24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Shughulikieni ubadhirifu bila kuoneana haya

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

WAZIRI  Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri na Manaibu Mawaziri kushughulikia ubadhirifu mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa muda mrefu.

Amesema hatua zichukuliwe bila kuoneana haya kama kuna ushahidi wa wazi kabla hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajakagua au viongozi wa juu kuchukua hatua.

Pia, amewataka kuepuka  matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa  chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Oktoba 29, 2021 wakati alipofungua Mafunzo ya Uongozi kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

“Ubadhirifu unatakiwa ushughulikiwe mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa muda mrefu na hatua zichukuliwe bila kuoneana haya kama kuna ushahidi wa wazi kabla hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajakagua au viongozi wa juu kuchukua hatua,”amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Mawaziri hao kuepuka matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali.

Amesema upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika Mawaziri hao wanahitaji  kupatiwa wasaidizi hao hivyo amewataka kuzingatia utaratibu huo na si vinginevyo.

Vilevile, amewaagiza wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukemesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora.

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote,”amesema.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.

Vilevile, amewataka viongozi hao kutumia mada zitakazowasilishwa ili ziweze kuwasaidia katika kuzisimamia vyema Wizara wanazoziongoza na taasisi zilizo chini ya wizara zao.

”Mwende mkazisaidie taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote. Nendeni mkawe msaada kwao,” amesema.

Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kwa kushirikiana na Taasisi zingine waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.

“Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini.

“Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila ubaguzi wa jinsia, kabila, dini na rangi ili mradi mtu hajavunja sheria. Tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa,” amesema Majaliwa.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Management ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ameiagiza Taasisi ya Uongozi ihakikishe inaendelea kuandaa mafunzo ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini, hususan ile inayosimamiwa na Ofisi ya Rais.

Amesema kikao hicho ni muhimu hivyo anatoa rai kwa  Wizara,Taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinawapitisha watendaji wake katika mafunzo yanayoandaliwa na Taasisi za uongozi hapa nchini.

“Jambo lingine ni Idara,Wizara,wakala wa Serikali kuhakikisha zinatenga bajeti ili kupelekwa kwa watumishi katika mafunzo ya taasisi ya uongozi pamoja na watumishi wa kada za chini, tunaamini baada ya mafunzo haya tutaimarisha maadili ya kiutendaji kwa kutengeneza utaratibu mzuri kwa kuzingatia kanuni taratibu  pamoja na sheria na miongozo ya Nchi,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles