Mwandishi Wetu, Ukerewe
Zaidi ya makaburi 80, yamechimbwa katika Kijiji cha Bwisya kwa ajili ya kuzika watu waliofariki katika ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere, iliyotokea Septemba 20, mwaka huu huko Ukerewe jijini Mwanza.
Tayari miili tisa ambayo haijatambuliwa imeanza kufanyiwa ibada ya mazishi katika kijiji hicho tayari kwa mazishi ya halaiki ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mmoja wa watendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza ambaye hakutaja jina lake, akihojiwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1), kuhusu idadi hiyo ya makaburi huku kukiwa na majeneza tisa pekee amesema bado kuna miili mingine inaendelea kuopolewa na mingine inaandaliwa ambayo itakuja kuzikwa katika makaburi hayo.
“Bado kuna miili inayoibuka kutoka chini inendelea kuopolewa, kwa hiyo makaburi hayo yameandaliwa maalumu kwa wale wanaopatikana na wanaendelea kupatikana ndiyo watazikwa hapo pia kuna miili mingine imeibuliwa hivi punde imeenda kuandaliwa kwa ajili ya maziko,” amesema.