Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Yanga tayari imemalizana na Heritier Makambo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili leo akitokea Horoya FC ya nchini Guinea.
Makambo ambaye amerejea Jagwani kwa mara ya pili anakuwa mchezaji wa tatu kutambulishwa na Wananchi katika kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao.
Nyota wengine ambao tayari wameshasaini mikataba na klabu hiyo, ni Fiston Mayele kutoka AS Vita ya DR Congo na Yusuf Athuman aliyekuwa Biashara United.
Hata hivyo, Yanga ambayo msimu ujao inatarajiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inatajwa kuwasajili, Dickson Ambundo(Dodoma Jiji), Shaaban Djuma(AS Vita) na Jimmy Ukonde (UD Songo).
Akizungumzia usajili unaoendelea, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Hersi Said, amesema watafanyia kazi maeneo yote yaliyokuwa na mapungufu katika msimu uliopita kwa kuzingatia matakwa ya mwalimu, kulingana na kile alichokiona kikosini.