28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Uwezo mkubwa wa Maabara Kanda ya Ziwa unavyofanikisha ulinzi wa afya ya jamii

Na Aveline Kitomary

Kwa sehemu yoyote duniani Maabara ni muhimu katika kufanya tafiti mbalimbali pamoja na vipimo vya aina tofautitofauti.

Umuhimu wa maabara huonekana dhahiri kutokana na kuwa katika kila tafiti au vipimo lazima afya ya viumbe hai na mazingira vihusike.

Maabara hukamilika hasa pale inapokuwa na vitu vya msingi vinavyohitaji ili kufanikisha uchunguzi.

Hapa nchini kuna maabara nyingi ambazo hufanya kazi mbalimbali katika kufanikisha usalama,ufanisi na ubora wa bidhaa zinazotumika, moja wapo ya maabara kubwa iliyopo nchini inapatikana Ukanda wa Kanda ya Ziwa ambayo ni maabara ya Mamlaka ya Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi (TMDA).

Hii imekuwa maabara yenye msaada mkubwa kwa ukanda huo kutokana na kuwa na uwezo mkubwa katika upimaji.

Tafiti mbalimbali za dawa, vipukusi, vifaa tiba,microbilojia hufanyika katika maabara hiyo.

Mafanikio ya tafiti hizo ni kutokana na maabara hiyo kuwa na vifaa vingi vya kisasa na vyenye uwezo mkubwa katika chunguzi zinazofanyika.

Maabara ya (TMDA) Kanda ya Ziwa ilianzishwa Mwaka 2018, lengo likiwa ni kutoa huduma katika maeneo makuu mawili, upande wa Maicrobiolojia na ule wa Kemia.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Maabara hiyo, Bugusu Nywamweru, maabara hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa dawa katika kipindi chote hadi sasa ambapo wameweza kupima jumla ya sampuli 860.

UPIMAJI SANITIZER

Moja wapo ya mashine ya kisasa iliyoko katika maabara hiyo ni ile ya kupima kiwango cha kilevi (alcohol) katika vitakasa mikono (Sanitizer).

Kaimu mkuu wa maabara Bugusu Nyamweru (kulia) na mchunguzi wa maabara Kapiliya Haruni (kushoto) wakionesha jinsi mashine ya HPLC inavyofanya kazi.

Nyamweru anasema upimaji wa kiwango cha pombe ni muhimu kutokana na uwezo wa kuwepo madhara endapo kiwango kinachotakiwa hakijazingatiwa.

Hapa naeleza; “Utumiaji wa vitakasa mikono visivyo na ubora unaweza kuwa na madhara makubwa ikiwemo kuwaka moto, kuharibu ngozi na kuwashwa, ni muhimu kiwango cha kilevi (alcohol) kiwe ni kile kinachohitajika ambacho hakitakiwa kupungua wala kuongezeka.

“Kama utatumia sanitaizer inakiwango kidogo cha alcohol wadudu wanatakiwa kufa hawatapata madhara hiyo ni hasara kwa sababu lengo halijafikiwa.

“Endapo kiwango cha alcohol kimezi pia madhara ni makubwa zaidi kuna uwezekano wa mtumiaji kuwaka moto,kuwashwa au kupata madhara katika ngozi hivyo watengenezaji wanatakiwa kuwa makini,” anafafanua Nyamweru.

Nyamweru anasema mashine ya kisasa ambayo inauwezo mkubwa wa kupima vipukusi inaitwa ‘Sanitezer machine’.

“Mashine hii inahusika katika uchunguzi wa vitakasa mikono na hii ni moja wapo ya vipukusi ambayo ipo katika kundi ya kuua vimelea vya bakteria au vimelea vinavyosababishwa na virusi. mashine hii inatumika kuangali ubora wa alcohol iliyoko ndani ya vitakasa mikono ni mashine ndogo lakini inafanya kazi kwa kutumia mvuke kuondoa kiwango cha pombe na pia kinakusanywa katika kifaa,”anaeleza.

Anasema baada ya mvuke kutolewa kiwango cha kilevi(alcohol) hupimwa kwa kutumia kifaa kinachoitwa ‘hyrometer’.

“Kifaa kingine kinaitwa ‘steam distiller’ hii inachuja formula iliyoko ndani ya vitakasa mikono hadi sasa tumeweza kupima sampuli zaidi ya 90 ya vitakasa mikono na ufanisi wake ni mzuri.

“Standard zinazotumika katika upimaji tunaangalia kama ni asilimia 70 tunaangalia isifike mfano vitakasa mkono haitakiwa kuwa chini asilimia 60 kwa hiyo tutatengeneza kiwango kinachofahamika kisha tutapima kwa utaratibu huohuo na tutalinganisha na sampuli yetu ambayo pia tutaipima kwahiyo majibu yatakayopatikana hapo tutajiridhisha kwamba kweli sampuli yetu inakiwango inachotakiwa kwa kulinganisha kwa kiwango cha kimataifa,”anafafanua Nyamweru.

Anasema kuwa Mashine hiyo inauwezo wa kufanya kazi kwa muda wa dakika nne hadi sita.

UWEZO WA DAWA KUTIBU

Mashine nyingine ni ile yenye uwezo mkubwa katika uchunguzi wa uwezo wa dawa kutibu ugonjwa husika.

Mchunguzi wa dawa, Kapilia Lameck, anasema mashine hiyo inayoitwa, High Performance Liquid Chromatragraphy (HPLC) inauwezo wa kugundua kama kiambata hai kilichopo kwenye dawa ni sahihi na kinauwezo wa kutibu ikiwemo dawa asili.

Hapa anafafanua zaidi; “Mashine hii inaanza na kupima uzito ili kuangalia kama dawa tunayopima ni ile inayokidhi vigezo vilivyowekwa. Katika dawa kuna layer zingine kama vibebeo kuna wakati mwingine tunaangalia ulinganifu wa uzito kutoka kidonge kimoja na kingine
na wakati wa kusajili vitu vingi vinaangaliwa ikiwemo uzito, mwonekano na mengine.

“Tunaweka dawa kwa ajili ya kuisaga baada ya hapo tunaweka kwenye mashine kwa ajili ya kuchangaya kwa dakika 20, lazima tuangalie kama kuna kiambata hai katika dawa husika,”anaeleza.

Lameck anasema mashine hiyo ya HPLC inauwezo wa kusoma dawa husika kwa kulinganisha na kiwango kilichowekwa kimataifa kwani wapo waliosajiliwa kitaifa kutengeneza dawa za mbalimbali na zimehakikiwa.

“Hivyo, tunakuwa na dawa ya kulinganisha nayo kama kulinganisha kwa dawa zingine na HPLC inapima dawa ili kuweza kusoma dawa husika kwa kuangalia viwango vya dawa inayotakiwa kimataifa baada ya maandalizi na upimaji kusoma.

“Katika soko la dawa kuna mambo mengi kama kutibu mtu na biashara, mtu mwingine anaweza kufanya udanganyifu ili kupunguza gharama hivyo sisi hapa tunahakiki hii inaonesha kama kuna kiambata hai kwenye dawa au hamna,”anabainisha.

Anasema katika upimaji wanatumia kemikali ambazo zimeelekezwa katika miongozo hivyo mashine inapokuwa inafanya kazi na kemikali zinakuwa zinapita katika mifumo ya mashine.

“Kwenye hii mashine kuna sehemu inabeba pampu ambayo inapanda na kushuka una’set’ unasubr inafanya kazi yenyewe hadi ulipo’set’ itaishia mahali kila kitu kimetenganishwa mpaka tupate kile tunachotaji.

“Mashine hii Inauwezo wa kupima dawa zaidi ya mmoja zinasomeka katika wavelate ina ‘plate’ mbili na kwenye ‘computer’ lazima uoneshe unameweka kwenye plate ipi hii inasaidia wakati wa kusoma na inafanya kazi kama roboti lazima useti,”anaeleza.

Anafafanua kuwa mashine hiyo inaweza kufanya kazi muda mrefu kwa kutumia umeme; “Unaweka jenereta automatic unaweza kuweka hata aina 20 za dawa,” anasema.

UCHUNGUZI KEMIKALI

Liquid Chromatograph Mass Spectroscopy (LSMS/MS) hii ni mashine iliyoko katika maabara hiyo ambayo inauwezo wa kuchunguza kemikali katika mwili wa binadamu.

Kaimu Mkuu wa Maabara, Nyamweru anasema mashine hiyo pia inauwezo wa kupima vipande vidogo vya kemikali vilivyopo katika mazingira, chakula na maji.

“Tunafanya chunguzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kitafiti, za kawaida, chunguzi za kung’amua au kutambua kiwango cha kemikali na dawa ndani ya mwili wa binadamu.

“Faida ya mashine hii ni kuwa unapofanya uchunguzi inauwezo wa kugundua vitu vidogo sana vilivyo katika mwili wa binadamu au katika sampuli inaweza kutambua hata kiasi cha kemikali.

“Uchunguzi unafanyika mara mbili hadi ile kemikali imeweza kuchanganuliwa katika vipande ambapo mwisho tutaweza kung’amua kwamba kipande hiki kinatokana na maumbile au kipande hiki kinatoka bacteria wa aina fulani,”anaeleza Nyamweru.

Anasema kuwa mashine hiyo pia inaweza kutumika katika kupima uchafuzi katika dawa na uwepo wa viambata hai sahihi.

“Kama kuna kiambata kingine ambacho sio hai au kiambata hai kilichoharibika katika mwili wa binadamu au tiba na katika masuala ya tafiti inaweza kutambua umbo la kemikali ya dawa au mchanganyiko unaotakiwa kufanyiwa kazi kwa tiba au shughuli yoyote.

“Katika kuangali dawa inavyofanya kazi mwilini tunafanya baada ya dawa kufika na mabaki yakatokea yana umbo gani na yametengenezwa kwa kemikali ipi tukitaka kujua kwamba dawa iliyotumika katika mwili wa binadamu katika eneo Fulani iko kwa kiasi gani.

“Tunataka kujua dawa iliyoko katika mkojo au mate au katika tishu ya mwili labda kwenye moyo,ini iko kwa kiasi gani,”anafafanua.

UWEPO WA KIAMBATA HAI

Maabara hiyo ya kisasa pia inamashine ambayo iko mithili ya tumbo la binadamu.

Mashine hiyo inayoitwa ‘desolution tester machine’ inaweza kuchunguza uwezo wa dawa kutibu katika mwili wa mwanabadamu na uwepo wa kiambata hai katika dawa.

Kaimu Menja wa TMDA kanda ya ziwa Sophia Mziray akieleza namna maabara hiyo inavyofanya kazi

Mchunguzi wa dawa, Kapilya Haruni anafafanua hapa: “Mashine hii kazi yake ni kuangalia namna gani dawa inaweza kuachia kiambata hai ambacho kipo ndani yake kwa kiwango kinachotakiwa ili iweze kuingia katika mwili wa binadamu na kufanya kazi kwa kiwango kilichokusudiwa.

“Mashine hii pia inaweza kutumika katika maeneo mbalimbali ya utengenezaji wa dawa kwa maana kwamba dawa inapotengenezwa inakuwa na viambata vingine ambavyo sio hai, hivyo mtengenezaji ili kujiridisha kwamba dawa aliyotengenezwa kiambata hai iliyopo itatoka kwa kiwango kinachotakiwa atatumia mashine hii,”anafafanua Haruni.

Anaeleza kuwa wanapotaka kupima kiambata hai wanalinganisha na mwongozo wa kimataifa wa dawa husika hivyo mashine hiyo inauwezo mkubwa kutambua dawa.

“Mtengenezaji wa dawa ni vizuri akafanya ulinganishwaji na mwongozo wa dawa husika ambao umeandaliwa (reference madicine) au dawa ya kufanyia mlinganisho. Kiwango cha kiambata hai inaweza kupimwa na mashine hii ambayo itaachanisha kiambata hai na kile ambacho sio hai na katika hatua hiyo tunaweza kutumia mashine zingine maalum kupima kiwango,” anasema.

Anasema upimaji kutumia mashine hiyo ni rahisi kutokana na kuwa na mfumo wa moja kwa moja (automatic) na kutoa kiwango kinachotakiwa kwa muda maalum.

“Kiambata hai ni ile kemikali ambayo inatambulika kisayansi kuwa inaleta tiba katika mwili wa binadamu kutokana na tafiti hizi kemikali zinaweza kuleta madhara hasi au chanya na endapo kiwango kitazidi inaleta madhara.

“Mashine hii inafanya kazi mithili ya tumbo la mwanadamu unaweka kwa muda ulio’set’ kama dakika 15 ili dawa iweze kuyeyuka hivyo ina’test’ myeyuko wa dawa na isipokuwa imeyeyuka haiwezi kufanya kazi iliyokusudiwa.

“Kwani dawa inapotumiwa na kuyenyuka inavunjika katika vipande ndipo inaweza kuingia kwenye seli kufanya kazi yake kama itabaki ilivyo haitafanya kazi iliyokusudiwa.

“Ndani ya hii mashine kuna vifaa tunaweka vimiminika ambavyo ni sawa na vile vilivyoko tumboni kwahiyo kama mwongozo utasema dawa hii inayeyuka kwenye asidi iliyoko tumboni ( hydcloric acid) flani basi kiwango hicho na sisi tunatengeneza na kuweka katika vibebeo vilivyopo katika hivi vifaa,” anasema.

Aidha, anabainisha kuwa kitu kingine wanachoangalia ni kiwango cha joto cha mwili wa mwanadamu ambacho kinatakiwa kufanana na mashine hiyo kuanzia nyuzi 36 hadi 37 ili kuweka mazingira sawa na tumbo.

“Baada ya hapo tunachukua vimimika maalum vilivyotolewa mashine hii inafanya myeyuso halafu tunaenda kwenye mashine nyingine
tunaweka muda kama itayeyuka kabla ya muda unaotakiwa kulingana na mwongozo inawezekana haijatengnezwa vizuri na ikichukua muda mrefu pia kutakuwa na tatizo katika utengenezaji.

“Baada ya hapo tunaenda kwenye mashine ambayo inaonesha kiambata kilichopo katika dawa hii ni kiasi gani na pia tutaweka kwenye mashine nyingine ambayo itasoma katika intesty ya dawa husika,”anafafanua Haruni.

KIWANGO CHA MADINI

Mashine nyigine inayopatikana ni Micro Plasma Atomic Emission Spectrophotometer (MPAES) ambayo inauwezo wa kupima madini mbalimbali yakiwemo tembo, copper, zink, mecyur na zingine.

Mtaalamu wa Maabara, Jovinary Rwezahura, anasema mashine ya MPAES inauwezo mkubwa wakupima madini zaidi ya moja kwa mara moja.

“Hii mashine kama zilivyo mashine zingine zinatumika kupima madini (heavy metal) tunasema madini tembo na zingine kama kupima sodium,copper, zink, meckyur na mashine hiyo inauwezo mkubwa hasa katika kupima madini mengi kwa wakati mmoja lakini mashine zingine haziwezi kufanya kazi zote hizo kwa wakati moja,”anaeleza Rwazehura.

Mtaalamu wa maabara Jovinary Rwezahura akipima kiwango cha alcohol katika kitakasa mikono.

Anasema upekee mwingine wa mashine .ya MPAES ni matumizi ya gesi ya Nitrogen ambayo inajikusanya kutoka katika mazingira.

“Faida nyingine hatutumii gesi zingine kama petroleum gesi ambazo hauruhusiwi kuacha mpaka uhakikishe imezimwa kama gesi zinazotumika majumbani lakini hii kwa sababu ya Nitrogen naweza kuwasha na kuweka sampuli na nikaendelea kufanya kazi zingine, baadae naweza kuizima.

“Mashine hii inatumika kupima madini kwenye vifaa tiba, maji, vipodozi, vyakula, sukari, mchicha pia tunapima madini hata kwenye maji pia tunaangali madini ambayo hayaruhusiwi kuwepo kama madini tembo kwa kiasi inayohitajika lakini hayaruhusiwi kuwepo na kama yapo kuna kiasi kinaangaliwa.

“Madini tembo hayahitajiki yanaweza kuharibu figo, mifupa inaweza isiwe imara, madini ya mekyuri yanaweza kuathiri mifumo ya neva ukawa unasahau kwahiyo madini tembo hayahitaji kabisa lakini tunaangali kama kuna kiwango kidogo ambacho kinaweza kuvumilka,”anabainisha Rwezahura.

Aidha, anafafanua kuwa, huwa wanapima pia vipodozi kwani vikiwa na madini tembo ngozi itaharibika na pia mashine hiyo inatumika kupima vifaa tiba kama sindano.

“Katika upimaji hatuweki sindano moja kwa moja kuna taratibu za kufanya kwa mfano madini yaliyoko kwenye sindano, tunachukua sindano tunaweka kwenye maji kwa muda fulani kama madini tembo yapo yanatakuwa yanatoka yanaingia kwenye maji.

“Kisha yale maji tunayachukua na kuja kupima kwenye mashine hivyo kama yapo tutayaona kama hayapo pia tutajua,”anasema Rwezahura.

Anaongeza; “Kama mtu akileta tukapima kama tunazuia tunamueleza kuwa tumezui kutokana na sababu zilizopo na huwa tunaangali viwango vya kimataifa na tunaangali kama kiwango kimepungu au kimezidi na kama kinavumilika,” anahitimisha Rwezahura.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Maabara hiyo Nyamweri anatoa wito kwa watafiti mbalimbali kutumia mashine hiyo ili kufanikisha tafiti zao.

Jengo la TMDA Kanda ya Ziwa

“Kwasasa vifaa vipo na kama kuna taasisi inahitaji kufanya tafiti katika eneo hilo uwezekano huo upo na wanakaribishwa kufanya tafiti lengo letu ni kupanua wigo wa upimaji sampuli kwa wadau mbalimbali katika eneo la kanda ya ziwa.

“Hasa kuangazia vitu vinayoathiri afya za watu hivyo tunakaribisha taasisi za tafiti kuleta sampuli zao katika maabara hii tuweze kupima na tunawakaribisha wadau, taasisi za afya kama NIMR, zingine binafsi wajue kuwa TMDA ina hivi vifaa,”anasema Nyamweri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles