26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ATAKA MIPAKA IHESHIMIWE KUEPUKA MIGOGORO YA ARDHI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

Na MOHAMED HAMAD -Kiteto

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuheshimu mipaka ya kiutawala na kuacha kuhamisha alama ili kuepuka migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Hatua hiyo imetajwa kuwa suluhisho la mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu, huku ukigharimu maisha ya watu, gari na mtambo wa maji kuteketezwa kwa moto.

Majaliwa alitoa onyo hilo jana wakati akiwa mpakani mwa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara na Kilindi mkoani Tanga.

Alisema mipaka hiyo imelenga kusaidia watawala kuongoza nchi.

Majaliwa alisema Serikali inautambua mpaka wa Kiteto na Kilindi wa mwaka 1961 wenye GN namba 65, na alisisitiza kuwa kamwe hautabadilika bali utaboreshwa.

Alisema mpaka huo utatafsiriwa kwa wananchi ili waweze kuelewa huku akiwaonya baadhi ya watumishi wa Serikali kutumia migogoro hiyo kujinufaisha.

Aidha aliwataka wakuu wa mikoa ya Manyara na Tanga kusimamia amani hadi Serikali itakapokamilisha kuweka alama upya zilizong’olewa, huku akiwataka wakulima na wafugaji kuendelea na shuguli zao bila kubughudhiwa.

“Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa mgogoro wa mpaka umeanza kushughulikiwa kwa kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya za Kiteto na Kilindi, wabunge, wenyeviti wa halmashauri na madiwani kuhakikisha wanasimamia agizo hilo la Serikali ili wananchi waishi kwa amani,” alisema.

Awali Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, alisema kazi ya kuweka alama hizo itaanza mapema wiki ya kwanza ya mwezi Februari ili kupunguza madhara wanayopata wananchi katika maeneo yao.

Naye Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Geoge Simbachawene, alitaka wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya tano, kwakuwa ina nia njema katika kuwatatulia matatizo yao huku akisisitiza kuwa  watumishi watakaobainika kuwa chanzo cha migogoro hiyo hawatakuwa na nafasi katika Serikali hiyo.

Awali wananchi wa Kijiji cha Mafisa wilayani Kilindi, waliweka mpaka wao kwa kutenganisha Mkoa wa Tanga na Manyara, baada ya mgogoro wa ardhi kati yao na wenzao wa Kijiji cha Lembapuli kilichopo wilayani Kiteto na kusababisha madhara.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kiteto, Emmanue Papian (CCM), aliwahakikishia wananchi wa Kiteto na Kilindi kuwa watafuata maagizo ya Serikali ambayo yametolewa na Waziri Mkuu ikiwa ni ufumbuzi wa mgogoro kati ya wilaya hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles