Na Yohana Paul, Geita
AFYA ya Uzazi na Uzazi wa Mpango ni miongoni mwa huduma muhimu zinazoigusa jamii moja kwa moja ambapo serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeendelea kuboresha huduma za hizo ili kufanikisha adhima ya uzazi salama kulenga kuimarisha nguvu kazi ya taifa.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba uzazi salama ni muhimili wa maendeleo ya taifa na huaksi maono ya nguvu kazi ya taifa ambayo utimirifu wake hutokana na uimara wa afya za wananchi na ndio kiini cha mafanikio ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya taifa.
Mwezi aprili mwaka huu, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu akihutubia bunge, anasema kwa miaka mitano iliyopita nchi imepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3.
Samia anasema, katika miaka hii mitano mpaka 2025, serikali imelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi.
Anasema serikali imeweka juhudi za makusudi kupunguza vifo vya wajawazito na watoto hususani kupitia Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ili kutilia mkazo uwajibikiaji wa wadau wote katika kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuweza kuzuia mwanamke kupoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika.
MKAKATI WA WIZARA YA AFYA
Akisoma Muhtasari wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Waziri mwenye dhamana Dk. Dorothy Gwajima anasemaserikali imejipanga kushirikiana na wadau wote kutekeleza Vipaumbele husika ili kuboresha utoaji wa huduma za afya, ustawi na maendeleo ya jamii.
Dk Gwajima anasema serikali inalenga kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za chanjo ili kuwakinga watoto chini ya miaka 5, akina mama wajawazito na kutoa chanjo nyinginezo za kimkakati za kukinga na kudhibiti magonjwa yanayozuilika kama Homa ya Ini, kichaa cha mbwa sambamba na Kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga vinavyotokana na uzazi;
Anasema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 huduma za chanjo zimefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95 katika kuwapatia chanjo walengwa wake wote huku mahudhurio ya wajawazito kliniki yalikuwa mazuri kwa asilimia 93.4 ingawa changamoto ni kuwa asilimia 36 tu walihudhuria kliniki kwa mara ya kwanza ndani ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito.
Anasema hali hiyo inachangiwa na mila na desturi za kutotoa taarifa za mimba changa katika kipindi hicho, ambapo serikali imepanga kutoa zaidi elimu ya afya ya uzazi kwa kuwa mbali na hilo upatikanaji wa dawa muhimu za Afya ya uzazi ulikuwa wa kuridhisha kwani kati ya wajawazito 1,101,830 sawa na asilimia 63 waliohudhuria kliniki walipata dawa zinazostahili kwa mama mjamzito.
“Idadi ya kina mama wajawazito waliojifungulia kwenye Vituo iliongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2015/16 hadi asilimia 81 mwaka 2020/21 jambo ambalo linachangia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
“Idadi ya akina mama waliojifungua na kurudi kliniki siku mbili baada ya kujifungua iliongezeka hadi asilimia 62 mwaka 2020/21 kutoka asilimia 34 mwaka 2015/16; Jumla ya Shilingi bilioni 24 zimetumika kukarabati vituo 813 kwa kujenga upya miundombinu ya maji na usafi wa mazingira,” anasisitiza Dk Gwajima.
Anaongeza kuwa, idadi ya Vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka 8,446 mwaka 2019/20 hadi 8,458 Machi 2021 huku hali ya upatikanaji wa dawa muhimu 312 katika vituo vya huduma za afya ikifikia asilimia 75.6 na katika maghala ya MSD asilimia 21 huku Serikali ikiongeza mtaji wa dawa na hadi kufikia Aprili 2021, Shilingi bilioni 151.38 zilitolewa na hazina
Anasema, jumla ya miradi 22 ya ujenzi wa Hospitali mpya, ukarabati wa majengo na upanuzi wa miundombinu ikiwemo ya TEHAMA kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa Kanda na Hospitali Maalum imeendeleakutekelezwa kwa thamani ya Shilingi bilioni 193.3 ambapo hadi kufikia Machi 2021, Shilingi bilioni 130.6 zimetolewa
“Aidha, Wizara imeendelea kufanya kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni katika mikoa mbalimbali nchini ambapo jumla ya wanafunzi 8,978 katika Shule za Msingi na wanafunzi 345 katika Shule za Sekondari na walimu 40 walifikiwa na kupata elimu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.
Dr Gwajima anaeleeza, katika kupinga na kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto Wizara imeendelea kutoa elimu kwa jamii na kupitia kampeni na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo Kampeni ya ‘‘Twende Pamoja: Ukatili Tanzania Sasa Basi”
Anasema katika Kukamilisha miradi 22 ya upanuzi, ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda na Maalum. Jumla ya Shilingi bilioni 193.2 zimetengwa;
Dk Gwajima anaongeza, katika Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi jumla ya Shilingi bilioni 263.8 zimetengwa. Kuimarisha huduma za afya nchini kwa kulenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Anasema, Wizara inaendelea na usambazaji wa vifaa na vifaa tiba ili kuviwezesha vituo vya afya vilivyoboreshwa kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni pindi mama anapokabiliwa na uzazi pingamizi na pia jumla ya Shilingi milioni 791 zimetengwa kwa ajili ya kuratibu kampeni za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa mwaka 2021/22.
BAJETI YA SERIKALI
Dkt. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2021/22, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 36.33 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote
Anasema, kati ya bajeti hiyo, Shilingi bilioni 233.3 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kama sehemu ya maboresho ya huduma za afya nchini na serikali imeendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo vituo vya kutolea huduma za afya kwa ngazi mbalimbali vimeendelea kujengwa.
“Sekta ya Afya ni sekta muhimu katika ustawi wa jamii yetu na ni moja ya mahitaji muhimu sana katika maisha ya sasa ya mwanadamu. Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana katika sekta hii, ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mabadiliko ya hali za kiafya kwenye kizazi cha leo.
“Hadi kufikia Juni 2021, kuna jumla ya maboma 8,004 ya zahanati ambayo yapo katika mikoa mbalimbali nchini na yapo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa. Vilevile, yapo maboma kwenye ngazi ya vituo vya afya zaidi ya 1,500 ambayo yametumia nguvu ya wananchi na yanahitaji kukamilishwa,” anasisitiza.
Aidha Dk. Mwigulu anasema serikali pia inaendelea kuboresha mazingira na sera ya elimu kwani kila mwaka kuna wanafunzi kati ya asilimia 15 – 20 wanatoka kwenye mfumo wa elimu kwa kutoendelea na kidato cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kupata ujauzito, utoro na hali ngumu ya maisha.
HALI IKOJE KITAIFA
Matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015-2016 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaonyesha kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya utafiti huo nchini, hali ya kiwango cha vifo kwa watoto wanaofariki kabla ya kutimiza umri wa mwezi mmoja ni vifo 25 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.
Aidha, kiwango cha vifo kwa watoto wachanga (idadi ya vifo miongoni mwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja) ni vifo 43 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai huku kiwango cha vifo kwa watoto wanaofariki kabla ya kutimiza miaka mitano ni vifo 67 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.
TDHS inaeleza takribani wanawake wote 98% wenye umri wa miaka 15-49 hupatiwa huduma ya mama mjamzito kutoka kwa mtoa huduma mwenye ujuzi, huku 24% ya wanawake ndio waliokuwa wamehudhuria kliniki katika mwezi wa nne wa ujauzito wao kama inavyoshauriwa.
Pia asiliami 51 ya wanawake walitembelea sehemu ya kutolea huduma ya afya mara nne au zaidi katika kipindi chao cha ujauzito na ili kusaidia kuzuia matatizo yanayoweza kutokea baada ya kujifungua asilimia 34 ya wanawake walipatiwa huduma ya uchunguzi katika siku mbili baada ya kujifungua.
Hadi mwaka 2015-2016 utafiti ulionyesha takribani theluthi mbili (63%) ya watoto nchini huzaliwa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya hasa vile vinavyomilikiwa na serikali huku ingawa ni asilimia 42 ya watoto wachanga walipatiwa huduma ya uchunguzi katika siku mbili baada ya kuzaliwa.