28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ujenzi wa kiwanda cha alizeti kwainua uchumi wa wananchi Hanan’g

Na Janeth Mushi, Hanan’g

Kuwezeshwa kwa kujengewa kiwanda cha kuchakata alizeti kwa jukwaa la wakulima wadogo na wasimamizi wa masoko ya alizeti Hanan’g (JUWAMA), kunatajwa kuongeza mnyororo wa thamani na kuinua wananchi kiuchumi.

Mbali na kujengewa kiwanda hicho na Shirika lisilo la Kiserikali la Oxfam Hongkong wakishirikiana na Shirika lislo la kiserikali la Ujamaa Community Resource Team(UCRT),kupitia mradi wa kuwainua kiuchumi wanawake na vijana wilayani hapa,jukwaa hilo limepwa zana mbalimbali kwa ajili ya zao hilo.

Zana hizo zilizoanza kutumika katika msimu wa mwaka 2019/2020, zimewezesha jukwaa hilo ambalo ni muunganiko wa vikundi sita vyenye jumla ya wanachama 174, ambazo ni pamoja na zana bora za kupura za kukamua mafuta ya alizeti ili kuongeza mnyororo wa thamani,badala ya kuuza alizeti ghafi wauze mafuta ya alizeti na mashudu.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi mara baada ya kutembelea vikundi hivyo,Katibu wa jukwaa hilo, Andrew Jacob,amesema awali kabla ya kupata zana hizo kupitia wadau hao wa maendeleo waliwezeshwa kupata mbegu na kulimiwa hekari 42 za alizeti ambazo zilipotakiwa kuvunwa walikumbana na changamoto ya uvunaji ambapo walilazimika kuweka kambi kwa siku 21 shambani.
 
“Tunashukuru kwa mradi huu kwani awali hali yetu kiuchumi haikuwa nzuri ila pia mashine hizo a kuvunia zitatusaidia kwani mwimu uliopita tulilazimika kuweka kambi kwa siku 21 ili tuvune,changamoto zilikuwa nyingi hasa kwa wanawake wenye ndoa,hii itatupunguzia muda mwingi wa kukaa shambani kwa ajili ya mavuno,”amesema.
 
Amesema kati ya wanakikundi hao 158 ni wanawake na wanaume 16 ambapo kwa sasa baada ya kujengewa kiwanda hicho wameweza kuongeza mnyororo mzima wa thamani ya zao hilo kwani awali walikuwa wakilima na kuuza alizeti ila kwa sasa wanalima,kumamua mafuta ya alizeti ambapo pia wanaumza mashudu.

“Kuanzia Julai mwaka jana hadi sasa tumeweza kukamua magunia 449 ya watu binafsi nje ya vikundi na kati ya hayo ni 398 na tumepata  zaidi ya Sh milioni 2.3,mengine 46 wameacha mashudu, kwani kama huna hela ya kulipia unaacha mashudu ambayo kwetu sisi ni faida zaidi kwani gunia moja tunauza Sh 30,000,”ameongeza.

Katibu huyo amesema katika kipindi hicho wamekamua magunia yao kama jukwaa 108,na kupata mafuta lita 1710 na baada ya kuza wamepata zaidi ya Sh.Milioni 6.47 na kuwa kupata mashudu gunia 108 ambapo kati ya hayo yamebaki magunia 54 ambayo wakiuza wanatarajia kupata Sh milioni 1.6.

“Jitihada za wadau zimesaidia kufikia hapo,tunatoka vijijini sana na tulikuwa tunadharaulika sana ila kwa sasa tumepiga hatua.Ukiangalia trekta walilotupa tumeweza kulima heka 91.5, kila heka tumepata Sh. 40,000 na kupata zaidi ya Sh milioni 3.6,”anafafanua.

“Ni mafanikio ambayo tumeweza kuyafikia,kiukweli Oxfam na ucrt wameunga jitihada za serikali mkono juu ya kuhamasisha viwanda,sikuwahi kutegemea kama siku moja ningeweza kuwa sehemu kama hii na kuwa nasimamia jengo kama hili(kiwanda),” Jacob.

Ametaja fadia nyingine ni pamoja na kupatiwa mafunzo ikiwemo ya matumizi ya mbegu za kisasa zinazowasaidia kuzalisha kwa wingi ambapo kwa gunia moja wanaweza kupata hadi lita 33 ukilinganisha na wakulima wanaotumia mbegu za kawaida wanaweza kupata hadi lita 17 kwa gunia moja.

Mmoja wa wajumbe wa jukwaa hilo kutoka kikundi cha Umoja, kilichopo kijiji cha Gasaboi, Magdalena Mathias, anasema kupitia jukwaa hilo ameweza kupata mtaji wa kuanzisha biashara ya mamalishe,duka pamoja na kilimo cha mazao mengine.

Anasema awali kabla ya elimu kutolewa katika maeneo hayo ya vijijini wanawake walikuwa hawaruhusiwi kufanya biashara na badala yake walikuwa wakitegema waume zao.

“Kikundi tulipewa elimu na UCRT na binafsi  kimenisaidia mimi binafsi niliwahi kukopa hela na kuongezea ujenzi wa nyumba yangu nikamalizia nyumba ya kisasa,nilikopa Sh 500,000,kabla nilichukua 100,000 na kuanza biashara ya mgahawa.

“Bila UCRT na wadau wengine wa maendeleo maisha yangebaki kuwa ya shida kama zamani nisingeweza kupeleka watoto shule,wametusaidia kwani tumeondokana na maisha duni sasa hivi hatuogopi tunaogopa kusomesha watoto hata mwanaume akikataa naweza kusomesha watoto mwenyewe,”amesema na kuongeza.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo,Dorris Ng’homange,amesema mchango wa wadau katika wilaya hiyo umesaidia wananchi kukua kiuchumi na kupungua kwa mfumo dume.

Amesema kupitia wadau hao wamefaidika na mradi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi,uliowezesha wanawake  kumiliki ardhi kwa hati jambo ambalo kwenye wilaya hiyo halijawahi kutokea.

“Kuna mafanikio makubwa wadau hao wamekuwa wakiwawezesha wahusika kwa mitaji kidogo na elimu zaidi kwa sababu mtu kichwa kikipona mambo mengine yote yatawezekana,wanawake na vijana wameweza kujitambua na kufanya baishara zinazowaongezea kipato,” amesema.

Aidha, Afisa huyo ameomba wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali ili kusaidia jamii ikue kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Awali Msajili wa Asasi zisizo za kiraia (NGO’s) na Mratibu wa viwanda wilayani Hanan’g,Gaudance William,amesema JUWAMA ni miongoni mwa viwanda vikubwa wilayani humi ambacho kinaweza kuchakata zaidi ya tani tatu kwa siku hivyo kusaidia kukuza uchumi wa eneo hilo.

“Kiwanda kina ufanisi mkubwa hivyo nitoe wito kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika halamashauri yetu waje fursa ni nyingi na mazao mengi yanazalishwa hapa kwami tumekuwa tukipata changamoto ya uongezaji thamani mazao,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles