27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

MKEMIA MKUU ASIMULIA MIKASA YA VIPIMO VYA DNA

profes-samwel-manyele

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MKEMIA Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, amesema ofisi yake ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), inapata misukosuko inapochukua sampuli za vipimo vya vinasaba (DNA) ili kubaini uhalali wa watoto au wazazi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili ofisini kwake Dar es Salaam hivi karibuni, Profesa Manyele, alisema mara nyingine wakati wa upimaji kipimo hicho hutokea vurugu, hivyo kulazimika kuwatoa wahusika nje kwa nguvu ili shughuli zao za kiofisi ziendelee.

“Kuna wakati baadhi ya wapenzi au wanandoa ulazimika kufikishwa ofisini chini ya ulinzi wa polisi, huku wengine wakikataa kukubaliana na matokeo, hivyo kusababisha vurugu,” alisema.

Profesa Manyele alisema kutokana na hali hiyo, upimaji DNA huchukua karibu asilimia 90 ya kazi za GCLA na hivyo kuwapa wakati mgumu katika utendaji kazi zao.

Alisema kwa kawaida ofisi hiyo uchukua sampuli za upimaji wa DNA kwa wazazi na mtoto wakiwa pamoja, lakini inapokuwa vinginevyo inaleta shida.

“Hivi vipimo kuna muda mwingine tunapata shida kuvipata kwa sababu hatuwezi kumpima mmoja mmoja, lazima wahusika waje kwa pamoja.

“Upimaji unakuwa mgumu na kuibua vituko na misukosuko mzazi mmojawapo anapokuwa hayupo tayari… Unakuta mtu wakati mwingine hataki kupima, hivyo hulazimika kuletwa chini ya ulinzi wa polisi,” alisema.

Profesa Manyele alisema ili kuepusha hali hiyo, ofisi hiyo huwa inawashauri wanaosimamia vipimo hivyo kuhakikisha wanawaandaa wahusika kisaikolojia ili wawe katika maelewano mazuri kabla uchukuaji wa sampuli zao haujafanyika.

Pia alisema wapo watu wanaoshindwa kwenda kupima jambo ambalo ofisi yake inalazimika kutuma wataalamu na kuwafuata walipo ili kuchukua sampuli zao.

Alisema wazazi wengine wanafika katika ofisi hiyo na kuanza kulalamikia matokeo ya vipimo yanapotoka tofauti na matarajio yao.

“Unakuta mzazi katika hisia zake ameshajihakikishia kuwa huyo mtoto si wake, au wengine wanadhani ni wa kwake.

“Sasa ikitokea majibu yakatoka tofauti, mtu anakasirika, anakuja hapa anagonga mlango wa ofisi huku akilalamikia matokeo ya DNA,” alisema.

Alisema mara nyingi watu wanaofanya hivyo wanaenda kinyume cha utaratibu kwa kuwa mtu anayepaswa kulalamikia matokeo ni aliyepeleka sampuli za vipimo hivyo.

Profesa Manyele alisema kutokana na unyeti wa vipimo vya DNA, ndiyo maana vinafanyika kwa usimamizi wa vyombo vilivyotajwa katika sheria, ikiwamo mahakama, ustawi wa jamii, hospitali, manispaa au mkuu wa wilaya, wakili wa kujitegemea, polisi na vituo vya utafiti.

Pia alisema yapo makosa yanayofanywa na watendaji wa manispaa, wilaya na mikoa kwa kushindwa kutunza vizuri matokeo ya DNA baada ya kuyapokea.

“Utakuta mhusika anaenda katika ofisi za wilaya au manispaa anamkuta ofisa anamuulizia kuhusu karatasi ya matokeo, anakuwa hajui alipoiweka, akiitafuta unamwona anaitoa chini ya uvungu, unashangaa anawezaje kuweka vile nyaraka muhimu kama ile,” alisema Profesa Manyele na kuongeza:

“Kinachotokea watu wanapokea matokeo yale bila kufuata taratibu za kiofisi. Mtu analetewa matokeo hakuna sehemu ambayo anasaini wala kuandika kama amepokea kitu. Kwa kifupi hakuna usiri wa matokeo katika ofisi hizo.”

Alitaja makosa mengine wanayoyafanya watendaji ni kusoma au kutoa taarifa za matokeo ya vipimo hivyo mbele ya mtoto husika jambo ambalo si sawa.

“Mtoto hatakiwi kujua haya mambo. Waachwe wazazi wenyewe wasikilize. Ikitokea mzazi amekuja na mtoto kuchukua matokeo, watendaji wanapaswa wahakikishe wanamshauri wakati mtoto hayupo. Hii itasaidia kwa ustawi wa mtoto husika,” alisema.

Profesa Manyele aliendelea kusema kuwa watendaji wanapaswa kuhakikisha wanawaelimisha wahusika wachukuliwe vipimo kuondoa dhana potofu ya kufikiri  kuwa kipimo hicho pia kinapima Virusi vya Ukimwi (VVU) jambo linalosababisha watu kuogopa.

Mbali na kujua uhalali wa watoto au wazazi, pia alitoa sababu za watu kupima DNA kuwa ni pamoja na kutatua malalamiko ya kesi za urithi na kutambua ndugu halali.

Alisema pamoja na kesi za watoto wanaopata mimba za utotoni kuwa nyingi, lakini ofisi hiyo haipokei kwa wingi malalamiko hayo kutokana na wahusika kutojua kama chombo hicho kinaweza kuwasaidia.

“Maofisa elimu na walimu inabidi wafahamu kuwa ofisi ya mkemia mkuu ina nafasi kubwa sana ya kutatua migogoro ya mimba za utotoni baada ya mtoto kujifungua. Hivyo inakuwa rahisi kwa mhusika kuchukuliwa hatua,” alisema Profesa Manyele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles