Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Jumamosi ya Februari 17,2024 safari ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ilihitimishwa rasmi nyumbani kwake Ngarash Wilaya ya Monduli mkoani Arusha huku Watanzania wakikumbuka alama ambazo ameziacha.
Ujenzi wa shule za sekondari kila kata maarufu ‘shule za kata’ ni moja ya kumbukumbu ya kudumu ya Lowassa kwa Watanzania.
Lowassa akiwa Waziri Mkuu alisimamia shule hizo ambazo zimeongeza idadi ya wanafunzi tofauti na miaka ya nyuma ambapo wengi walikosa nafasi kutokana na uhaba wa shule.
Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake wakati wa maziko ya Lowassa, alisema idadi ya wanafunzi wa sekondari imeongezeka kutoka 265,000 mwaka 2004 hadi kufikia milioni 2.8 mwaka 2023.
Rais Samia anasema Lowassa alipenda vijana wapate maarifa na ujuzi na ndiyo maana kipaumbele chake cha kwanza hadi cha tatu kilikuwa ni elimu kama nyenzo ya kujikomboa na umaskini.
Anasema misimamo yake katika elimu ndiyo ilimsukuma kusimamia kwa mafanikio mipango ya maendeleo ya elimu ya sekondari na kusimamia ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata nchini.
Lowassa pia anakumbukwa namna alivyosimamia uanzishwaji wa programu ya kuendeleza walimu (Crash Program) maarufu kama ‘voda fasta’ iliyokuwa na lengo la kukabili changamoto ya uhaba wa walimu hasa kutokana na ongezeko la wanafunzi wa sekondari.
Rais Samia anasema katika kufanyia kazi maono yake mwaka 2023 Serikali ilifanya maboresho ya sera ya elimu na mitaala ya elimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya sasa.
Maji kutoka Ziwa Victoria
Uunganishaji maji kutoka Ziwa Victoria kwa wakazi wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora ni mradi mwingine utakaokumbukwa.
Lowassa alipokuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Uvuvi licha ya shinikizo kubwa la kutotumia maji ya Ziwa Victoria lakini kwa ujasiri na ushupavu wa uongozi alishauri vema Serikali na hadi sasa maji hayo yanatumika katika mikoa hiyo.
Pia alisimamia na kufuatilia kwa karibu uundwaji wa mamlaka za maji za miji mikuu ya mikoa zilizoleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za maji safi na uondoaji wa majitaka.
“Somo hapa ni kwamba tukipewa dhamana za uongozi kwa kuaminiwa katika nafasi mbalimbali ni lazima tuwe na uthubutu na ubunifu pamoja na kujitoa mhanga kusimamia na kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa weledi na uaminifu bila kukubali kuyumbishwa.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wetu katika maeneo tuliyokasimiwa, tusisubiri kusukumwa daima tuwe mbele tuweze kuona mbali zaidi ya wale tunaowaongoza,” anasema Rais Samia.
Alikuwa mlezi
Lowassa alikuwa mlezi aliyelea na kukuza wanasiasa vijana wengi ambao wanaendelea kulitumikia taifa mpaka sasa.
Rais Samia anasema Lowassa alilea kwa kujenga na si kwa kubomoa huku akikumbuka alivyofanya naye kazi yeye akiwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, bungeni na kwenye Kamati Kuu ya CCM.
“Kwenye suala la ulezi nikiuliza waliopata malezi ya Lowassa kuanzia Monduli, serikalini, bungeni kwenye CCM hata chama cha Mbowe (Chadema), mikono mingi sana itainuliwa.
“Nilijifunza mengi kutoka kwake kati ya hayo nililoliona kwa mheshimiwa Lowassa ni kwamba ukimheshimu anakuheshimu,” anasema Rais Samia.
Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Maasai Tanzania, Isack Meijo, anasema Lowassa aliwaunganisha Wamaasai wote, kuwahamasisha elimu na kuacha mila potofu kama za ukeketaji.
“Ni mtu mwenye upendo, mnyenyekevu, hakati tamaa, ana ushawishi mkubwa ndani ya jamii na taifa na anakubalika na kila mtu.
“Alikuwa na kawaida kila mwisho wa mwaka anaita jamii yake tunakula nyama, tunachinja zaidi ya madume 12 tunakula…si kwamba anachinja kwa sababu ni tajiri bali ana moyo wa kushirikiana na watu wa aina yote.
“Hapendi umaskini alikuwa anafundisha watu waondokane na ufukara na amefanya hivyo kwa Wamasai alipeleka watu Uganda kujifunza kuhusu jinsi ufugaji,” anasema Meijo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anasema Lowassa alikuwa na karama ya ajabu aliyeweza kuunganisha makundi mbalimbali wakati wote.
“Alikuwa na unyenyekevu mkubwa sana, alileta kasi ya ukuaji wa demokrasia katika nchi yetu, yeyote aliyefanya kazi na mheshimiwa Lowassa aliishia kuwa rafiki yake. Alikuwa hana mipaka ya kikabila wala kiimani, alimfanya kila mtu kuwa rafiki yake,” anasema Mbowe.
Ukomavu wa kisiasa
Itakumbukwa Julai 28,2015 Lowassa alijiengua CCM na kujiunga na Chadema baada ya kuenguliwa kugombea urais.
Aidha Julai 30,2015 Lowassa alichukua fomu ya urais kupitia Chadema na baadaye chama hicho kiliungana na vyama vingine vya CUF, NLD na NCCR – Mageuzi katika muungano uliokuwa ukijulikana kama Ukawa.
Katika kinyang’anyiro hicho cha urais Lowassa alipata kura zaidi ya milioni sita ambazo hazijawahi kupatikana kwa upinzani katika uchaguzi mkuu hatua iliyowezesha upinzani kupata idadi kubwa ya wabunge na madiwani.
Hatua yake ya kuhamia upinzani ilisababisha kutupiwa maneno na kashfa nyingi lakini wakati wote huo hakuwahi kutoa kauli za kejeli badala yake alitanguliza utaifa mbele na mara zote alisisitiza amani.
Aliporejea CCM Machi Mosi,2019 Lowassa aliwashukuru Watanzania kwa kumpigia kura milioni sita na kusema nilikuwa kura nyingi.
Lowassa alikemea siasa za ubaguzi huku akiwataka Watanzania kuwa kitu kimoja kwani wote ni ndugu.
Rais Samia anasema Lowassa alichipukia na kulelewa na CCM lakini alipofanya maamuzi ya kuhamia chama kingine aliendelea kunadi sera zake na kuifafanua dhana ya safari ya matumaini bila kutukana, kukejeli au kumzushia mtu uongo.
“Aliwahi kuhama kutoka CCM kwenda Chadema mpaka aliteuliwa kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, hakuwahi kuwananga wala kusema vibaya kule alikotoka.
“Tunapata somo kubwa la siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kusameheana na siasa za kuleta maendeleo. Huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa na ni njia nzuri ya kuchukua kama tunataka kumuenzi Lowassa na vitendo vyake,” anasema Rais Samia.
Alichotufundisha ni kwamba tunaweza kutofautiana mitazamo, misimamo na sera bila kutukanana, kulumbana wala kutikisa misingi ya utaifa na mshikamano na bado tukaelewana.
Huyo ndiye Edward Ngoyai Lowassa. Mungu amlaze mahala pema peponi.