24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA MADINI, BUNGE LAGEUKIA GESI, SAMAKI

ESTHER MBUSSI NA GABRIEL MUSHI

BAADA ya Bunge kuunda kamati za kuchunguza biashara ya madini ya tanzanite na almasi, sasa limeunda tena kamati ya kuchunguza sekta ya gesi na uvuvi wa bahari kuu, maeneo ambayo yanatajwa kupotezea Serikali mapato kama ilivyo kwenye madini.

Jana Spika wa Bunge, Job Ndugai, akitangaza wenyeviti wa kamati hizo, alisema ile ya gesi itaongozwa na Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Tanzanite ambayo ripoti yake ilimfanya Rais John Magufuli kuagiza eneo lote la migodi ya Mirerani lizungushiwe uzio, huku ikielezwa kuwa, sasa mapato ya madini hayo yamepanda.

Kwa upande wa Kamati ya Kuchunguza Sekta ya Uvuvi, Ndugai alisema itaongozwa na Anastazia Wambura, huku akisema ameona ni busara kwa mara ya kwanza kamati teule ya Bunge iongozwe na mwanamke.

Ndugai alisema uamuzi huo unatokana na kusuasua kwa sekta hizo, ambapo Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu kuna zaidi ya Sh bilioni 400 ambazo zinapotea bure, huku sekta hiyo ikichangia pato la Taifa kwa asilimia 1.4, ambayo ni sawa na Sh bilioni 3.2.

Ndugai alisema kanuni ya 5 (1) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, inampa madaraka ya kuunda kamati kwa kadri atakavyoona inafaa, hivyo anaunda kamati hizo ili kupata sababu za msingi za sekta hizo kuzorota.

Alisema ukubwa wa ukanda wa bahari katika uvuvi wa Tanzania unalingana na nchi ya Namibia, ambayo yenyewe inaingiza pato kwa asilimia 10.

Ndugai alitaja wajumbe wa Kamati ya Uvuvi kuwa ni Musa Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud Salim Abdalah, Tauhida Nyimbo na Mbaraka Dau.

Wengine ni Dk. Immaculate Semesi, Dk. Christina Ishengoma, Stanslausi Mabula, Mussa Mbarouk na Cosato Chuma, ambao wataongozwa na Mwenyekiti wao, Anastazia Wambura.

Wajumbe wa Kamati ya Gesi alisema watakuwa ni Innocent Bashungwa, Dastan Kitandula, Dk. Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa na Ruth Moleli.

Wengine ni Richard Mbogo, Omari Kigua, Abdala Mtolea na Sebastian Kapufi na Mwenyekiti wake Dotto Biteko.

Ndugai alimwagiza Katibu wa Bunge kuangalia namna ya kuwawezesha wabunge hao ili watekeleze majukumu yao ambayo watayafanya kwa siku 30. Alisema kamati hizo zitaanza kazi pale zitakapoarifiwa na Katibu wa Bunge.

Pia Spika amesema atawachongea mawaziri kama watashindwa kupeleka bungeni muswada wa sheria inayotambua Dodoma ni makao makuu ya nchi.

“Mmetupiga danadana sana, hivi ni nani aliyekalia muswada huo ama mnataka siku moja muamue kwenda Dar es Salaam tena, nasema kama bado nimekalia kiti hiki hakuna mtu ataweza kupenyeza ajenda hiyo,” alisema Ndugai.

Kiongozi huyo alisema mawaziri wamekuwa wakilidanganya Bunge kila wakati kwamba muswada huo unapelekwa bungeni, lakini jambo hilo halitekelezwi.

Alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali ahakikishe muswada huo unasomwa kwa mara ya kwanza kwenye Mkutano wa 10 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 30, mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles