26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Makinda aukimbia uspika

1126*Aingia mitini dakika za mwisho licha ya kampeni

*Mpambano mkali kwa Sitta, Nchimbi, Ndugai

 

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

VITA ya kuwania uspika wa Bunge, imepamba moto huku Spika anayemaliza muda wake Anne Makinda, akishindwa kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo, tofauti na ilivyotarajiwa.

Habari zilizolifikia MTANZANIA jana jioni zinaeleza kuwa, Makinda ameshindwa kuchukua fomu kutokana na ushauri aliopata kutoka kwa watu wake wa karibu wakiwamo makada wenye heshima ndani ya CCM.

Chanzo chetu cha habari kilichopo karibu na Makinda kimeeleza kuwa, pamoja na mambo mengine huwenda mwanasiasa huyo mkongwe ametishwa na idadi ya watu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo wakiwamo vigogo wenye majina makubwa.

Chama Cha Mapinduzi kilitangaza ratiba ya uchukuaji fomu za uspika kwa wanachama wake kuanzia juzi, ambapo kwa wagombea wasiokuwa wabunge wateule mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ilikuwa saa 10 jana jioni.

Baadhi ya vigogo waliochukua fomu ni pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, Naibu Spika anayemaliza muda wake, Job Ndugai na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi.

Kampeni za Makinda

Siku moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)kutangaza orodha ya majina ya wabunge wa viti maalumu, Makinda alianza kampeni zake kwa kuwaomba wabunge wateule kumpigia kura za ndiyo, ili awe Spika wa Bunge la 11.

Mbali ya kufanya hivyo, wapambe wake pia walikuwa katika harakati za kuwashawishi wabunge hao wateule kwa kujenga hoja ya kuhakikisha Spika huyo wa Bunge la 10 anendelea kuongoza muhimili huo.

Katika ujumbe wake mfupi aliotuma Spika Makinda kwa wabunge wateule ambao MTANZANIA iliupata ulisema:

“Mheshimiwa mbunge mteule nachukua fursa hii kukupongeza kwa dhati kwa ushindi ulioupata. Hii inaonesha imani kubwa waliyonayo wananchi wa jimbo lako, sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Hivyo Mungu kakuteua uwatumikie watu hawa na sisi Watanzania wote kwa ujumla, hongera sana.

“…mimi ndugu yako kwa unyenyekevu na heshima kubwa kwako kama mbunge wangu, naomba kugombea uspika kwa mara nyingine, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nakutegemea sana naomba uniunge mkono. Asante kwa ukarimu wako ubarikiwe,” ulisomeka ujumbe huo mfupi.

Baada ya kusambaa kwa ujumbe huo wa simu mijadala kadhaa iliibuka kuhusu uamuzi wa Makinda kuwania nafasi hiyo, huku wabunge wateule wakigawanyika katika makundi mawili. Moja linalomuunga mkono na jingine likimpinga.

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imeongozwa na maspika watatu, Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda, ambaye kwa sasa anamaliza muda wake.

Hoja zilizopita chini yake

Atakumbukwa namna alivyosimamia hoja ya sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo iliwang’oa mawaziri kadhaa wa Serikali ya awamu ya nne.

Mawaziri hao kung’oka kulitokana na utekelezaji wa maazimio ya Kamati teule ya Bunge iliyochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni hiyo. Kamati hiyo ya Bunge iliongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli.

Mawaziri hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Dk. Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi).

ESCROW

Spika Makinda pia atakumbukwa kwa namna alivyosimamia Bunge baada ya kuibuka kwa sakata la uchotwaji wa fedha za Escrow zaidi ya Sh. bilioni 200 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika sakata hilo baadhi ya mawaziri na vigogo wengine wa Serikali walipoteza nafasi zao kutokana na maazimio ya Bunge.

Waliong’oka ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyuma na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Kashfa hiyo iliibuliwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye katika uchaguzi wa mwaka huu ameshindwa kutetea jimbo hilo.

Kumbukumbu za Makinda

Anne Makinda, alizaliwa Julai 15, mwaka 1949, alikuwa Mbunge wa Njombe Kusini ingawa mwaka huu hakugombea nafasi hiyo.

Mwaka 2006-2010, alikuwa Naibu Spika wa Bunge katika Bunge la tisa,  na mwaka 1990 na 1995 alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Katika miaka ya nyuma alishawahi kushika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwa ni pamoja na kutumikia nafasi ya ukuu wa mkoa.

Mwaka 2008, alikumbana na zahama ya kutumiwa ujumbe mfupi wa simu zaidi ya 400 na za miito ya simu 200 zenye matusi ya nguoni kutoka kwa watu wakimtaka ajiuzulu baada ya kutangaza kuivunja Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Hatua hiyo ilitokana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza namba za simu za Spika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Dar es Salaam na kutangaza kutumia ‘nguvu ya umma’, kumlazimisha ajiuzulu.

Waliochukua fomu

Hadi kufikia jana makada waliochukua fomu ili kumrithi Makinda ni pamoja na Samuel Sitta, aliyekuwa Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Leonce Mulenda, Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk. George Nangale na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Wengine ni aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Muzamil Kalokola, Banda Sonoko, Simon Rubugu pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Kwa siku ya jana waliochukua fomu ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Ubungo, Dk. Didas Masaburi na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mbulu, Balozi Philip Marmo.

Wengine ni Naibu Spika wa Bunge anayemaliza muda wake na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai na Abdalah Mwinyi ambaye ni mtoto wa rais wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Wengine ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson, Julius Pawatila, Mbunge mteule wa Jimbo la Chato, Dk. Medard Kaleman, Diwani wa Kata ya Goba, Watson Mwakalila, aliyekua Mbunge wa Viti Maalum, Ritha Mlaki, Veraikunda Urio, Agnes Makune na Mbunge mteule wa Ilala, Mussa Azan Zungu.

NDUGAI ANENA

Akieleza sababu zilizomfanya achukue fomu ya uspika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Bunge la 11 lina changamoto nyingi, hasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wabunge wakiwamo vijana.

Alisema kutokana na hali hiyo anahitajika kiongozi mwenye hekima na busara ambaye ataweza kuliongoza Bunge katika kipindi chote cha mijadala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles