Mwandishi Wetu, Arusha.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo amezindua maabara ya kisasa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, iliyojengwa na Serikali kugharimu zaidi ya Sh bilioni 2.3.
Akizindua maabara hiyo, Waziri Majaliwa amewataka wanafunzi, taasisi na mashirika mbalimbali kutumia maabara hiyo ili kuwezesha sekta ya sayansi kukua zaidi kwani serikali inaendelea kujenga maabara za sayansi katika shule mbalimbali pamoja na kuajiri walimu wa masomo ya sayansi.
Aidha, amesema sekta ya nyuklia ikitumiwa vizuri inaweza kuleta maendeleo katika sekta ya viwanda kwani serikali inaweka mkazo zaidi katika sekta ya viwanda kwa ajili ya kuinua uchumi ifikapo 2025.
“Serikali imejenga maabara hii ili kuhakikisha usalama wa wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi ya  kinyuklia.
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuhakikisha maabara hii inajengwa nchini kwani ni ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Bara la Afrika,” amesema.
Wakati huo huo, Majaliwa amefungua mkutano wa Wataalamu wa Mionzi kutoka nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), katika Kituo cha Mikutano cha Kimtaifa cha Arusha (AICC).
Umoja wa Ulaya (EU), umefadhili bila ya masharti kwa serikali ya Tanzania vifaa na mafunzo kwa wataalamu watakaosimamia maabara hiyo kwa gharama ya Sh milioni 6.6 ambapo maabara hiyo itatoa huduma katika nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Nchi za SADC.