28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| TACAIDS inavyotumia walimu kudhibiti UKIMWI nchini

*Nikupitia mradi wa ‘Timiza Malengo’  

*Wafikia Shule 1,961 na walimu 3,923 katika Halmashauri 18

Na Nadhifa Omar, TACAIDS

Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI wa mwaka 2016/2017, kundi la vijana wa miaka 15 hadi 24 ndio lililoathiriwa zaidi na maambukizi mapya ya VVU.

Kwa sasa, Tanzania ina jumla ya watu 1,700,000 wanaoishi VVU na tayari wanatumia dawa za kufubaza Virusi (ARVs).

Takwimu zinaonesha kuwa maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka ni watu 68,000, anaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuthibiti UKIMWI nchini (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko.

“Pamoja na kuonekana kupungua kwa maambukizi, bado kundi la vijana lipo kwenye hatari zaidi, hasa wasichana. Takribani asilimia 30 hadi asilimia 40 ya vijana wanaopata maambukizi mapya ya VVU, asilimia 80 ni vijana wa kike,” anasema Maboko.

Walimu kutoka Shule mbalimbali za Mkoa wa Dodoma wakiwa kwenye  mkutano wa  Elimu ya VVU na UKIMWI, Afya ya Uzazi na Stadi za Maisha.

Ili kulinusuru kundi hilo la vijana ambao ndio tegemeo katika jamii na nguvu kazi ya Taifa, pamoja na shughuli mbali mbali zinazoendeshwa na TACAIDS imekuja na mpango wa kutoa elimu ya VVU na UKIMWI, Afya ya Uzazi na Stadi za Maisha kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari, kwa kuzingatia Watoto na Vijana Balehe wanatumia muda mwingi wakiwa na Walim Shuleni.

Kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu, UKIMWI na  na Malaria (GFATM), TACAIDS inaratibu Mradi wa ‘Timiza Malengo’  ambapo Shule 1,961 na walimu 3,923 katika Halmashauri 18 za Mikoa ya Tanga, Morogoro, Dodoma, Singida na Dodoma wamefikiwa.

Elimu hiyo inahusisha pia VVU na UKIMWI, Afya ya uzazi, Stadi za Maisha na UVIKO -19, ili kuwaongezea ujuzi Walimu katika maeneno ya shule na kuwawezesha kusambaza maarifa ndani na nje ya taasisi.

“Na tafiti zinasema maambukizi ni makubwa kwa vijana wa kike kutokana kuanza ngono katika umri mdogo wa miaka 10 bila kinga,” anasema Maboko na kusistiza kwamba:

Kundi la walimu ni muhimu kwani lina uwezo wa kufikisha elimu hiyo kwa haraka na kwa wakati mmoja nchi nzima, jambo ambalo Tume haina uwezo wa kulitekeleza bila kushirikiana na Wadau wakiwemo Walim.

Aidha, Walimu ni sehemu ya wazazi ambao muda mwingi wana ukaribu na wanafunzi, hali inayorahisha mawasiliano wakati wa utoaji wa elimu ya VVU na UKIMWI, Afya ya uzazi, Stadi za Maisha.

Walimu watasaidia pia katika suala la uundaji wa ‘club’ za  kudhibiti UKIMWI /Afya kwa wanafunzi ambazo mojawapo ya agenda itakua ni kuzuia na kuthibiti maambukizi mapya ya VVU.

Wakati huohuo, wanafunzi nao watasaidia kufikisha elimu hiyo kwa wanajamii wengine ili mwitikio wa UKIMWI uzidi kuwa endelevu na mtambuka.

TACAIDS inalenga pia kuwashirikisha Maafisa na  Wadhibiti Ubora/Wakaguzi wa Elimu ili wasaidie kutilia mkazo na kusimamia utoaji wa elimu ya VVU kwa wanafunzi.

Hatua hiyo itasaidia pia kuzuia mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, matumizi ya dawa za kulevya, tumbaku na pombe ili watoto waweze kumaliza salama elimu zao na kutimiza malengo yao ya maisha watakayokuwa wamejiwekea.

Kwa mujibu wa Dk. Maboko, vijana ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa masomo, watapata elimu ya kujikinga na VVU, elimu ya biashara, kuandaa andiko la biashara kulingana na matakwa ya kila mlengwa. Kisha Wasichana Balehe na Wanawake Vijana hao watapatiwa mtaji ili kuanzisha shughuli zitakazowawezesha kiuchumi.  Kuwawezesha wasichana balehe na wanawake vijana kiuchumi ni hatua nyingine inayotekelezwa na TACAIDS ili kundi hilo libaki salama kiafya.

Walengwa wote walio ndani na nje ya Shule wanapatikana kutoka kwenye kanzi data ya TASAF kwenye mradi wa kunusuru Kaya Maskini. Hii imerahis

 “Aidha, tunatafuta namna bora ya kuwafikia wengi zaidi walio nje ya mfumo wa mfumo rasmi wa elimu, kwani kupitia TASAF tutawapata wale tu wanaohudumiwa na mfuko huo,” anasemaa Dk. Maboko.

Tafiti imeonesha pia kwamba kundi hilo ni miongoni mwa makundi ya vijana walio katika mazingira hatarishi ya maambukizi ya VVU, kwani baadhi wamekua wakijiingiza kwenye ngono isiyo salama ili kukidhi mahitaji yao na familia.

Sambamba na hilo, Tume imekua pia ikihamasisha jamii kwa ujumla kupima afya ili watakaobainika kuwa na maambukizi ya VVU waanze kupata huduma kwa wakati, hasa matumizi ya ARVs.

Hatua ya upimaji afya itawasaidia vijana ambao hawajafikiwa na mradi wa ‘Timiza Malengo’ na hatimaye kufanikisha lengo la kidunia la kuwa na maambukizi sifuri, ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, licha ya maambukizi kwa vijana kutopungua, TACAIDS inajivunia mafaniko kadhaa ambayo tayari imeyafikia, ikiwemo kupungua kwa vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa asilima 50,  kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2021.

Kupungua kwa vifo ni Mwitikio bora wa wadau wakiwemo Wizara ya Afya ambao hupima afya za walengwa mara wanaogundulika na maambukizi ya VVU huanza  kutumia ARVs kwa kufuata ipasavyo ushauri wa wataalam wa afya.

Aidha, kwa watu wazima kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kimepungua kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka jana (2021).

Kwa mujibu wa TACAIDS, hali kadhalika maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia saba mwaka 2021.

“Aliendelea kueleza kuwa matumizi ARVs kwa wenye maambukizi ya VVU yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi asilimia 98 mwaka jana,”anasema Dkt Maboko.

Kwa mujibu wa Tume, Serikali inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia shabaha za Kimataifa za tiba, ambapo Tanzania ipo kwenye hatua nzuri za kufikia malengo ya Kidunia ya ‘Tisini na Tano Tatu (95-95-95)’ ifikapo mwaka 2025.

 Alifafanua maana ya ‘Asilimia 95 ya Watu Wanaoishi na VVU (WAVIU) wawe wamepimwa  na kujua hali yao ya maambukizo ya VVU; Asilimia 95 ya wale wanaojua hali zao  wawe wameshaanza kutumia dawa za kufubaza VVU (ARV); na Asilimia 95 ya wale wanaotumia ARV wawe wamefubaza VVU katika miili yao’

Hadi sasa watu wenye maambukizi ya VVU (WAVIU) wanaofahamu hali zao za mambukizi ni asilimia 83, waliopo kwenye matibabu ni asilimia 98 na  walifubaza VVU ni asilimia 92.

Kwa upande wa unyanyapaa na ubaguzi kwa mujibu wa Takwimu za kitaifa, kiwango kimepungua kutoka 28 mwaka 2013 hadi asilimia 5.5 mwaka 2021.

Kwa maendeleo endelevu ya kudhibiti VVU, Tume imefanya mapitio ya Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibti UKIMWI (NMSF IV 2018/19 – 2022/23) na kuanza maandalizi ya Mkakati wa Tano (2022/23 – 2025/26).

Tume pia imefanikiwa kukamilisha miongozo mingine muhimu ikijumuisha; Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji kwenye UKIMWI wa mwaka 2020; Mwongozo wa Kitaifa wa Sekta zote wa utekelezaji wa afua za kudhibiti unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na VVU na UKIMWI (Faharisi ya UKIMWI); Mwongozo wa kuwawezesha watendaji muhimu kufanya afua za UKIMWI kwenye Bandari, Maziwa na jamii inayozunguka maeneo hayo wa mwaka 2020; na Mwongozo wa utoaji wa huduma za kudhibiti VVU na UKIMWI katika maeneo hatarishi na mpakani pamoja, Mkakati wa mawasiliano, Mkakati wa Taifa wa Kondom na  Mkakati wa Uratibu wa Asasi za Kiraia.

Tume imeweza pia kutoa elimu ya Sheria, ya VVU na UKIMWI na Haki za binadamu iliyowahusisha wadau mbalimbali. Elimu hiyo inajumuisha kujua haki na wajibu kwa watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na masuala ya Unyanyapaa na Ubaguzi pamoja na Ukatili wa Kijinsia.

Miongoni mwa makundi ya wadau waliofikiwa na elimu hiyo ni pamoja na WAVIU, Vijana, Polisi- Dawati la Jinsia, Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Waratibu wa Mikoa na Halmshauri, Jeshi la Magereza, MaafisaUstawi wa Jamii, na Waajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles