KIUNGO wa Klabu ya New York City FC, Andrea Pirlo, amesisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka katika klabu hiyo na kujiunga na Manchester City na Inter Milan kama taarifa zilivyosambaa.
Nyota huyo ambaye alikuwa anakipiga katika Klabu ya Juventus ya nchini Italia, alijiunga na Klabu ya New York City
wakati wa majira ya joto, lakini timu hiyo yenye mastaa kama vile David Villa, Frank Lampard na Pirlo imeshindwa kufanya vizuri msimu huu katika Ligi Kuu nchini Marekani ambapo imemaliza ikishika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi.
Kutokana na klabu hiyo kushindwa kuchukua ubingwa msimu huu, taarifa zilienea kwamba nyota huyo anatarajia
kuondoka katika ligi hiyo lakini amekanusha kupitia akaunti yake ya Twitter na kusema hana mpango wa kuondoka.
“Nimeshangaa kuona mitandao mingi nchini Italia ikitoa taarifa kwamba ninaondoka katika klabu yangu ya New
York City FC, hakuna ukweli wowote juu ya habari hiyo, nitaendelea kuitumikia ligi hii mpaka mwisho wa mkataba wangu,” alisema Pirlo kupitia akaunti yake ya Twitter.