Christina Gauluhanga Na Faustine Madilisha (TUDARCO)-Dar es salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili imeamua kutumia vipimo vya vinasaba (DNA), kutambua ndugu wa majeruhi wa moto wa lori la mafuta waliolazwa hospitalini hapo, baada ya kujitokeza watu wasiojuana kila mmoja akidai kuwa na uhusiano na wagonjwa hao.
Utata mwingine ni watu hao kutoa alama za utambuzi kwa wagonjwa hao kuwa ni walionyoa nywele mtindo wa kiduku, ilihali karibu majeruhi wote hao wamenyoa mtindo huo.
Alama nyingine wanayotumia kudai kuwa ni ndugu zao, ni kusema wana miguu mikubwa ilihali wagonjwa wote hao miguu yao imevimba.
Baada ya kutokea ajali hiyo ambayo hadi sasa watu waliofariki dunia wamefika 76, Rais Dk. John Magufuli alifika hospitalini hapo kuwafariji majeruhi.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alitangaza kutoa Sh 500,000 hadi milioni 1 kwa kila majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, Meneja Vinasaba kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Khadija Mwema, alisema uchunguzi huo utashirikisha ndugu wa karibu ili kuondoa utata uliopo sasa.
Alisema utafiti unaonyesha ulinganishi wa kitaalamu unaleta zaidi matokeo mazuri ya sampuli endapo watajitokeza zaidi watoto au wazazi ambao hurahisisha utambuzi.
“Kitaalamu sampuli hizi ni rahisi katika utambuzi, ila kama hakuna watoto au wazazi huwa tunapendekeza kutumia kaka, baba mdogo au dada ili kupata usahihi wa vinasaba,” alisema Khadija.
Alisema ofisi yao inaendelea kuchukua vinasaba ili kuondoa utata unaoibuka hivi sasa wa utambuzi wa majeruhi, hasa walio mahututi.
Akizungumzia majeruhi hao, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema awali walipokea 46 na nane wamefariki dunia hadi sasa.
Alisema wengine 38 wamelazwa wodini ambao kati yao 25 wameanza kujitambua na 13 wamelazwa chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU).
Aligaesha alisema tangu watangaze watu kujitokeza kutambua ndugu zao, wengi wameanza kujitokeza huku kukiwa na changamoto kadhaa zinazojitokeza.
Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ndugu zaidi ya mmoja ambao hawafahamiani kung’ang’ania mgonjwa mmoja, kila mtu akitaja alama zake.
“Wengi wanaokuja wanatwambia huyu mimi ni ndugu yangu na mwingine hivyo hivyo, ukiwaambia wataje alama, kila mmoja anakwambia alinyoa kiduku wakati walio mahututi wote 13 wamenyoa hivyo.
“Alama nyingine ambayo inatajwa na ndugu hao ni miguu mikubwa, sasa tunashindwa kuielewa ni miguu mkubwa wakati wote wamevimba miguu, hivyo tumeamua kutupilia mbali vigezo vyote hivyo.
“Jambo hili linatupa ugumu na ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya utambuzi ili kuondoa utata uliopo na tuweze kuwatambua ndugu halisi wa wagonjwa hawa,” alisema Aligaesha.
Alisema sababu kubwa iliyowafanya wawashirikishe Ofisi ya Mkemia mkuu ni kwa sababu majeruhi hao wameungua kwa asilimia 80 hadi 95.
KITENGO CHA DAMU SALAMA
Katika hatua nyingine, Ofisa Mhamasishaji Damu Kitengo cha Damu Salama Jiji la Dar es Salaam, Dk. John Daniel, alisema wanakabiliwa na upungufu wa damu.
Dk. Daniel alisema katika Hospitali ya Muhimbili na Mloganzila kwa siku wanatumia chupa 120 hadi 180 za damu.
Alisema asilimia 100 ya majeruhi wa moto wanakuwa wamepoteza maji mwilini.
Dk. Daniel alisema wakipokea damu kutoka kwa wachangiaji, huingizwa kwenye mashine maalumu ambayo huchuja na kupata majimaji (plazma), ambayo hutumika kwa majeruhi wa moto.
“Chembechembe nyekundu wanatumia wanaokabiliwa na upungufu wa damu na ile ya chembe sahani hutumika na wagonjwa wa saratani.
“Majeruhi wa moto asilimia 90 hupewa majimaji ya damu ambayo yakichujwa kutoka kwa wachangiaji yana uwezo wa kuhifadhiwa mwaka mmoja bila kuharibika,” alisema Dk. Daniel.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujitolea damu huku akisisitiza wachangiaji watumie vinywaji laini kama juisi, maji na matunda na kuachana na imani potofu kuwa bia ndiyo inayochangia kuongezeka damu kwa wingi.
Pia, Mufti Sheikh Abubakar Zubeir alifika Muhimbili na kutembelea wodi waliolazwa majeruhi hao kwa lengo la kuwajulia hali na kufanya nao ibada.
Wakati huohuo, zaidi ya vijana 500 wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, wamejitokeza Muhimbili kuchangia damu.
Akizungumzia tukio hilo, Ulega ambaye aliongozana na vijana 50 kutoka Mkuranga, alisema ni vyema wananchi wakajenga mazoea ya kuchangia damu kwakuwa kuna upungufu mkubwa wa damu nchini.
Alisema binadamu yeyote anayepungukiwa damu, hakuna kitu mbadala zaidi ya kuongezewa nyingine, hivyo ni muhimu kujenga mazoea ya kujitolea damu ili kuokoa maisha ya jamii nzima.
“Kama kiongozi nitaendelea kuhamasisha uchangiaji damu, kwani natambua thamani ya wenzetu waliopata ajali hiyo na ili wapate nafuu na kurejea kwenye majukumu yao ya kila siku, ni lazima kila mtu aguswe kwa nafasi yake,” alisema Ulega.