28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Waliozembea ajali ya lori la mafuta wachukuliwe hatua

Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo katika tukio la ajali ya moto iliyotokea Agosti 10, mwaka huu mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 104, majeruhi na uharibifu wa mali.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, jijini Dodoma ambalo limeahirishwa hadi Novemba 3.

“Baada ya tukio hilo la kusikitisha, tarehe 12 Agosti 2019 niliunda kamati maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru madaktari, wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.

 “Nawasihi Watanzania wenzangu tujifunze kutokana na ajali hiyo iliyotokea Morogoro, na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika maeneo ya ajali.

“Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada kwa waathirika wa ajali badala ya kutumia kama fursa za kujinufaisha isivyo halali,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania kutumia fursa ya upungufu wa nafaka katika nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuzalisha zaidi mazao hayo ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba zaidi.

Alisema hali ya usalama wa chakula katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imetetereka kutokana na athari mbalimbali, ikiwemo ukame katika upande wa magharibi wa ukanda, mvua zilizokithiri, mafuriko na vimbunga vya Idai na Kenneth pamoja na wadudu waharibifu wa mazao na magonjwa.

“Athari hizo zimesababisha uzalishaji wa nafaka kama mahindi, mtama, mpunga, ngano na ulezi ndani ya SADC upungue kwa asilimia 14 kutoka tani milioni 42.6 mwaka 2018 hadi tani milioni 36.8 mwaka 2019.

“Hata hivyo, Tanzania na Afrika Kusini kwa kipindi hicho zilizalisha ziada ya mazao hayo ambayo yanakadiriwa kukidhi mahitaji kwa mwaka 2019/2020,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles