30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Mfahamu Bernard Membe

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Leo Ijumaa Mei 12, 2023, majira ya saa tano za mchana, taarifa ya kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, kutoka Chama cha Mapinduzi, (CCM), ndipo zilipoanza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Amefariki asubuhi katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam, baada ya kupelekwa alfajiri ya leo. Msaidizi wa Membe, Allan Kiluvya ameeleza kwa vyombo vya habari kuwa alipata changamoto ya kifua.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia mtandao wa Twitter amemwelezea marehemu alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi kwa weledi.

Baada ya kumaliza masomo ya juu nchini Marekani mwaka 1992, Membe alipewa kazi ya kuwa mshauri katika Ubalozi wa Tanzania, huko Ottawa nchini Canada, kutoka mwaka huo hadi 2000.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Hayati Bernard Membe.

Membe ni mwanachama mkogwe wa CCM, aliyepata kukitumia chama hicho katika nafasi ya Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwongo mmoja na nusu, kutoka mwaka 2000 hadi 2015.

Kufuatia uchaguzi mkuu wa 2005, uliomuweka madarakani Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete; Membe aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa mambo ya ndani. Mabadiliko ya baraza la Mawaziri ya Oktoba 2006, yakamuhamisha na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini.

Chini ya serikali hiyo hiyo, Membe akashika nyadhifa kubwa zaidi, pale alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichukua kijiti hicho kutoka kwa Asha-Rose Migiro. Alikaa katika nafasi hiyo kutoka 2007 hadi 2015.

Membe alipata kushika wadhifa wa uenyekiti wa baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja wa Afrika, mwaka 2008. Pia, alikuwa mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe – 2013, kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Tanzania ilifungua balozi katika nchi mbali mbali ulimwenguni. Pia, Tanzania ilipokea viongozi wakubwa ulimwenguni kama Raisi wastaafu wa Marekani George W. Bush, Barack Obama, Xi Jinping (China) na Jacob Zuma (Afrika Kusini

Mbio za urais na mvutano ndani ya CCM Membe

Membe aliwahi kuwania kuteuliwa na chama tawala (CCM) kuwania urais katika uchaguzi Mkuu wa 2015

Membe alikuwa miongoni mwa makada wa CCM alioingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya chama hicho kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2015. Jina lake likawa miongoni mwa yaliyokatwa na kupitishwa jina la hayati John Pombe Magufuli.

Kukosa nafasi ya kuiwakilisha CCM kukawa ndio mwanzo wa mwanasiasa huyo kuingia katika mvutano na chama chake na kuonekana kana kwamba anamtunishia misuli Rais Magufuli. Na hilo alikuishia vizuri.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo, hayati Bernard Membe, anayebusu kadi ya CCM baada ya kukabidhiwa na Shaka katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtama, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtama mkoani Lindi.

Februari 2020 alifukuzwa uanachama na CCM, kupitia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, akituhumiwa kukiuka miiko na katiba ya chama. Mwenyewe alikana tuhuma hizo na kusema alifukuzwa kwa kuwa alitaka kugombea na kushindana na Magufuli ili ateuliwe kuiwakilisha CCM katika ngazi ya urais.

Membe alijiunga na ACT Wazalendo Julai 2020, na kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huo, na kupata asilimia 0.5 ya kura zote. Uchaguzi ambao ulimrudisha Magufuli wa CCM madarakani.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 Membe alihamia chama cha upinzani cha ACT na kuchukua fomu za kuwania urais Tanzania

Alipotoka

Barnad Kamilius Membe amefariki akiwa na miaka 69 – alizaliwa Novemba 9, 1953, Rondo, Chiponda mkoani Lindi, wakati huo Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania ikiwa chini ya himaya ya Mkoloni, Mwingereza.

Alianza kupata elimu yake ya msingi mwaka 1962, katika shule ya Chiponda, Lindi. Elimu ya sekondari aliipata shule ya Namupa Seminary, Lindi. Sekondari kidato cha tano na sita aliipata Itaga Seminary, Tabora.

Membe alisoma Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nchini Tanzania. Alijiendeleza kielimu, katika chuo kikuu cha Johns Hopkins, nchini Marekani katika fani ya Uhusiano wa Kimataifa kati ya1990 na 1992.

Membe ameacha mjane mmoja na watoto watatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles