Na Ahmed Makongo-BUNDA
KUANZIA mwaka 2008 hadi mwaka 2018 jumla ya majangili 4,337 yamekamatwa na askari wa wanyama pori wa kampuni ya Grumeti Reserves, katika mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo, pamoja na pori la wananchi la Ikona, yaliyoko pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Grumeti Reserves, Ami Hamidu Seki, wakati akiwasilisha mada katika Mkutano Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara, ambapo alisema kuwa katika kipindi hicho kampuni hiyo ilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kufanya jumla ya doria 54, 335 ambapo waliyakamata majangili hao.
Alisema kuwa majangili hayo tayari yalikuwa yameshaua wanyama mbalimbali wapatao 2,929, kwa kutumia silahajadi zikiwemo nyaya zipatazo 23,314.
“Kampuni yetu imeshapata mafanikio mengi ya uhifadhi wa wanayama pori, kwani kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2018, tulifanikiwa kukamata majangili 4,337 ambayo tayari yalikuwa yameshaua wanyama mbalimbali,” alisema.
Aidha, alisema kuwa katika kipindi hicho pia walikamata mifugo ya wananchi iliyoingizwa katika mapori hayo ipatayo 275,657, ambapo wamiliki wa mifugo hiyo serikali iliwapiga faini ya jumla ya Sh milioni 255.98
Aliongeza kuwa pia mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka idadi ya wanyama katika mapori hayo kutoka wanyama 15,233 mwaka 2003 na kufikia wanyama 36,321 mwaka jana.
Alifafanua kuwa mwaka 2003 wanyama aina ya nyumbu walikuwa 605 na mwaka jana wamefikia 7,709, pofu walikuwa 254 na wamefikia 1,116, tembo walikuwa 355 na kufikia 1,116, twiga 331 na wamefikia 759, kongoni 189 wamefikia 289, swala pala 7,147 wamefikia 9,826, nyamera 5,705 wamefikia 11,995, ngiri 435 wamefikia 2,494.
Akizungumzia hali ya ujangili, alisema kuwa bado ni changamoto kubwa kwani pamoja na kufanya doria za mara kwa marana kuyakamata lakini bado ujangili unafanyika.
Kwa uapande wake Ofisa Utalii wa Hiofadhi ya Taifa Serengeti, Fred Shirima, alitoa wito kwa waandishi wa habari kufanya utalii katika hifadhi hiyo na kupiga picha kwa ajili ya kutengeneza makala jambo ambalo litasaidia kuitangaza hifadhi hiyo.
Wakati huo huo, mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima, aliyekuwa mgeni rasimi katika mkutano huo, aliutaka uongozi wa kampuni ya Grumeti Reserves, pamoja na hifadhi ya taifa ya Serengeti, kuwatumia waandishi wa habari walioko mkoani humo, kwa ajili ya kutangaza mambo ya kimaendeleo wanayoyafanya katika jamii inayowazunguka na nchi kwa ujumla.