33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo saratani ya matiti kuongezeka kwa asilimia 80 mwaka 2030

Tunu Nassor -Dar es salaam

VIFO vitokanavyo na ugonjwa wa saratani ya matiti vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashine mpya ya uchunguzi wa saratani uliofanyika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Daisy Majamba, alisema ugonjwa huo bado ni tishio kwa wanawake.

Alisema inakadiriwa ifikapo 2030 idadi ya wagonjwa wapya itaongezeka kwa asilimia 82 jambo ambalo linahatarisha ustawi wa afya nchini.

“Tusipochukua hatua mapema za tahadhari, hali ya saratani ya matiti inaweza kuwa mbaya zaidi, ndiyo maana Serikali inashirikiana na sekta binafsi kulitatua,” alisema Daisy.

Alisema saratani ya matiti kwa sasa inashika nafasi ya pili kati ya saratani zinazosababisha vifo zaidi ukiacha ile ya mlango wa kizazi.

“Tunahitaji kuwajengea uwezo Watanzania, hasa kwa kutoa elimu ya ufahamu wa ugonjwa huo kwa wanafunzi mashuleni ili kuwe na uelewa wa kutosha katika jamii,” alisema Daisy.

Aliipongeza Hospitali ya Aga Khan (AKHS) kwa kununua mashine mpya ya uchunguzi wa saratani ambayo ina teknolojia ya kisasa ya 3D.

“Tunaamini kuwa kwa kupata mashine hii itasaidia kupunguza tatizo ambalo linaonekana kuongezeka kila kukicha,” alisema Daisy.

Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Afya wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Sulaiman Shahabuddin, alisema wataendelea kuwekeza kuhakikisha matibabu ya kisasa yanapatikana nchini.

“Tulikuwa wa kwanza kufunga mashine ya RMI, baadaye RIS na mashine nyingine nyingi zenye teknolojia za kisasa, na sasa tumeleta hii ili kuboresha huduma za afya nchini,” alisema Shahabuddin.

Daktari Bingwa wa Radiolojia wa AKHS, Dk. Pili Ally, alisema mashine hiyo itasaidia uchunguzi zaidi wa saratani ya matiti kwa kuwa inamwezesha daktari kuona ndani zaidi ya kipimo cha awali cha 2D kwa kuwa ina kifaa cha ziada.

“Mashine hiyo ni ya kwanza kwa Tanzania na Afrika ya Mashariki, na ya pili kusini mwa Afrika. Awali ilipatikana Afrika Kusini pekee,” alisema Dk. Pili.

Alisema mashine za awali zilikuwa na maumbile ya kutisha ambayo huwaogopesha wanawake na kuwafanya washindwe kufanya vipimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles