28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Chuo cha DIT – MYUNGA mkombozi wa maendeleo mkoani Songwe

Na Regina Kumba, DIT

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Myunga ilianza mwaka 2014 wakati Baraza la Taasisi hiyo lilipokabidhiwa rasmi na Serikali majengo na miundombinu ya iliyokuwa kambi ya Ujenzi wa Barabara Ikana-Lahela kilichopo Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe.

Eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na Mradi wa “Millenium Challenge Account-Tanzania (MCA-Tanzania) likisimamiwa na “Tanzania Roads Agency (TANROADS)” Tanzania.

Mwaka 2017 Baraza la Taasisi lilianzisha DIT-Kampasi ya Myunga na kuelekeza Menejimenti ya DIT kupata hatimiliki ya eneo la DIT Kampasi ya Myunga, kuanza kutoa mafunzo ya ufundi stadi, kutoa mafunzo ya kozi fupi, kurekebisha na kujenga miundombinu mipya, kufufua maabara ya kupima udongo na kuanzisha mafunzo ya Ufundi Sanifu katika ujenzi chini ya baraza la Taifa la Ufundi (NACTE).

Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Dk. Richard Masika anasema mwaka 2019 DIT- Myunga ilipata usajili wa kuendesha mafunzo ya Ufundi Stadi chini ya Vocation Education Training Authority (VETA).

Mwaka 2020 ilipata usajili kuendesha shughuli za kutoa huduma za upimaji ubora wa vifaa vya ujenzi chini ya ‘Engineering Registration Board’, mwaka 2021 ilipata usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Tanzania (NACTE) na mwaka huo huo Taasisi ilipata hati ya kumiliki eneo la DIT Myunga, lenye ukubwa wa hekari 120.

Mhandisi Dk. Masika anasema pamoja na mafanikio mengi ya Taasisi, bado kuna changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na uhaba wa watumishi na ufadhili wa kundi maalumu la wanafunzi wa shahada ya uhandisi ili kufikia lengo linalokusudiwa.

“Kwa kuwa nia ya Taasisi ni kutoa mazao bora ya wahitimu kwa uwiano wa mhandisi mmoja fundi sanifu watano na fundi stadi 25, ambao wanatarajiwa kuchangia katika kuchachua uchumi wa viwanda, kumekuwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na ufadhili kwa kundi maalum la wanafunzi,” anasema.

Mhandisi Dk. Richard Masika.

Aidha, changamoto nyingine anazitaja kuwa ni kukosekana kwa miundombinu rafiki ikiwemo mabweni ya kutosha kwa wanafunzi wa jinsia ya kike, utayari mdogo wa viwanda kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wetu, nafasi za waalimu wetu kujifunza viwandani “Staff Industrial Attachment” na wataalam wa viwandani kujitolea kutoa uzoefu wao katika Taasisi na uhitaji wa kuongeza maeneo katika Kampasi ya Myunga.

“Sambamba na malengo ya uanzishwaji wa Kampasi hii, mojawapo ikiwa ni kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Uchimbaji wa madini, ikiwezekana Taasisi iongezewe eneo linalopakana na Kampasi ya Myunga “Blasting site”, ili kutoa fursa kwa vijana kusoma fani hiyo kwa vitendo,” anasema Mhandisi Dkt. Masika.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojhia Dar es Salaam, Prof. Preksedis Ndomba anasema kwa mwaka huu wa masomo 2021/2022 DIT Myunga imedahili wanafunzi 11 katika ngazi ya stashahada ya Uhandisi wa Ujenzi, na wanafunzi 10 katika fani ya ufundi bomba na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi waliodahiliwa kuwa ni 21 idadi ambayo inawiana na rasilimaliwatu na miundombinu iliyopo kwa sasa.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojhia Dar es Salaam, Prof. Preksedis Ndomba.

Anasema DIT inandesha mafunzo yake kiubunifu zaidi kwa kuhusisha mafunzo darasani, atamizi za teknolojia (technology incubator) na mafunzo kwa vitendo viwandani (Teaching factory) kukidhi mahitaji ya soko.

Aidha, uanzishwaji wa atamizi (Incubator) una lengo la kuwawezesha wahitimu kuingiza bunifu zao sokoni ili kuwawezesha kujiajiri na kuanzisha viwanda vidogo vidogo. Vile vile, mafunzo ya vitendo viwandani yanatekelezwa kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanda na maeneo mbalimbali ya kazi halisi za uzalishaji nje ya Kampasi.

“Katika mpango huu, tunashirikiana na Taasisi mbalimbali ndani na nje ya Mkoa Songwe ili kuwawezesha wanafunzi kutembelea na kushiriki kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo husika,” anasema Prof. Ndomba.

Kozi zinazotolewa Katika Kampasi ya DIT Myunga ni Stashahada ya Ufundi Ujenzi(Diploma in Civil Engineering) 11, Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi Bomba (NVA in Plumbing and Pipe Fitting) 15 na Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi wa mifumo ya TEHAMA saba jumla wanafunzi 33.

Katika mwaka wa masomo 2020/2021 jumla ya wahitimu walitunukiwa vyeti vya kuhitimu mafuzo ya Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi Bomba (National Vocational Award (NVA) Level II in Plumbing and Pipe Fitting), pamoja na wahitimu Sabini (65) wakitunukiwa vyeti vya kufuzu mafunzo ya wanagenzi katika fani za Ufundi Bomba na Ufundi wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Mafunzo haya mafupi yamefanyika kwa kwa ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

”Naomba nieleze pia kwamba, Wahitimu wa programu hizi ni mafundi stadi wanaohitajika sana kuhudumia sehemu mbalimbali zikiwemo mashuleni, mahospitalini, ofisi na maeneo yote yanayotumia mifumo ya TEHAMA” anaongeza Prof. Ndomba.

Wahitimu hao katika ngazi ya pili ya mafunzo ya ufundi stadi katika fani ya Ufundi bomba (NVA Level II in Plumbung and Pipe fitting), walidahiliwa na kuanza masomo yao katika mwaka wa masomo 2019/2020, ambao mfumo wa utoaji mafunzo ulikuwa ni muda mwingi kwenye vitendo wakiwa hapa Chuoni, lakini pia katika miradi mbalimbali ya maji inayosimamiwa na RUWASA.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba anasema Kampasi ya DIT Myunga ipo katika himaya ya Mkoa wake hivyo Kampasi hiyo ni kwaajili ya maendeleo ya eneo hili na kukuza maendeleo ya mkoa wa Songwe na Taifa kwa Ujumla.

“Ninashawishika kuamini kwamba uwezo mkubwa mlionao na shughuli nzuri mnazozifanya katika Kampasi yenu kuu ya Dar es Salaam zitafanywa pia hapa kwa kiwango na ufanisi ule ule na hivyo kupaisha Sekta ya elimu katika mkoa wetu,” anasema Mgumba.

Aidha, Mgumba anasema kuwa Mkoa wa Songwe ni mpya ukilinganisha na mikoa mingine hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya ili kupata maendeleo kama ilivyo katika mikoa mingine.

“Tunahitaji wataalamu mbalimbali na wadau wa maendeleo ili kuendana na kasi tuliyoikusudia, ni matumaini yangu kuwa wataalamu wa Taasisi hii pia tutawatumia katika kushauri na kutekeleza mikakati mbalimbali ya maendeleo mkoani mwetu,”.

“Juhudi zilizofanywa na Taasisi ya DIT katika kupahuisha mahali hapa kwa muda mfupi ni dhahiri kwamba mna azma ya kupaendeleza mahali hapa kama serikali ilivyotarajia na mimi nitoe ahadi kuwa Serikali ya Mkoa wa Songwe itaungana nanyi kwa kutoa msaada utakaohitaijika kutoka sekta mbalimbali zilizopo chini ya mamlaka yangu kuhakikisha kwamba maendeleo ya kweli yanafikiwa,” anasisitiza Mgumba.

Anasema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kupiga vita umaskini kwa kuweka mazingira mazuri kwa wahitimu wa vyuo, ikiwemo DIT waweze kujiajiri.

“Jambo hilo linawezekana endapo wahitimu wetu watakuwa na moyo wa uthubutu wa kuanzisha biashara/ makampuni/ viwanda kwa kutumia elimu na ujuzi walioupata vyuoni.

idha, Serikali inalenga kuendelea kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, nishati miundombinu ya mawasiliano na usafiri” anasema Mgumba.

Mgumba anatoa mwito kwa DIT kuweka juhudi za dhati katika kuboresha mafunzo ya ufundi sanifu na ufundi stadi ili kupata maendeleo na ukuaji wa uchumi wa haraka.

Mkoani Songwe, DIT inalea wabunifu, mmojawapo akiwa ni Adam Kinyekile anayefanya shughuli zake Tunduma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles