, badala ya kuhangaika kuwaza namna gani tunamsaidia mtu, wao wanawaza hela imepatikanaje, kama wewe huna huruma na watu, wengine hawana huruma?

“Mtu akija na njaa, hana chakula, akaja kugonga kwako ukampa chakula, mtu atakuuliza umelima shamba gani? Wanaohoji hata Mungu hawana, ni dalili kwamba watu wameishiwa upendo wa Mungu, huko ni kutokuhangaika na matatizo ya watu, kuhangaika na wale wanaoshughulika matatizo ya watu.

“Mtu ambaye ana Mungu, lazima atakuwa anashughulikia matatizo ya watu, mtu ambaye hana Mungu anashughulikia wale wanaoshughulikia matatizo ya watu. Kuna pande mbili, haki inasimama upande wa Mungu na dhuluma inasimama upande wa shetani, sasa kama mtu anasaidiwa unaanza kuhoji maana yake ni kwamba wewe upo upande wa shetani,” alisema.

Kwa sasa Makonda amekuwa mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kutimiza ahadi yake ya kutoa misaada iliyogharimu Sh milioni 164.

Makonda aliyejipambanua kama kiongozi mwenye wepesi wa kuwafikia wananchi na kutatua kero zao, hivi karibuni alifanya ziara ya siku 10 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na kusikiliza kero za wananchi, ambako aliahidi misaada ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa kero zinazoikabili jamii.

Hata hivyo, kitendo cha kutimiza ahadi zake kimeibua mitazamo mbalimbali inayojikita katika hoja ya wapi anakopata fedha, sababu za kuficha anakopata fedha na kwanini imekuwa rahisi kwake kutoa misaada hiyo.

Pia wengine wanataka kujua nguvu ya fedha aliyonayo katika kutoa msaada wakati Serikali yenyewe inabana matumizi kwa maendeleo makubwa ya nchi.

Baadhi ya misaada ambayo Makonda ametoa ni pamoja na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 3.9 katika kituo cha kurekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya na zawadi ya pikipiki mbili zenye thamani ya Sh milioni tatu kwa viongozi na watumishi walionyesha ufanisi katika majukumu yao.

Pia alitoa zawadi iliyogharimu Sh milioni 5.3 kwa watumishi wanne wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao wameonyesha utumishi bora na alitoa msaada wa Sh milioni moja kwa mjasiriamali mmoja wa Soko la Sterio ili kuimarisha mtaji wake.

Katika kuunga mkono jitihada za kukabiliana na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya kusambazia maji kwa wananchi wa Gongolamboto na Pugu, Makonda, alimkabidhi Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, hundi ya Sh milioni 13.

Alitoa msaada wa Sh laki tano ili kukamilisha ununuzi wa tenki la maji kwa wananchi wa Buyuni, Kata ya Pemba Mnazi. Msaada mwingine alioutoa ni Sh milioni 36 za mabati 2,000 ya ujenzi katika Sekondari ya Jitegemee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles