24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: RMO Shinyanga aeleza walivyopiga hatua kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua

Na Damian Masyenene, Shinyanga

Imeelezwa kuwa uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma, ushirikishwaji wa jamii, elimu na utambuzi wa akina mama wajawazito na viashiria hatari kisha kuchukua hatua za udhibiti imechangia kwa kiasi kikubwa kuusaidia mkoa wa Shinyanga kupiga hatua katika kupunguza vifo vya akina mama wanaofika kujifungua na vile vya watoto wachanga.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mganga Mkuu (RMO) wa Mkoa huo, Dk. Nuru Mpuya, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji katika sekta ya afya kwenye kikao cha ushauri cha mkoa huo Februari 10, mwaka huu, ambapo alieleza kuwa vifo vya akina mama wanaoenda kujifungua vimepungua kutoka 74 mwaka 2015 hadi 46 mwaka 2020.

Dk. Mpuya ameongeza kwa kueleza kuwa kwa upande wa vifo vya watoto wachanga, mkoa huo umeweza kupunguza tatizo hilo kutoka vifo 1,340 mwaka 2015 hadi vifo 586 mwaka 2020.

Kaimu Mganga Mkuu (RMO) wa Mkoa huo, Dk. Nuru Mpuya.

Amesema kuwa wamepiga hatua hizo kutokana na juhudi mbalimbali walizozifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya ikiwemo kuboresha vituo vya afya 11 vikiwemo saba ambavyo sasa vinatoa huduma ya upasuaji, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa na uwepo wa wataalam wanaojengewa uwezo kupitia mafunzo kazini na  semina.

“Tumejitahidi kupunguza vifo hivi lakini bado kuna changamoto tunahitaji kuzifanyia kazi na kumaliza tatizo. Kila kifo kinapotokea ni kawaida timu kwenda kujiridhisha sababu zake na kujadili namna ya kuchukua hatua za kuzuia tatizo kutojitokeza tena, pia tunao mradi wa TAXI JAMII ambao umesaidia pale ambapo hakuna ambulance, taxi hizi hutoa huduma ya kusafirisha wagonjwa hususan akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua.

“Pia tunatoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuwasaidia akina mama wenye changamoto za uzazi. Tumeanzisha utaratibu wa kuwatambua wamama wenye dalili/vidokezo vya hatari, ambapo tunawafuatilia kwa ukaribu na kufanya usimamizi saidizi na shirikishi kwenye vituo vya kutolea huduma,” alieleza.

Katika hatua nyingine, Dk. Mpuya ameeleza kuwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana, jumla ya mabinti 759 wanaoishi katika mazingira hatarishi wamesaidiwa na kuwezeshwa kupata mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020, ili kuwanusuru na changamoto ya mimba na ndoa za utotoni.

Mbali na mafanikio hayo, Dk. Mpuya alieleza changamoto zinazoendelea kuwakumba, ambazo ni pamoja na uhaba wa watumishi ambao ni asilimia 30 ya mahitaji, ukosefu wa madaktari bingwa katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya hususan wa magonjwa ya akina mama na watoto, pia mwitikio mdogo wa watu kujiunga na huduma ya bima ya afya ya CHF Iliyoboreshwa ambapo ni asilimia 6.1 tu ya kaya zimejiunga na huduma hiyo.

“Mkoa utaendelea kuweka mipango yake kwa kushirikiana na wadau kuajiri watumishi, kupeleka madaktari wetu kujiendeleza kupata ujuzi wa kibingwa. Katika kupunguza vifo tunaendelea kuweka mazingira ya kupata madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto ili kuepuka tatizo hilo ambalo sehemu kubwa linasababishwa na umbali wa kufika sehemu za kupata huduma za afya,” ameeleza.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini (2015/16-2019/20) iliyotolewa Agosti 19, mwaka jana jijini Dodoma na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya hususani afya ya uzazi na mtoto, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma.

Ambapo, kuimarishwa kwa ubora wa huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto kumeleta ongezeko kubwa la akinamama wanaohudhuria mara nne au zaidi kwenye kliniki ya wajawazito kutoka akinamama 747,524 (asilimia 39) mpaka akinamama 1,758,191(asilimia 81) Juni 2020.

Pia, Kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka akinamama 1,226,707 (asilimia 64) mwaka 2015 mpaka akinamama 1,801,603 (asilimia 83) Juni 2020 na kuvuka lengo la asilimia 80 ambalo Serikali ilijiwekea katika Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto ya mwaka 2016-2020.

“Takwimu zetu za mwaka 2019/20 vifo vya watoto wachanga vilikuwa vifo 7 kati ya vizazi hai 1,000, ambapo takwimu za utafiti wa mwaka 2015/16 ilikuwa vifo 25 kati ya vizazi hai 1000. Hali hii inaashiria kuwa tutakapofanya utafiti wa hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini ifikapo mwaka 2021, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini Tanzania kitakuwa kuwa chini ya vifo 190 kwa vizazi hai 100,000 ukilinganisha na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kama ilivyotolewa taarifa kwenye utafiti wa mwaka 2015/16,” ilisema taarifa hiyo.

Vile vile, ilielezwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za mapitio ya vifo hivyo zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinazuilika, kwani, sababu zake ni pamoja na kupoteza damu wakati wa uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua na kifafa cha mimba ambavyo huchangia asilimia 50 ya vifo vyote. Sababu zingine zinazopelekea vifo vitokanavyo na uzazi ni pamoja na upungufu wa damu unaotokana zaidi na lishe duni na ukosefu wa madini chuma mwilini hasa wakati wa ujauzito, maambukizi ya bakteria baada ya kujifungua, uchungu kinzani, kupasuka mfuko wa uzazi

Moja ya wadau wa afya mkoani hapa, Shirika la Thubutu Africa Initiative linalofanya kazi za kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana kupitia mradi wake wa TULONGE AFYA umeweza kuwasaidia jumla ya vijana 51,917 kupata elimu hiyo katika wilaya ya Shinyanga na kuwasaidia kubadili fikra juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na kukomesha ukatili na unyanyasaji kwa wanawake.

Kwa mujibu wa Meneja Miradi wa Shirika hilo, Paskalia Mbugani, kwa mwaka 2020, jumla ya wasichana 18,028 na wavulana 18,958 walinufaika na elimu hiyo katika halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, huku vijana wa kiume 6,956 na wa kike 7,975 wakinufaika katika Manispaa ya Shinyanga kwa mwaka huo.

Vile vile, kwa mwaka 2019, Vijana wa kiume 6,844 na wasichana 3,331 katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakinufaika na wavulana 1,397 na wasichana 3,323 katika Manispaa ya Shinyanga wakinufaika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles