24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa azindua mwongozo wa uwekezaji Iringa

Na Mwandishi Wetu, Iringa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Iringa katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Mkwawa.

Akizungumza jana Jumamosi, Januari 23, katika tukio hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba Serikali itaendelea kudumisha amani na utulivu ambao ni muhimu kwa wawekezaji na wananchi hivyo wawekezaji wa ndani na nje wasisite kuwekeza nchini.
 
Amesema uwekezaji ni tegemeo la Taifa katika kukuza uchumi na kuongeza ajira, hivyo serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa Watumishi wa Umma wanaohusika na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kwa lengo la kuhakikisha kuwa hawasumbuliwi na pale ambapo hawatohudumiwa vizuri ikiwemo kutozwa gharama za ziada watoe taarifa kwa mamlaka husika.

“Katika ziara zangu za mikoani nimesisitiza sana umuhimu wa watumishi wa umma kuwatumikia wananchi wote kwa usawa na bila ubaguzi. Aidha, nimeagiza Wananchi wote na wageni wakiwemo Wawekezaji wanapofika kwenye Ofisi zote za Umma, wapokelewe kwa staha, wasikilizwe na kupewa huduma wanazohitaji kwa uharaka na ufanisi bila urasimu,” amesema Majaliwa.
 
Alisema mwongozo huo aliouzindua umebainisha vivutio vilivyoko mkoani Iringa ikiwemo mazingira mazuri ya biashara, nguvu kazi, amani na utulivu, maliasili nyingi na soko la kutosha.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa uandaaji wa mwongozo huo wa uwekezaji na amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania wajipange vizuri katika kushindana Kimataifa kwa kuzalisha bidhaa bora.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alisema lengo la kongamano hilo la uwekezaji mkoani Iringa ni kuanisha fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Iringa na kuzitangaza ili ziweze kutambulika na kuvutia wawekezaji wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles