26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa mgeni rasmi mahafali waliosoma nje

Na Mwandishi Wetu–Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya pili ya kimataifa kwa wanafunzi waliosoma nje ya nchi yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki Mlimani City, Dar es Salaam.

Mahafali hayo yanatarajiwa kuwakutanisha wanafunzi 400 waliosoma vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kupitia taasisi ya elimu nje ya nchi ya Global Education Link (GEL).

Mkurugenzi wa (GEL), inayowaunganisha wanafunzi na vyuo vikuu nje ya nchi, Abdulmalik Mollel akizungumza jana kwenye kikao cha maandalizi ya mahafali hayo, alisema lengo ni kuhakikisha wanafunzi Watanzania waliosoma nje ya nchi hawarudi kimya kimya na kinyonge kwani wao ni wazalendo walioamua kuacha fursa zilizoko huko baada ya masomo yao na kuja kuijenga nchi yao.

Mollel alisema wahitimu hao waliaminiwa na taifa na ndiyo sababu walipewa viza za kwenda kusoma nje ya nchi kwa manufaa yao, familia zao na nchi yao, hivyo kurudi kwao ni kurejesha furaha nyumbani kwani wanatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa nchi.

Alisema GEL itawakutanisha wanafunzi hao kujenga mtandao na taasisi na watu mbalimbali hapa nchini baada ya kukaa nje ya nchi kwa muda mrefu ambako huko walishajenga aina nyingine ya maisha.

“Mfano mtoto ameenda huko akiwa na miaka 17, amekaa huko miaka minne au sita, anarudi amekuwa mtu mzima, amekuta mambo mapya, sasa akifika akikosa timu kama aliyokuwa nayo kule anakata tamaa.

“Sasa kitendo cha kuwakutanisha watu waliokuwa Uingereza, India, China, Canada au Afrika Kusini kwenye jengo moja ni jambo kubwa sana na la msingi,” alisema Mollel.

Aidha, alisema wanafunzi hao wakikutanishwa wataona kama milango ya maisha yao imefunguliwa kwani watatengeneza mtandao mpya na wenzao waliomaliza nao mwaka mmoja kwenye vyuo hivyo nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mollel, mahafali hayo ni fursa kwa wahitimu hao kwani kuna kampuni mbalimbali ambazo zimetoka kwenye nchi ambazo wanafunzi hao walisoma ambazo zitakuwa zinatafuta wataalamu wa fani wanazozihitaji hivyo wakikutanishwa itakuwa na manufaa kwao.

“Kuna wawekezaji ambao wanatafuta watu waliosoma kwenye nchi zao angalau wenye kujua lugha zao kidogo, sasa hii ni nafasi ya kuwaita hawa kwamba nani amewekeza nini na anahitaji vijana wataalamu sasa ukiwakutanisha ni fursa kubwa sana kwa wawekezaji na vijana,” alisema Mollel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles