Na Brighiter Masaki
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amepiga marufuku kuingia kwenye vyombo vya usafiri, ikiwamo daladala na sehemu za kutoa huduma bila kuvaa barakoa kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.
Makalla ametoa maelekezo hayo baada ya mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, huku akipanga kufanya ziara za kushtukiza kwenye vituo mbalimbali.
“Tutakuwa na ziara ya kushtukiza kwenye vituo vya daladala, Feri, mabasi ya mwendokasi, maeneo ya masoko na sehemu zote za kutoa huduma ili kuangalia utekelezaji wa agizo hili,”amesema Makalla.
Aidha ameitaka Mamlaka ya Usafiri Ardhini ( LATRA), kusimamia magari ya abiria kuhakikisha inakuwa ‘level seat ‘kuepuka uambukizwaji wa ugonjwa huo.
“Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya isimamie utekelezaji wa mwongozo wa Wizara ya Afya na vyombo mbalimbali kutekeleza kupunguza msongamano wa abiria na ukishaona kumejaa acha tafuta usafiri mwingine,” amesema Makalla.
Aidha Makalla amesema Serikali imejipanga kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wote watakaofika hospital na kuwataka wananchi watakaoona dalili za Corona kuwahi vituo vya Afya.