PARIS, UFARANSA
MAKAMU wa Rais wa Guinea ya Ikweta, Teodorin Obiang, ameshtakiwa nchini Ufaransa akituhumiwa kupora mali za nchi yake na kuzitumia kugharamia maisha yake ya anasa.
Obiang ambaye pia ni mtoto wa rais wa muda mrefu wa Guinea ya Ikweta, Teodoro Obiang Nguema, anatuhumiwa kuchota zaidi ya dola milioni 100 kutoka hazina ya Serikali.
Fedha hizo anadaiwa alizitumia kununulia jumba la kifahari katika mtaa wa matajiri jijini Paris, na magari kadhaa ya kifahari yanayotengenezwa nchini Italia.
Teodorin Obiang, mwenye umri wa miaka 47, hakuwapo mahakamani wakati mashtaka dhidi yake yakisomwa na wakili wake ameomba muda zaidi wa kuandaa utetezi.
Mahakama imesema itaamua leo ombi hilo la kuahirishwa kwa kesi hii, uamuzi ambao Shirika la Kimataifa dhidi ya Rushwa, limesema ni mbinu ya kuchelewesha haki kutendeka.