26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Wagonjwa 11 wafanyiwa upasuaji wa uvimbe

Na CLARA MATIMO-MWANZA

WAGONJWA 11 wasiojiweza wamepatiwa huduma ya upasuaji baada ya taasisi ya kimataifa ya Lions Club kuwalipia gharama zinazofikia Sh milioni mbili.

Taasisi hiyo yenye makao yake nchini Marekani inayojishughulisha kusaidia watu  wasiojiweza, imewezesha upasuaji huo kwenye Hospitali ya Bukumbi  iliyopo Wilaya ya Misungwi kupitia tawi lake la mkoani Mwanza.

Akizungumza hospitalini hapo alipokwenda kuwaona wagonjwa hao mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, aliiomba taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali  ili kupunguza changamoto zilizopo katika jamii.

“Lions Club imekuwa ikifadhili mambo mengi katika jamii yetu kwa ajili ya kusaidia  changamoto ambazo  inakabiliana nazo, niwaombe muendelee kuwa na moyo huo, mmekuwa wadau wakubwa sana kwa maendeleo ya taifa, mnajitoa sana, naamini na taasisi zingine zitafuata nyayo zenu,” alisema Mongela.

Rais wa Lions Club Tanzania, Bakari Omar alisema wanavutiwa na jinsi ambavyo hospitali hiyo inavyothamini kwa kutunza misaada wanayoitoa  na jinsi inavyowafikia walengwa maana walijenga wodi  zaidi ya miaka 30 iliyopita,  lakini hadi leo bado inahudumia wagonjwa.

Kwa upande wake, Rais wa Lions Club Tawi la Mwanza, Mahesh Choudhary, alisema wanayapa kipaumbele magonjwa ya upasuaji kwa sababu ni hatarishi  kwani mgonjwa asipofanyiwa upasuaji kwa wakati  athari  zake ni kubwa anaweza kupoteza maisha.

 “Unapokuwa na uvimbe sehemu yoyote ya mwili ni hatarishi kwa sababu usipopata matibabu  ya upasuaji haraka  athari zake ni kubwa  ndiyo maana klabu yetu tukaona tujikite sana kwenye eneo hilo ila tunatoa msaada wa elimu na mahitaji mengine,” alisema Choudhary.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bukumbi, Dk. Suzan Charles, alisema  wagonjwa hao 11 wamefanyiwa upasuaji mbalimbali ikiwemo kina mama  kutolewa uvimbe kwenye kizazi,  tezi dume, macho, koo na meno na wote wanaendelea vizuri.

Baadhi ya wanufaika akiwemo Mariana Gervas na Perepetua Simon, walisema wamesumbuliwa na maumivu muda mrefu, lakini walishindwa kumudu gharama za matibabu kwa sababu wana vipato vya chini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles