24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Wanafunzi wapunguza kunawa mikono shuleni

Na Renatha Kipaka, Kagera

WANAFUNZI wamepunguza kunawa mikono wakiwa shule kiasi cha mwezi mmoja tu baada ya shule kufunguliwa toka zilivyofungwa kutokana na ugonjwa wa Covid- 19.

Kwa karibu mwaka mzima dunia imekumbwa na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababisha virusi vya corona, na japo sasa imetangazwa kuwa maradhi hayo hapa nchini yamekoma, bado kuna haja ya kuchukua tahadhari kubwa, hasa kwa wanafunzi.

Justa Mwombeki (13) ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kashai, Bukoba, maoni yake ni kuwa kwanza panahitajika umakini mkubwa kuhusu ugonjwa huo kwani tangazo kwamba ugonjwa umeisha limechangia sana wanafunzi kujiamini na kuona kawaida na hivyo kutochukua tahadhari.

Mwombeki anasema si kwamba tahadhari kama kunawa mikono imeisha la hasha, maana hata kabla ya ugonjwa huu kutajwa kuwa upo wanafunzi walikuwa wakinawa mikono walipokuwa wakitoka chooni kama ilivyo kawaida.

“Mimi nimekuwa shahidi.Walimu wetu wakitusisitiza kunawa mikono ili tusipate magonjwa ya mlipuko kwa kutumia vibuyu chirizi ili tuwe salama.
“Hivyo hata sasa ugonjwa wa Covid-19 umetupa somo kuwa hatupaswi kuishi kwa mazoea,” anasema Mwombeki.

Anaeleza kuwa baada ya Covid 19 kuingia uliwekwa mkazo na hata majumbani wazazi walihimizwa kuweka utaratibu wa kunawa kwa kutuma vibuyu chirizi kwa maana hiyo kazi ilikuwa nyepesi kudhibiti gonjwa hilo.

“Naweza kusema kuwa kwa nafasi kubwa sisi wanafunzi tulikuwa mabalozi katika kuzibiti tatizo la Covid 19 majumabani kwetu na kupita sisi watoto wazazi wetu nao walifuata taratibu za afya kwa umakini mno,” anasisitiza Mwombeki.

Lakini anasema kazi haikuwa nyepesi kwani “Kuna wanafunzi wenzetu wanaotoka pembezoni kiukweli kazi haikuwa nyepesi kuhakikisha wanakubali kunawa mikono mara kwa mara maana si kawaida yao,” anasema.

Mwombeki anasema kwa hulka za binadamu watu wana desturi ya kusahau mapema, na kwa janga hili la Covid 19, inaelekea watu wamesahau mapema sana;

“Hivyo niombe serikali itengeneze mfumo wa afya katika shule zote ili kuwaweka tayari watoto.

“Nitoe ushauri kwa wanafunzi wenzangu kuwa waendelee kupeleka taarifa kwa wazazi wao kuwa usafi ni zaidi ya Covid 19 maana kuna magonjwa yatokanayo na uchafu ambayo ni hatari kwa binadamu,” anasema Mwombeki.

Kwa mujibu wa Mwombeki, wazazi wazingatie kanuni za afya, wajue kuwa usafi ni kati ya stadi za maisha maana mtoto anapokuwa katika hali ya usafi anasoma akiwa huru na huweza kujikinga na magonjwa hatari ya mlipuko.

Mwombeki anasema usafi ukitiliwa mkazo Serikali itaepuka kutumia fedha nyingi kununua dawa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko na badala yake itafanya maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake, Baraka Matayo, 14) anayesoma katika mojawapo ya shule binafsi kwenye Manispaa ya Bukoba alisema kuwa pamoja na kwamba ugonjwa wa Covid 19 umetangazwa kwisha wao wameendelea kupimwa joto wakati wa kuingia darasani.

Matayo anasema kuwa vibuyu chirizi bado vipo lakini havitumiki kama ilivyokuwa hapo awali.

“Wakati ugonjwa ulipotangazwa kuwa upo nchini tulikuwa tunanawa mara nyingi. Mfano, mimi nilikuwa ninanawa mikono wakati wa kuingia darasani, kutoka darasani, wakati wa kunywa uji na wakati wa kutoka chooni.

“Lakini sasa ninanawa wakati wa kutoka chooni tu,” anasema Matayo.
Shule za msingi nchini kote zilifungwa machi 17, 2020 na kufunguliwa Juni 29, 2020 ambapo wanafunzi waliendelea kunawa mikono yao wakijikinga na ugonjwa huo kwa siku mara 16.

Lakini mwezi mmoja tu baadaye hali hiyo ilianza kupotea siku hadi siku kwa kuamini kuwa ugonjwa wa Covid 19 haupo tena.

Sababu nyingi zimetajwa kuwa ni chimbuko la mabadiliko hayo, ikiwamo uhaba wa maji.

Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi anayeshughulikia Afya ya Lishe pamoja na Mazingira katika Shule za Msingi na Sekondari, Florence Kibani, anasema ya kuwa katika Manispaa ya Bukoba pamoja na kwamba zipo shule zenye matanki ya kuvunia maji ya mvua yenye ujazo tofauti na ambazo zina maji ya BUWASA, zipo pia ambazo hazina miundombinu kabisa ya kupata maji mpaka wanafunzi waende kuchota maji mtoni.

Aidha, shule nyingi sasa zinakabiliwa na tatizo la bili kubwa za maji kwa zile zenye maji ya BUWASA kutokana na maji kutumika kwa kiwango kikubwa wakati wa kilele cha maradhi ya Covid-19 japo nyingine ziko mbali na vyanzo vya maji.

“Sasa hapo kuna mambo ambayo tunaweza kuona kuwa inakuwa vigumu kusema kuwa watoto watachota maji mtoni ili kuendelea na utaratibu wa kunawa mikono mara 16 kwa siku na wakati huo huo masomo yanatakiwa kukamilika kwa siku kwa mujibu wa ratiba,” anasema Kibani.

Katika Manispaa ya Bukoba ni shule chache sana ambazo zinaendelea na utaratibu wa kunawa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 na hizo nazo zinafanya hivyo si kwa kiwango cha wakati kama ulipotangazwa ugonjwa huo kuingia nchini.

“Kwa sasa kilichobakia ni kunawa mikono wakati wa kutoka chooni kama ilivyo desturi ya wanafunzi,” anasema Afisa Elimu huyo.
Uchunguzi umeonyesha ya kuwa kuna shule ambazo bado wanajitahidi kunawa mikono lakini nazo siyo kama wakati ule ugonjwa wa Covid- 19 ulipokuwa kwenye kasi.

Shule hizo ni pamoja na Shule ya Msingi Nshambya, Bilele kutokana na kuwa na maji ya uhakika.
Shule zinazotajwa kuwa na watoto wanaotoka katika mazingira magumu ni pamoja na Kyakairabwa ambayo inafikia wakati walimu wao wanalazimika kuwaosha wanafunzi kulingana na hali ya maeneo husika.

“Sasa najaribu kufikiria hawa watoto wasiokuwa na uwezekano wa kuoga wenyewe wakati wa Covid- 19 walikuwa katika hali gani au ndiyo walikuwa wakimtegemea Mungu pekee,” anasema Florence Kibani.

Kwa upande wake Mganga wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Mustafa Waziri alisema kwa ujumla, watu wengi, wakubwa kwa wadogo, hawana utaratibu wa kunawa mikono.

Anasema waliweka utaratibu wa kila mwezi kuwa na zoezi la kunawa mikono lakini pamoja na hayo bado katika shule za msingi maji yapo na sabuni lakini wanafunzi wamekuwa wakipuuza kabisa kunawa mikono wakiamini kuwa hakuna tena ugonjwa wa Covid-19.

“Mimi sipendi kusema uongo Covid-19 imekwisha sawa lakini kuna usafi binafsi ambao wazazi wenyewe wanatakiwa kuwaelekeza watoto si mpaka kuwe na ugonjwa. Watu wabadilike jamani.

“Mfano, kuna maeneo muhimu sana kama katika vituo vya afya, inawekwa sabuni na maji lakini unamshangaa mzazi anamleta mtoto wake anampitisha hata bila kunawa mikono.

“Sasa hapo tunatarajia kuwa kuna usafi? Mwisho wa siku yakitokea magonjwa inakuwa vigumu sana kuwanusuru,” alisema Dk. Waziri na kuongeza:
Aidha anaongeza kuwa; “Hapa mjini kuna Shule za Msingi kama Bilele, Mafumbo na Kashai, hivi karibuni nimekwenda kukagua hali ya mazingira, lakini nimekuta hakuna hata ndoo moja ya maji ya kunawa mikono,” anasema Dk. Waziri.

Hata katika vituo vya afya watu hawataki kunawa mikono. Hawana hofu tena mpaka watangaziwe na Serikali.

“Kunawa mikono kwa watoto wakiwa shuleni inawasaidia kuona kuwa hata kama si Covid- 19, yapo magonjwa mengine ya kuambukiza yatokanayo na uchafu wa mikono kama kuhara na kipindupindu. Kwa hiyo kunawa mikono ni lazima ili kuendelea kujikinga na magonjwa hayo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles