26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ATOA MAAGIZO TISA

GABRIEL MUSHI NA ESTHER MBUSSI – DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amehitimisha Mkutano wa Tisa wa Bunge kwa kutoa maagizo tisa kwa mawaziri, wabunge na maofisa masuhuli.

Baadhi ya mawaziri waliolengwa na maagizo hayo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamisi Kigwangala, aliyetakiwa kuongeza kasi ya kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Maliasili ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi wa Taifa.

Pia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kukamilisha kazi ya kusambaza mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa wadau wote ili kuwezesha wizara, mikoa na mamlaka za serikali na taasisi zote za umma kuanza mchakato wa kuandaa mpango wa bajeti wa mwaka 2018/19.

Majaliwa ametoa maagizo hayo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, ambapo watunga sheria hao wanatarajiwa kukutana tena kwenye mkutano wa 10 Januari 30, mwakani.

Akizungumzia ya Sekta ya Maliasili na Utalii, Majaliwa alisema, Serikali imeboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia njia za kielektroniki, ambapo sasa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 60.1 mwaka 2014/15 na  kufikia Sh bilioni 102 mwaka 2016/17.

“Lakini juhudi mbalimbali zimesaidia kupata ongezeko la watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,284,279 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 12.9.

“Kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi bilioni mbili mwaka 2016,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Dk. Kigwangala kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza na kuendeleza fukwe ambazo hazina shughuli.

Aidha, Majaliwa aliwaagiza viongozi na watendaji wote wa serikali kuzingatia kikamilifu mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya mwaka 2018/19 ili kuendeleza mafanikio ya serikali ya awamu ya tano.

Kuhusu maandalizi ya bajeti kwenye halmashauri, alisema: “Naomba kutumia fursa hii kuwasihi wabunge kwa nafasi zao kama wajumbe wa mabaraza ya madiwani kwenye halmashauri za majimbo yao, wawasaidie kutoa elimu na ufafanuzi kuhusu mchakato wa maandilizi ya mpango wa bajeti wakati wa baraza la madiwani.

“Aidha, nawaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wazingatie miongozo hii iliyotolewa na wawashirikishe wananchi na sekta binafsi katika kupanga mipango ya maendeleo ya maeneo yao.”

Akitoa maagizo kwa maofisa masuhuli kuhusu Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2018/19 na mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya mwaka 2018/19, alisema: “Wazingatie ukusanyaji wa mapato ya ndani, wahakikishe makusanyo yote yanawekwa kwenye mfuko mkuu wa serikali.

“Kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato, kuhakikisha zabuni za watoa huduma na makandarasi zinatolewa kwa wanaotumia mashine za kielektroniki (EFDs) na kuhakikisha kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na kutoa gawio stahiki kwa Serikali.

“Wadhibiti matumizi na kupunguza gharama. Maofisa masuhuli wahakiki watumishi ili kuhakikisha mishahara inalipwa kwa watumishi wanaostahili.”

Aidha, aliagiza uhakiki wa kina uendelee kufanywa kwa waliokwama madaraja ili wapandishwe na malimbikizo ya watumishi yabainishwe, ikiwa ni pamoja na madeni ya watumishi kuwekwa vizuri ili kufikia hatua ya kulipa.

“Pamoja na hayo, maofisa masuhuli waendelee kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa taasisi za Serikali ili kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha taasisi za Serikali zinajiendesha kibiashara, zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

“Kulipa na kuzuia ongezeko la madeni ya Serikali. Maofisa masuhuli wote wahakikishe madai ya watoa huduma yote yamehakikiwa na mkaguzi mkuu wa ndani wa serikali na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika.

“Kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha na kuzingatia matumizi ya hati ya ununuzi zinazotolewa kwenye mfumo wa malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa madai,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles