23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 9, 2023

Contact us: [email protected]

‘Kuchukulia poa’ kunavyoiweka Dar hatarini maambukizi Corona

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

JANGA la virusi vya Corona, hususan wimbi la tatu, limebadili maisha ya maeneo mengi duniani. Hata hivyo, kwa baadhi ya wananchi wa Dar es Salaam mfumo wao bado ni uleule wa siku zote.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi.

Kwani kama tunavyofahamu kwamba maeneo mengi yamepiga marufuku misongamano, kutilia mkazo uvaaji wa barakoa kwenye vyombo vya usafiri wa umma na kunawa mikono kadri inavyowezekana. Hata hivyo, wengine wameenda mbali zaidi kwa kuweka zuio la wananchi wake kutokutoka nje (Lockdown), uamuzi ambao Tanzania bado haujafikia.

Dar es Salaam ni miongoni mwa ile ambayo Mkuu wake wa Mkoa, Amosi Makalla, ametoa agizo Julai 26, mwaka huu, akikazia wananchi kuvaa barakoa kwenye maeneo ya stendi, kivuko cha Kigamboni na kwenye vyombo vya usafiri wa umma.

Licha ya agizo hilo kutolewa, bado mwitikio wa utekelezaji wake umekuwa hafifu huku kila mmoja akitoa sababu zake anazoamini kuwa yuko sahihi.

Kwani kwenye vyombo vya usafiri wa umma kama mabasi yaendayo haraka misongamano ni mikubwa ingawa wengi wanavaa barakoa.

Hali hiyo ya msongamano ndiyo iliyoko pia kwenye usafiri wa daladala ambapo baadhi ya abiria bado wanakubali kusimama huku wanafunzi ndio wakiwa wahanga wakubwa pamoja na kutokuwa na barakoa.

Baadhi ya wakazi hao wa Dar es Salaam, akiwemo Theresia Cloud (38), ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Ubungo, amesema haoni haja ya kuhangaika na barakoa kwa sasa kwani janga hilo lilishakuja na kupita, hivyo hata hili litapita kwa uwezo wa Mungu.

“Ugonjwa wenyewe uko wapi? Mbona wimbi la kwanza lilikuja na tukamuomba Mungu na maisha yanaendelea? Hivyo, hatuwezi kuacha kwenda kutafuta fedha eti kisa magari yamejaa.

“Najua Mungu ninayemuamini ataendelea kunitetea kama ilivyokuwa huko nyuma. Wangapi waliovaa barakoa huko nje na wamefariki,” amesema Theresia.

Wakati akisema hayo, kwa upande wake, Amina Hamoud (32), ambaye ni mwanafunzi wa elimu ya juu na mkazi wa Yombo Vituka, amesema anaona kupanda na barakoa kunamfanya aonekane ‘anajishaua’.

“Kaka yangu nikwambie, huku kwetu ukipanda kwenye gari ambalo wengi hawajavaa barakoa, halafu wewe umevaa unaonekana kama unajishaua. Kwa hiyo ndio maana inabidi tu kuendelea na maisha yetu.

“Kwanza unapumua kwa shida ukivaa, kama ni kunawa tutanawa tu maisha mengine yaendelee lakini huu uzungu wa kutembea umevaa ‘madude’ wakati huumwi inakuwa ni changamoto, wengine hatujazoea,” amesema Amina.

Naye Martin Mazugwa, dereva wa daladala la Gongo la Mboto–Makumbusho, amesema: “Elimu bado ndogo kwa sababu mwanzoni ilikuja imani kwamba hizi barakoa za kitaalamu zina matatizo, zinaweza kuwa zimepandikiziwa virusi. Hizi za mitaani nazo zilishawahi kutolewa kasoro, kwamba zinasababisha usipumue vizuri kwani hazifuati utengenezaji wa kitaalamu.

“Pia, kwa upande wangu, hapa kwenye usukani ni mbali na abiria wengine na kumbuka nina kioo kulia kwangu, hivyo napata hewa ya kutosha,” anasema.

Dereva huyo anasema anajitahidi pia kufuata masharti yaliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa abiria wanaowabeba ni waliokaa kwenye viti. Hata hivyo anasema, anapokuja mwanafunzi amechelewa masomo na hawezi kusubiri gari jingine siyo rahisi kukubali kulipa shilingi 400 ili akae hivyo wanalazimika kusimama.

“Au mama anatoka huko alikotoka anakwamba ana haraka sana na anataka kuwahi na anakwambia kama ni kufa atakufa yeye, sasa hapo hebu niambie kama ni wewe utafanya nini?”

Ama hakika dereva huyo anawakilisha sehemu ya Watanzania wengi ambao kwao suala la kuzingatia usalama wa afya zao bado ni changamoto.

Hivyo, elimu inapaswa kutolewa zaidi ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo maelekezo hayo yanayotolewa na Serikali.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema kuwa wameanza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa elimu inatolewa ikiwa ni pomoja na kuwaelimisha madereza na makondakta wa daladala ili waweze kuwa makini kwa abiria wao.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa Madereva na Makondakta ili kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa abiria wao juu ya kuzingatia afya zao, kama mtu atakuta gari limejaa basi asipande asubiri jingine ikiwamo pia kuvaa barakoa,” amesema Makalla. “

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,351FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles