25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Makala: Mwamko wa jamii juu ya Uzazi wa Mpango Geita

Na Yohana Paul, Geita

MJI wa Geita, mkoani Geita ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi nchini kutokana na uwepo wa shughuli za uchimbaji wa madini na hivyo kuchagiza ongezeko la watu kwa maana ya wenyeji na wengine na kupelekea muingiliano mkubwa wa kijamii.

Inafahamika kuwa, serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na taasisi zisizokuwa za kiserikali imeendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi ili kuwaepusha kina mama na madhara yatokanayo na kuzaa mfululizo na pengine kupunguza kasi ya ongezeko la watu nchini.

Hadi sasa elimu ya afya ya uzazi imeonekana kuzaa matunda kwa kina mama walio na wasio kwenye ndoa kupangilia uzazi kwa kutumia njia za asili na zile za kisasa ambapo baadhi ya kina mama wakazi wa halmashauri ya mji wa Geita wameeleza kunufaika na elimu hiyo. 

Mwamko wa kina mama ukoje?

Velediana Renatus (35) mkazi wa mtaa wa Katundu kata ya Kalangalala Geita mjini anasema ana miaka 15 kwenye ndoa, na sasa ana watoto watano, amekuwa hatumii uzazi wa mpango za kisasa anakiri kwamba watoto aliowapata wamemtosha kwani maisha ni magumu.

Anasema suala la kupanga idadi ya watoto linategemea zaidi na uelewa wa mwanaume na kama ni muelewa, suala la kupishanisha watoto litawezekana na hata kuamua lini mpate ili kuepuka kuzaa kwa msongamano.

“Ukiwa siku za hatari, inatakiwa wewe mwanamke umwambie mwanaume, ndani ya siku kadhaa tendo la ndoa lisiwepo, mkielewana mnamudu, mkishindwana mwanaume akatumia lazima, utabeba mimba, ila mimi nikiwa nanyonyesha mwaka mmoja na iezi saba huwa siingii hedhi.

“Kuzaa watoto wachache kwa kweli inasaidia, mimi watoto nilionao kazi zangu nazimudu, napangilia, na kiukweli bila mwanaume kuelewa ningekuwa nazaa ovyo ovyo na mwisho wa siku wale watoto ningeshindwa kuwatunza, ila kwa sasa hivi nina uwezo wa kuwatunza,” anaeleza.

Naye Esther John (28) mkazi wa mtaa na kata ya Nyankumbu Geita mjini Geita, mjasiliamali mdogo anakiri kuzaa kwa mpangilio imemusaidia kumudu gharama za mavazi, malazi na chakula na gharama zingine za kuwatunza watoto.

“Mimi nikifikisha watoto wanne nitaenda kituo cha afya niangalie kufunga uzazi, kiukweli naogopa kuzidisha watoto maana tunaangalia na maisha yajayo, kwamba tunaweza kuwamudu, ila kwa sasa hawa watoto tulionao naweza kufanya kazi zangu vizuri,” anasema. 

Naye Kudrah Charles (32) mkazi wa mtaa wa Nyankumbu yeye ni mama wa watoto wanne na mjasiliamali mdogo wa matunda anasema amedumu kwenye ndoa kwa muda wa miaka 15 na sasa anatumia njia ya uzazi wa mpango wa kuweka njiti kila baada ya miaka mitano ili kutenganisha watoto.

Anasema alifikia hatua hiyo baada ya kujadiliana na mme wake na kufikia makubaliano wa namna ya kuzaa watoto wachache na kwa kusubiri miaka mitano ili kumpa nafasi yeye kama mama muda wa kupumunzika na kufanya kazi za ujasiliamali sokoni.

Anaeleza, yeye na mme wake wamejiwekea malengo ya kuzaa watoto sita pekee kusudio likiwa ni kupata watoto watatu wa kiume na watoto watatu wa kike na makubaliano yao ni kuwa watakapofikisha idadi hiyo ya watoto basi watasitisha kuzaa.

“Mume wangu ndio aliniambia nianze kutumia uzazi wa mpango, kwa sababu nilipozaa mara ya kwanza nilikaa nikiwa nanyonyesha baada ya miezi saba nikabeba ujauzito mwingine, kwa bahati mbaya nilikuwa nanyonyesha huku naingia siku zangu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima (aliyesimama katikati) akizungumuza na watumishi wa sekta ya afya mkoani Geita alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa hivi karibuni. Kushoto na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dk Japhet Simeo na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo.

“Kipindi hicho nilikuwa situmii njia yeyote, mme wangu akaniuliza, kwani hakuna njia ya kuzuia mimba?, ndio nikamwambia ngoja niende hospitali, nilianza kuchoma sindano, mara ya kwanza waliniambia zina madhara, lakini toka nimeanza kutumia sijaona madhara, mpaka sasa,” anasema Kudrah.

Anasema alitumia njia ya sindano kwa muda wa miaka mitatu, ndipo aliposhauriwa na muuguzi msimamizi wa kitengo cha uzazi katika kituo cha afya cha kata ya Nyankumbu kilichopo Geita mjini  kubadili na kuanza kutumia vidonge na baadaye njiti ambazo zimemusaidia sana hadi leo hii. 

“Kalenda ilinishinda kwa sababu siku zangu huwa zinaingiliana, ndiyo maana nikashindwa, kwa sababu huwezi kujua siku ya hatari ni ipi, ila nikitaka kuzaaa huwa naenda tu natoa njiti na sasa hivi inanisaidia kwa sababu huwez kufanya biashara ukiwa na watoto wadogo,” anaongeza.

Naye Sung’wa Joseph (43) mkazi wa Nyankumbu na mama wa watoto watano anasema yupo kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 20 lakini yeye na mme wake walishauriana kuzaa kwa mpangilio ili kuepuka kuzaa watoto wengi wasiowamudu ndipo wakachagua kutumia njia ya kalenda. 

Anasema, kushirikishana kwa pamoja juu ya kupanga watoto imekuwa na tija kwani mme wake amekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha hawafanyi tendo la ndoa kwa siku hatarishi kupata ujauzito na wamefanikiwa kwani hadi sasa ana miaka saba hajabeba ujauzito.

“Mimi natumia njia ya kalenda tu kupangilia watoto, toka nimeingia kwenye ndoa, ukiitumia vizuri hamna shida kabisa, nikiona siku za hatari namushirikisha mme na uzuri mme wangu anaelewa na kuzaa kwa mpango inasaidia sana, mwili unakaa vizuri, mimi nafanya kazi zangu vzuri,” anasema Sung’wa.

Kwa upande wake, Tatu Samson (35) mkazi wa mtaa mtaa wa Geseco kata ya Kalangalala anajishughulisha na kazi ya ushonaji, anaweka wazi kuwa matumizi ya uzazi wa mpango yamewasaidia sana yeye na mme wake kupata watoto kwa muda wanaotaka na kuwalea vizuri.

Anasema wamekuwa kwenye ndoa kwa kipindi cha miaka 17, sasa na wamezaa watoto wanne ingawa mtoto mmoja alifariki, lakini anakiri kuwa kupangilia uzazi kumempa nafasi ya kufanya kazi na watoto wameweza kusoma vizuri.

Anaeleza, kwa sasa anatumia njia ya kalenda kupanga uzazi lakini alishawahi kutumia njia zingine ambapo alitumia vidonge kwa muda wa miezi sita kwa bahati mbaya akapata maudhi kidogo kidogo ikiwemo kupata hedhi mara mbili kwa mwezi na kuongezeka kichefu chefu. 

“Nilipoona hivo nikaanza kuchoma sindano kwa muda wa miaka miwili, mkono ulianza kupooza, nikaenda kituo cha afya nikashauriwa nisitumie sindano wala vidonge mpaka niwe nimepimwa, maana ukitumia bila kupima inaleta shida.

“Ni kweli mimi nilianza kutumia nikiwa sijapimwa, mhudumu akanishauri niende kupimwa, baada ya kupimwa nikaanza kutumia vidonge sikuona madhara tena, kichefuchefu nikawa sioni na mzunguko wa siku zangu zikawa zinaenda vzuri tu, anaongeza.

Anasema kwa sasa anahitaji mtoto mmoja na akimupata ataenda kiuo cha afay akapate ushauri ili afunge kizazi lakini anafuraha kwenye ndoa kwani mme wake ndio  alimufundisha kalenda nay eye ndio huwa anamuelekeza hadi wameweza kupanga uzazi.

Mtazamo wa kina baba ukoje?

Faustine Mabula (30) ni baba wa watoto wawili na amekuwa kwenye ndoa kwa miaka nane sasa, anasema  ni ukweli ulio wazi kutumia uzazi wa mpango kuna  faida kubwa hasa kuwezesha kuwapatia watoto malezi bora na hata kuwasomesha kwa jinsi unavyotaka.

“Uzazi wa mpango utakusaidia kufikia malengo yako mwaka hadi mwaka, mimi nipo kwenye ndoa kwa miaka nane sasa, lakini nimekuwa nikifuatilia kalenda ya mke wangu ndio maana leo tuna watoto wawili ila malengo yetu ni watoto watano.

Mabula anaeleza kuwa, changamoto ya upatikanaji wa elimu na huduma kwa maeneo ya vijijini imewafnya watu wengi kutopangilia uzazi kwa kuwa wanazaa watoto wengi kwa ajili ya kupata nguvu kazi kwenye shughuli za uvuvi na ufugaji.

“Vijijini wegi hawatumii uzazi wa mpango kwa sababu ya shughuli za kilimo na ufugaji, wengi tunaamini siwezi kuzaa watoto wachache wakati nina mashamba makubwa,ndiyo maana ukiona hivo kwanza unaoa wanawake wawili au zaidi wakusaidie.

“Ukifanya hivyo utakuwa ma watoto wengi kwa ajili ya nguvu kazi, kwenye mashamba na mifugo, ukijibana sana utahangaika kuendesha miradi, lakini tatizo pia huduma za uzazi wa mpango kijijini zipo ila kidogo sana, ndio maana wengie hawaelewi na wanazaa watoto wengi,” anaeleza.

Taarifa za jumla mjini Geita

Akielezea mwenendo wa matumizi ya uzazi wa mpango mjini Geita, Muuguzi Mkuu Halmashauri ya mji wa Geita, Caritus Ntambi anasema hadi sasa kiwango cha matumizi ya uzazi wa mpango bado hakizidi nusu.

Anasema watumiaji wa uzazi wa mpango katika halmashauri ya mji wa Geita imefikia asilimia 35.3 kiwango ambacho bado ni kidogo ikilinganishwa na uhalisia wa idadi ya watu.

Anasema takwimu zinaeleza asilimia 25 ya kina mama wanaojifungua wanatakiwa kutumia huduma ya uzazi wa mpango, lakini mpaka sasa kwa walio wengi hawafanyi hivo.

Anasema juhudi zinaendelea kufanyika kutoa elimu ya uzazi ili kuongeza idadi ya watumiaji wa uzazi wa mpango, kwani tafiti zinaonyesha uzazi wa mpango umesaidia kupunguza vifo vya wajawazito wanaojifungua kwa asilimia 40.

Aidha halmashauri ya mji wa Geita imeendelea kuhamasisha wakina mama wajawazito chini ya wiki 12 kuhudhuria kliniki ili kupata elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango, ambapo jumla ya wanawake 1,185 walihudhuria kliniki kwa kipindi cha kuanzia julai na desemba 2020 sawa na 36% ya lengo la 40%.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles