30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa azindua mkakati mpya kudhibiti Ukimwi

Na SARAH MOSES, DODOMA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/2019 hadi mwaka 2022/2023 unaotarajia kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023.

Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU kwa watoto kwa chini ya asilimia tano ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia mbili ifikapo mwaka 2030.

Akizindua mkakati huo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika kitaifa Dodoma jana, alisema matayarisho yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2013/2014 hadi mwaka 2017/2018.

Mbali na matokeo hayo, pia alisema mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70 ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo mwaka 2023 na kuelekea kuutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Alisema mkakati huo umepanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwamo afua zinazotekelezwa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi (PEPFAR).

“Pia Mfuko wa Dunia wa Kudhibiti Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) na jitihada nyingine za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi mbalimbali.

“Ili kupata matokeo mazuri tunapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kufuata na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa,” alisema.

Alisema maadhimisho hayo husaidia kubaini changamoto, mafanikio na kuja na mikakati ya kupambana na maambukizi ya VVU na Ukimwi.

“Siku hii hutoa fursa kote duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano ya Ukimwi katika jamii zetu,” alisema.

Pia alisema kiwango cha upimaji wa Ukimwi bado hakiridhishi hasa kwa upande wa wanaume kwa kuwa ni asilimia 45 tu waliojitokeza kupima afya zao.

Katika hatua nyingine, aliagiza mikoa yote kufanya uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu katika ngazi za mikoa na hata wilaya.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika mikoa yote nchini jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU, wakiwamo wanawake 136,389 na wanaume 125,725.

“Natoa wito kwa mikoa na wilaya zote kuwa kampeni hii iwe endelevu. Viongozi katika ngazi mbalimbali tuungane katika uhamasishaji wa jambo hili kwa sababu vita dhidi ya VVU na Ukimwi inahitaji dhamira ya dhati na tafakuri ya kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya,” alisema.

Pia alisema Serikali itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa VVU, kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles