28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAMBA APIGILIA MSUMARI POMBE YA VIROBA

Na JUSTIN DAMIAN


OFISI ya Makamu wa Rais Mazingira, imeweka masharti magumu kwa watengenezaji wa pombe kali inayofungashiwa kwenye plastiki maarufu kama ‘viroba’ ambao  wanasema watahitaji muda wa ziada kabla ya kuhamia kwenye chupa.

Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira January Makamba aliwaambia waandishi wa habari   Dar es Salaam jana kuwa  dhamira  ya Serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa urahisi wa pombe hiyo.

Alisema hiyo ni  kutokana na kufungwa kwenye plastiki na kwa ujazo mdogo jambo linalozidisisha matumizi  hadi kwa watoto.

“Iwapo kuna wazalishaji watakaohitaji muda wa ziada wa kuhamia kwenye chupa, wataomba kibali maalum cha muda mfupi ambacho hakitatolewa hadi mwombaji awasilishe kabla ya tarehe 28/02/2017,” alieleza Waziri Makamba.

Kuhusu masharti mapya kwa waombaji, Waziri Makamba aliyataja na ushahidi/barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Nyingine ni ushahidi/barua/cheti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),  cheti au barua kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  pamoja na Cheti cha Tathmini ya Athari za Mazingira (NEMC)/Ofisi ya Makamu wa Rais

Alisema vigezo vingine ni ushahidi kwamba katika kipindi cha mpito mzalishaji atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji wa vifungashio  bandia (anti-counterfeit technologu) na uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuhusu usajili wa kampuni na usajili wa chapa ya kinywaji (brand)

“Haya ni baadhi tu ya masharti na tunaamini yatasaidia kuondoa tatizo hili la pombe ya viroba kwa asilimia zaidi ya 90,” alisema.

Makamba alisema  akiwa kama waziri mwenye dhamana ya mazingira, atatunga kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali kwa mujibu wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Alisema  zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashiwe kwenye chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) na kwa ujazo usiopungua milligram 250.

“Kanuni zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji nchini na matumizi ya pombe zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya malighafi  ya vifungashio vya plastic (viroba) vitakavyotumika kufungashia pombe kali.

“Atakayekiuka masharti ya kanuni atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja,” alifafanua

Alisema biashara ya viroba pamoja na athari zake kwa mazingira kutokana na kuzagaa, pia inakadiriwa kuipotezea Serikali Sh bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi.

Wafanyabiashara wapinga

Baadhi ya wafanyabiashara wa vileo   wamelalamikia uamuzi wa Serikali kupiga marufuku uuzaji wa ‘viroba’ kwa madai kuwa muda uliotolewa ni mfupi mno, anaripoti ABRAHAM GWANDU kutoka Arusha.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti tangu jana, walisema hatua hiyo ni uonevu na haipaswi kufanywa na serikali inayojali wananchi wake.

Katika ziara yake mkoani Manyara mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alisema Serikali imepiga marufuku pombe hizo kwa sababu zinatumiwa vibaya wakiwamo wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabashara wenzake wa maduka ya jumla na reja reja, Meneja wa duka la jumla la J.J Lombure Enterprises, Innocent Shange alisema wanaunga mkono hatua iliyochukuliwa na serikali.

Hata hivyo alisema   kwa bidhaa inayozalishwa nchini ilitakiwa wenye viwanda na wasambazaji wapewe muda wa kutafakari.

"Sisi tumenunua mzigo mkubwa kwenye stoo yetu kutoka kiwandani, hatujui nani atarudisha gharama zetu.

“Viwanda vimezalisha kwa wingi itakuwa hasara kubwa na itarudisha nyuma mitaji ya wauzaji wadogo.  Je, fedha tulizonunulia bidhaa hizo zitarudishwa na nani?” alihoji mfanyabiashara huyo.

Baadhi ya wamiliki wa viwanda vya uzalishaji wa vinywaji vya  Mega Trade Investment Limited na Banana Investment vya Jijini Arusha walisema tayari wameanza utekelezaji wa agizo la serikali pamoja na mazungumzo yanayoendelea kwa manufaa ya pande zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles