Na Clara Matimo, Mwanza
Makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza wamefanya mafunzo ya uwandani(Mafunzo kwa vitendo) kwa ajili ya kutambua mipaka iliyopo kwenye ramani na kudodosa mipaka ya wana kaya waliomo katika ramani hiyo.
Wakizungumza na Mtanzania Digital, kwa nyakati tofauti leo Agosti 12, 2022 baadhi ya makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu wametaja changamoto walizokutana nazo katika zoezi hilo kuwa ni baadhi ya watu waliowafikia kutokukubali kutoa taarifa rasmi, kushindwa kuingia baadhi ya maeneo kutokana na uwepo wa ziwa Viktoria na kutozungumza kwa uwazi na ukweli.
“Tunatambua taarifa alizotoa mtu ambaye tunakwenda kumfanyia sensa si sahihi baada ya kutoa taarifa za awali na kadri unapoendelea kumhoji maswali kuhusiana na taarifa zilezile majibu yanabadilika hivyo unapata mashaka kwamba yawezekana taarifa nilizopewa awali si za kweli.
“Tunaomba viongozi wa serikali ya mtaa waendelee kutoa elimu katika vikao vyao mbalimbali kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa zoezi la sensa ya watu na makazi na pia watoe taarifa za kweli siku ya sensa kwa makarani wa sensa ili zoezi hili muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu lifanikiwe,” amesema Mary Nyirenda, Karani wa sensa.
Nao baadhi ya makarani pamoja na msimamizi wa sensa, 2022 waliokuwa eneo la ziwa namba mbili katika Kata ya Butimba iliyopo Wilaya ya Nyamagana akiwemo, Joyce Kaganda, Joseph Juma kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) na Nyanda Malulu (Msimamizi) wamesema uwepo wa ziwa imekuwa ni changamoto katika kutambua mipaka maana ramani inaonyesha inatakiwa waende mbele lakini mbele kuna ziwa.
“Changamoto hii tumeitatua kwa kuwa tuko na viongozi wa mtaa ambao wametusaidia sana kutuelekeza njia ya kupita kuna maeneo ambayo inabidi urudi nyuma uzunguke ndiyo uyafikie maana kwa kufuata ramani unajikuta umefika ziwani,” amesema Joyce.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mafunzo ya sensa ya watu na makazi kituo cha Ualimu Butimba, Innocent Mujaya, amesema zoezi hilo la siku moja ni utekelezaji wa mafunzo kwa vitendo.
“Kituo changu kina makarani na wasimamizi wa sensa wapatao 352, tulianza mafunzo ya nadharia sasa tuko mafunzo kwa vitendo, kuna mambo ya msingi yanayopaswa kufanyika kabla ya sensa, wakati wa sensa na baada ya sensa hivyo zoezi la leo ni moja ya mambo ambayo yanapaswa kufanyika kabla ya sensa.
“Moja ya mambo muhimu ya kufanya kabla ya sensa ni kutambua mipaka iliyopo kwenye ramani kama tunavyofanya leo ambapo kila karani anatambua mipaka yake ambayo atafanya zoezi la udodosaji, atatakiwa adodose waliomo ndani ya mipaka yake haruhusiwi kutoka nje ya mipaka yake,”ameeleza Mujaya.