Na MURUGWA THOMAS,
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia duka na kupora Sh milioni 22 na vocha za simu za mitandao tofauti zenye thamani ya Sh milioni 47 mali ya mfanyabiashara Revocatus Zunza wa mjini Tabora.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Khamis Issa alisema tayari polisi wanafanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika na uvamizi huo ikiwa ni pamoja na kuwatia mbaroni.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Aprili 16, mwaka huu katika mtaa wa Jamhuri katikati ya mji wa Tabora siku ya Sikukuu ya Pasaka wakati mmiliki wa duka hilo akiwa kwenye mapumziko ya Pasaka.
Duka lililovunjwa na kuibwa lipo mkabala na ilipo sanamu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere eneo la soko kuu la mjini Tabora jengo ambalo linamilikiwa na familia ya marehemu Dk. Othman.
Mmiliki wa duka hilo, Revocatus Zunza ambaye ni wakala wa kuuza vocha za jumla wa makampuni mbalimbali ya simu za mkononi, alisema aligundua wizi huo Jumatatu asubuhi alipofika kufungua duka.
Zunza alidai watu waliohusika na wizi huo inaonekana waliingia ndani ya duka lake kupitia chumba cha jirani ambacho kilivunjwa tofali za moja la ukuta wake na kuiba fedha na vocha.
“Siku ya tukio nilipita eneo hili nikitokea kanisani, nilikuta mlango wa chumba cha jirani ambacho mpangaji wake hatujawahi kuonana ukiwa wazi.
“Nje kulikuwa na mmiliki wa jengo na watu ambao walionekana kufanya ukarabati, sikutilia shaka nadhani inatia shaka,” alisema.
Baadhi ya watu wanaofanya biashara jirani na eneo la tukio wamedai kuwa Jumamosi ya Aprili 15, mwaka huu waliwaona watu wakifungua mlango wa chumba hicho.
Walisema watu hao waliingiza ndani mitungi ya gesi kitendo hicho hakikuwashutua kwa vile wananchi wengi hufanyia shughuli zao hapo.